29.7 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

BODABODA ZINAOGOPWA ZAIDI KULIKO  HATA MAGARI

LICHA ya kutoa ajira kwa vijana wengi hapa Tanzania, usafiri wa Pikipiki maarufu kama Bodaboda umegeuka na kuwa hatari na wa kuogopwa zaidi kuliko hata magari binafsi au  yale ya usafiri wa umma yaani Daladala.

Abiria wa Mwendo Kasi ni miongoni mwa watu walionufaika na faida za usafiri wa Bodaboda kama abiria na kushuhudia jinsi Pikipiki zinavyoogopwa zaidi na watembea kwa miguu kuliko magari yote yapitayo barabarani.

Kinachofanya Bodaboda ziogopwe na abiri watembeao kwa miguu ni kasi yao hata pale ambapo panahitaji wasimame ili watumia barabara wengine wapite, wao hukatisha na kusababisha hofu kwa raia kwa kuwa nafahamu hakuna mtu anayetaka kupoteza kiungo au maisha katika ajali kizembe.

Siyo madereva wote wa Bodaboda wana tabia hiyo. Wengine ni wastaarabu na wanafuata sheria za barabarani ili kunusuru maisha yao na ya abiria wengine, lakini madereva wengine  wavunjifu wa sheria  na sidhani kama walipita VETA au chuo chochote kunoa ujuzi wazo wa kuendesha vyombo vya moto.

Bila shaka wamefundisha wao kwa wao, wanaachia Pikipiki kisela tu na mabosi nao wanawakabidhi vyombo vya moto madereva ambao wanafahamu kabisa hawana ujuzi, ila kwa kuwa ni ndugu au wanafahamiana, wanapeana dili ambazo zimekuja kuwa majanga.

Abiria wa Mwendo Kasi mara kadhaa nimeshuhudia mazingira ya kutokea ajari katika makutano ya barabara kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam. Ila hii inatokea sana pande za Ubungo pale wanapopaita mataa.

Muda mwingine kunakuwa hakuna Trafiki, hivyo taa huongoza vichwa ngumu vya baadhi ya madereva wa Bodaboda ambapo nadhani wamejifunzia udereva huku uchochoroni na mara nyingi hufanya kazi hiyo kama Deiwaka.

Mfano taa zinasimamisha magari yanayotoka Kimara kwenda Posta ili magari yanatoka Mwenge kwenda Mbagala yapite. Lakini utaona dereva wa Bodaboda anayetoka Kimara anakatiza haraka akiwa amebeba abiria katikati ya magari yanatoka Mwenge kwenda Mbagala hali inayopunguza usalama wake na abiria aliyempakiza.

Muda mwingine magari yote husimama ili watembea kwa miguu wapite, Bodaboda anakatisha katikati yao na kufanya hofu itawale kwa hawa raia, wanaogopa bodaboda kuliko wanavyoogopa magari.

Maana wenye magari eneo kama lile hawawezi kufanya uzembe ila hawa Bodaboda kwa vile wanajihisi ni wadogo basi wanaweza kupenya sehemu yoyote ile hata kama ni hatari kwao.

Kwao inaweza isiwe ishu sana kwa sababu kasi kwake nd’o muhimu. Akiwaisha abiria anapata abiria mwingine fasta na jioni inapofika anakuwa amekamilisha hesabu ya bosi huku roho yake kutwa nzima akiwa ameiweka rehani.

Ninavyofahamu mimi Bodaboda ni ofisi. Ni ofisi ambayo kila anayeendesha ni lazima aipe heshima yake. Navutiwa na baadhi ya waendesha Pikipiki kwa kulifahamu hili, wanavaa mavazi safi na wanaendesha kwa ustadi mkubwa.

Kwa leo naomba niishie hapa, Abiria wa Mwendo Kasi nimefika mwisho wa safari yangu, natelemka tukutane tena wiki ijayo kwenye safu hii ambayo lengo lake ni kuyoosha pale palipopinda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles