LOS VEGAS, MAREKANI
ALIYEKUWA mume wa nyota wa muziki, Whitney Houston, Bobby Brown, amefunguka kwa mara ya kwanza kuwa ahusiki kumshawishi mke wake kutumia dawa za kulevya.
Whitney alipoteza maisha 2012 kutokana na matumizi mabaya ya dawa hizo na mtoto mmoja aliyemuacha, Kristina Brown naye alifariki kwa madai ya kutumia dawa hizo kwa kiasi kikubwa.
Ilidaiwa kwamba mume wa Whitney, Bobby Brown, alihusika kumshawishi mke wake kutumia kama ilivyo kwake lakini alikana.
Akihojiwa na mtandao wa 20/20, Bobby alikanusha habari hizo ambazo zilianza kuenea tangu kifo cha mke wake mwaka 2012.
“Niliyasikia mengi yakiongelewa juu ya kifo cha mke wangu na hata mwanangu, lakini ukweli ni kwamba kila mmoja alikuwa na akili zake na maamuzi yake, sikuweza kumshawishi atumie dawa ila mwenyewe alijikuta akitumia na sikuweza kumkataza kwa kuwa ni maamuzi yake.
“Ukweli utabaki kuwa hivyo hata kama watu wakizidi kuyaongea ambayo wanayajua wao, lakini mimi nalijua hili ambalo nimeliweka wazi,” alisema Bobby.