THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
WACHEZAJI waliokuwa majeruhi katika kikosi cha Simba, John Bocco, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomary Kapombe, jana walijumuika na wenzao kwenye mazoezi ya kujiandaa na michezo ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba itashuka dimbani Jumapili hii kuumana na Mbeya City, katika mchezo wa Ligi Kuu utakaochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Bocco hajaitumikia Simba katika mchezo wowote wa Ligi Kuu msimu huu kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuashiria ufunguzi wa msimu mpya.
Kapombe alikosa mechi mbili za ligi hiyo, dhidi ya Singida United na Mwadui kutokana na kusumbuliwa na malaria, wakati Tshabalala aliumia akiwa kwenye majukumu ya kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Katika mazoezi hayo yaliyofanyika kwa saa moja na nusu Viwanja vya Gymkhana jijini hapa, nyota hao walishiriki kila hatua na kuonekana kuwa fiti dakika zote.
Baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems, alisema amefurahi kuwaona wachezaji hao wakiwa wameimarika.
“Tunajiandaa vizuri kuikabali Mbeya City, nafahamu mchezo utakuwa na ushindani mkubwa lakini tumejipanga kupambana licha ya kuwa tumetoka kufungwa katika mechi iliyopita.
“Huwezi kucheza mfululizo bila ya kufanya makosa, kuna wakati unaweza ukapoteza.
“ Ninaweza kusema uchovu pamoja na ubovu wa viwanja vilichangia wachezaji washindwe kucheza katika viwango vyao,”alisema Patrick.
Wakati huo huo kikosi cha Simba kiliingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo wa kesho.
Simba ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 18, baada ya kushuka dimbani mara saba, ikishinda sita na kupoteza mmoja.