KAMPALA, UGANDA
MWANAMUZIKI aliyegeukia siasa, Bobi Wine, ambaye alikuwa akishikiliwa kwa karibu wiki mbili nchini Uganda, ameachiliwa huru kwa dhamana na Mahakama Kuu mjini Gulu, kaskazini mwa nchi hiyo.
Mbunge huyo wa Kyadondo Mashariki ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, amepewa dhamana pamoja na wabunge wengine watatu na watuhumiwa wengine wanane.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuhusika katika tukio la kuurushia mawe msafara wa magari ya Rais Yoweri Museveni wakati wa kampeni za ubunge za uchaguzi mdogo wa Arua.
Kassiano Wadri, aliyeshinda ubunge wa Arua ni miongoni mwa wabunge waliokuwa wamezuiliwa.
Wadri ameachiwa kwa dhamana lakini akazuiwa kuzuru eneo la ubunge lake kwa miezi mitatu bila idhini ya mahakama.
Maombi ya dhamana ya washukiwa wengine 21 walioshtakiwa pamoja na Bobi Wine, yangesikilizwa na mahakama baadaye jana.
Awali, taarifa zilikuwa zimesema kuwa wakili wa kimataifa aliyekuwa amepewa kazi ya kumwakilisha Bobi Wine, amezuiwa kuingia nchini humo.
Gazeti la Monitor la hapa liliripoti kuwa Robert Amsterdam ameorodheshwa kama mtu asiyetakiwa  Uganda na Serikali ya nchi hiyo.
Alikuwa miongoni mwa mawakili waliokuwa wameorodheshwa kumtetea Kyagulanyi katika kesi ambayo ameshtakiwa kwa uhaini.
Jukumu la raia huyo wa Canada lilikuwa kuhusika na masuala ya ufundi, kutoa ushauri na pia kusaidia katika kufanya utafiti.