23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

BOBALI: NINAUMIZWA NA MGOGORO NDANI YA CUF

* Asema anaamini utakwisha japo unachochewa na mahasimu wao


Na ELIZABETH HOMBO

HAMIDU Hassan Bobali ni miongoni mwa wabunge vijana katika Bunge la 11 ambao wanalichachafya Serikali kwa hoja.

Bobali ambaye ni Mbunge wa Mchinga mkoani Mtwara kupitia Chama Cha Wananchi (CUF), katika Bunge la 11 alikuwa wa kwanza kuhoji kurejeshwa kwa mjusi mkubwa wa kihistoria aliyechukuliwa hapa nchini na kupelekwa Ujerumani.

MTANZANIA limefanya mahojiano na Bobali ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CUF (JUVICUF), pamoja mambo mengine amezungumzia mikakati ya jimboni kwake na mgogoro ndani ya CUF huku akisema anaumizwa akiwa kama mwanasiasa kijana.

MTANZANIA: Ni mambo gani ambayo uliyaahidi kuyafanya katika jimbo lako na kuyatekeleza katika kipindi hiki?

BOBALI: Maeneo mengi ya jimbo yalikuwa hayapitiki. Miundombinu ilikuwa ni kero sana lakini kupitia ushirikiano wa halmashauri tumeweza kujenga barabara nyingi sana.

Kati ya barabara 12 zilizokuwa zinasumbua, zilizobaki sasa ni mbili tu. Hili ni jambo ambalo ninajivunia, niliamua nisicheze mbali na halmashauri huku nikiwa sikosekani kwenye vikao vya madiwani.

Jambo lingine ambalo ninajivunianalo ni zao la korosho kupata soko, ni jambo nililolipigia kelele. Nashuruku wabunge wa Lindi na Mtwara tumekuwa wamoja katika hili, kuimarika kwa bei ya korosho ni faraja kwetu sote.

Pia kwa upande wa elimu; nimetumia mfuko wa jimbo vizuri mpaka sasa hakuna shule ya sekondari ambayo haina umeme. Nimetumia mfuko wa jimbo kuhakikisha shule zote za msingi zina umeme.

Maeneo ambayo hakuna shule za msingi pia tumeanza kuzijenga.

Wakati nagombea ubunge niliahidi kuwasomesha wanafunzi wa kidato cha nne ambao wamefaulu kwenda kidato cha tano na tayari nimewalipia ada jumla ya wanafunzi 25 waliofaulu kwenda kidato cha tano mwaka 2015.

Mwaka 2016 wamefaulu wanafunzi 20 nao nitawalipia kwa sababu ndio ilikuwa hoja yangu ya kwanza wakati wa kampeni.

Vile vile tumeanzisha kitu kinaitwa jimbo test, unafanyika mtihani wa kijimbo lengo likiwa ni kuwapima watahiniwa wetu.

Kwa upande wa afya; tumeanza kujenga zahanati katika vijiji mbalimbali na nne zinasubiri kufunguliwa na nyingine moja nimeanza kujenga mwenyewe baada ya mwaka mmoja itakuwa tayari.

Pia tumeanza kujenga nyumba za waganga. Vilevile nimeshirikiana na wananchi kujenga kituo cha cha afya badala ya zahanati tu.

Lakini pamoja na hilo, tuna changamoto kubwa ya magari matatu ya wagonjwa ni chakavu sana yaani yote ni mabovu, nimetoa fedha za mfuko wa jimbo. Tunachoomba hivi sasa ni wafadhili watusaidie magari ya wagonjwa.

Pamoja na hilo, pia wahudumu wa afya ni wachache. Kuna zahanati hatufungui kwa sababu wahudumu ni wachache.

MTANZANIA: Ni mara yako ya kwanza kuwa bungeni, pengine ni hoja gani ambayo umeiwakilisha na unajivunia?

BOBALI: Jambo ambalo ninajivunia kuwasilisha bungeni ni hoja ya kurejeshwa kwa mjusi mkubwa wa kihistoria aliyechukuliwa hapa nchini na kupelekwa Ujerumani.

Pia mapendekezo yetu mengi, serikali imeyachukua. Kamati yetu imetembelea Manyara tumeona namna wafugaji wanavyopata shida kupata maji. Serikali iandae mkakati wa kuchimba mabwawa.

MTANZANIA: Unauzungumziaje mwenendo wa Bunge la 11 kwa ujumla wake?  

BOBALI: Bunge la 11 ni ‘undefined’; lakini kwa upande mwingine kwa mara ya kwanza limekuwa moja tumeungana kutetea hadhi yake na madaraka ya Bunge.

Msimamo wa spika umeonyesha ameweza kufanya kazi lakini hatukuanza vizuri tulikuwa ‘separated’ kadiri siku zinavyokwenda mbele, watu wamezoeana. Spika ametuonyesha mwanzo mzuri na sasa anakidhi vigezo vya kuwa Spika.

Awali ilikuwa ni ugeni, kila mtu alikuwa anazungumzia uvyama na Naibu Spika na yeye alikuwa mgeni ndio maana yakatokea yale yote.

MTANZANIA: Upinzani kwa sasa unaonekana kupoa tofauti na huko nyuma ambapo walikuwa wakiibana serikali kwa mambo mbalimbali ikiwemo ufisadi, unadhani kasi ya Rais Magufuli imesababisha hilo?

BOBALI: Hapana. Kuzuia mikutano ni jambo mbaya sana lakini ni kwa sababu hataki uwazi huku anapambana na corruption huku hataki transparent.

Hili la kuzuia mikutano itatubeba sana wapinzani. Yeye Rais anadhani anatuumiza sisi lakini watanzania nao wanahoji kilicho behind.

Kuruhusu tu mikutano wakati wa kampeni tutakavyoyaeleza mambo yetu hawatakuwa na muda wa kujibu na hata hawataaminiwa na watanzania na sisi yatatupa kiki.

Ni changamoto lakini tunabadili gia lakini bado haijawa kigezo cha sisi kutofanya siasa.

MTANZANIA: Unaizungumziaje nafasi ya CUF ndani ya Ukawa?

BOBALI: CUF tuko Ukawa na hatutoki. Kama ni mtu mmoja amepinga Ukawa ni yeye kwa sababu hatujafikia malengo ambayo yalikuwa ni kuiondoa CCM madarakani na kupata katiba ya wananchi.

Baada ya hapo sasa tunaweza kuamua kuwa na chama kimoja na vyovyote vile tunakavyoamua.

MTANZANIA: Taarifa zilizopo ni kwamba Chadema ina mpango wa kuua Ukawa ili kibaki pekee chenye nguvu na ndio hoja ambayo inatumiwa na Profesa Lipumba, hili unalizungumziaje?

BOBALI: Kama inaextend sioni kama ni tatizo kama chama cha siasa lakini kama inatumia hiyo nguvu kupitia mgongo wa CUF au chama kingine kilichopo ndani ya Ukawa ni dhambi kubwa sana.

Kwa mfano chama chetu kimejengwa kwa miaka mingi na watu walijitoa na kilipitia vipindi vigumu sana. Sasa leo mtu aamke tu asubuhi aseme anakiua CUF si jambo rahisi kwa sababu chama kiliaminiwa na wengi.

Kama mkakati huo upo ni mbaya sana na tutakuwa hatuna nia ya kuiondoa CCM madakarani.

MTANZANIA: Unauzungumziaje mgogoro unaofukuta ndani ya chama chenu?

BOBALI: Mgogoro ni mkubwa, mimi kama mwanasiasa kijana sipendi haya binafsi unaniumiza…naamini siku moja mgogoro huu utaisha japo CCM wanachochea usiishe. Ipo siku wanachama wataziweka kando njama hizi.

MTANZANIA: Unadhani upinzani unatakiwa ufanye nini ili kujahakikishia ushindi mwaka 2020?

BOBALI: Waisue Ukawa wajue kabisa kwamba ukishavunjika ndoto ya CCM kutoka madarakani haipo. Habari za kugawana kata na vijiji ifanyike mapema mwaka 2018. Hata wa ubunge na udiwani mgawanyo ufanyike mwaka 2019. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles