Na Mwandishi wetu,
MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Dotto Biteko, amempongeza Rais Dk. John Magufuli kutokana na uamuzi wake wa kuunda kamati maalum kwa ajili ya kuchunguza mchanga wa madini.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana baada ya Rais Magufuli kukabidhiwa ripoti ya pili, Biteko alisema ripoti zote mbili zimethibitisha kilio cha Watanzania kuhusu kuibiwa rasilimali za madini uliofanywa kwa miaka mingi.
“Rais amejibu kilio hiki cha Watanzania, wananchi walikuwa wanaamini na hasa wale wanaozunguka migodi kwamba tulikuwa tunaibiwa.
“Ripoti zote mbili zimethibitisha ukweli juu ya kilio hiki na katika hili nampongeza Rais kwa uamuzi wake wa kuunda kamati maalumu ambazo zimetuletea matokeo chanya,” alisema.
Hata hivyo Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe, alisema kamati yake inasubiri maelekezo ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, atakapounda kamati ya kufuatilia uchimbaji wa madini ya almasi.
“Spika ameahidi kuunda kamati ya kufuatilia suala la uchimbaji wa madini ya almasi kabla ya Bunge hili la Bajeti halijaisha.
“Siku zote sisi wabunge na wajumbe wa kamati za Bunge tumekuwa tukifanya kazi chini ya maelekezo ya Spika, hivyo katika hili tunasibiri mwongozo na maelekezo yake,” alisema.