28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Bodaboda wapinga mauaji kwa maandamano

p-2

Na IBRAHIM YASSIN-MBOZI

MADEREVA wa bodaboda katika Mamlaka ya Mji wa Vwawa, wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe, wameandamana hadi Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa, wakipinga tabia ya watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, kuwaua na kuwapora bodaboda zao.

Waendesha bodaboda hao waliandamana jana baada mwenzao mmoja, Paul Mwambije, kuuawa kwa kunyongwa na kuporwa pikipiki wiki iliyopita.

Pia, walikuwa wakilalamikia mwenzao mwingine, Ayoub Kanyeleza, kutekwa na watu wasiojulikana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni na kuporwa pikipiki yake hivi karibuni.

Akizungumza na MTANZANIA jana, shuhuda wa maandamano hayo, Elikana Lwila ambaye ni dereva wa bodaboda katika kijiwe cha Vwawa makaburini, alisema Kanyeleza alijeruhiwa baada ya kukodishwa na watu wawili na kuwapeleka katika Kijiji cha Ilika, Kata ya Asamba.

“Walipokuwa njiani, ilitokea pikipiki moja ambayo iliwazuia kwa mbele ikiwa na mtu mmoja ambaye aliungana na wale waliobebwa wakaanza kumchoma na kitu chenye ncha kali shingoni na shavuni na kumtupa akiwa hoi kisha kumpora pikipiki.

“Baada ya tukio hilo, msamaria mwema alitokea na kumbeba hadi hospitali kisha akatoa taarifa polisi na kwenye uongozi wa waendesha bodaboda ambao walifika Hospitali ya Vwawa kumuona.

“Baadaye jana (juzi), majeruhi alihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya baada ya hali yake kuwa mbaya,” alisema Lwila.

Katika tukio la pili, Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda hao katika kijiwe hicho, Godfrey Kaijage, alisema Mwambije alikodiwa na mtu mmoja aliyemwelekeza ampeleke nyumbani kwa mganga wa kienyeji aitwaye Kamzembe.

“Walipokuwa njiani, walijitokeza watu wengine na kumteka kisha wakamnyonga shingo hadi kufa na kumtupa pembezoni mwa barabara na kumpora pikipiki yake.

“Kupitia umoja wetu, tulianza msako kwa kushirikiana na polisi ambapo tuliwakamata watu wawili, Lwitiko Mwakyusa na mwenzake ambaye hakufahamika jina.

“Kwa hiyo, kutokana na matukio hayo, tumeamua kuandamana ili kufikisha kilio chetu polisi kwa sababu inaonekana hakuna watu wa kutusaidia kukabiliana na wahalifu hao,” alisema Kaijage.

Naye Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Songwe, Mathius Nyange, alithibitisha kuwapo kwa maandamano na matukio hayo ya uhalifu.

Pamoja na hayo, alisema Jeshi la Polisi, mkoani hapa linaendelea kufuatilia matukio hayo kwa ajili ya kuwakamata watuhumiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles