25.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Biteko aainisha mafanikio sekta ya madini

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Madini, Dotto Biteko, amesoma bajeti ya wizara yake kwa mara ya kwanza tangu apandishwe kutoka naibu waziri na kuwa waziri kamili, ambapo amesema sheria mpya ya madini, ukuta wa Mererani, umeleta mapinduzi katika sekta hiyo.

Akisoma bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2019/20 bungeni jijini hapa jana, alisema kutokana na sheria ya madini na mikakati ya kudhibiti utoroshwaji wa bidhaa hiyo, Serikali imetaifisha madini ya Dola za Marekani milioni 13.5 na Sh milioni 6.3

Alisema kwa Tanzanite, mwaka 2018, wachimbaji wadogo pekee wamechangia Sh bilioni 1.4 na uzalishaji umeongezeka kutoka kilo 147.7 hadi 781.204.

Biteko alisema Tume ya Madini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, vimekuwa vikiendelea kudhibiti utoroshwaji madini kuhakikisha rasiliamali hiyo inatumika kwa manufaa ya Watanzania.

Alisema hadi kufikia Februari, zilikamatwa karati 66.60 za madini ya almasi yenye thamani ya Dola za Marekani 34,782.52  jijini Dodoma.

“Aidha, gramu 77.0 za madini ya dhahabu zenye thamani ya Sh milioni 6.3 zilikamatwa mkoani Tabora na kilo 75,957.30 za madini ya vito yenye thamani ya Dola za Marekani 1,795,87.87 zilikamatwa jijini Dar es Salaam,” alisema Biteko.

Alisema kilo 5.72 za madini ya dhahabu yenye thamani ya Sh milioni 389.7 zilikamatwa mkoani Geita, gramu 11,445.52 za madini ghafi na karati 1,351 za vito vyenye thamani ya Sh milioni 206.5 zilikamatwa mkoani Arusha huku tani 3.7 za madini ya Rhodelite, zenye thamani ya Dola za Marekani  50,162.46 zilikamatwa mkoani Morogoro.

Biteko alisema mkoani Mwanza yalikamatwa madini ya dhahabu kilo 319.594 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 11.7.

MADINI YATAIFISHWA

Alisema madini yaliyokamatwa katika Mikoa ya Dodoma, Tabora, Mwanza na Dar es Salaam yalitaifishwa.

Aidha alisema madini yaliyokamatwa mikoa ya Arusha, Morogoro na Geita yapo katika hatua mbalimbali ya uchunguzi.

“Mpaka Machi, madini ambayo yaliyotaifishwa yalikuwa na thamani ya Dola za Kimarekani milioni 13.5 na Sh milioni 6.3,” alisema Biteko.

MAOFISA MADINI WAKAZI WAIMARISHA ULINZI

Biteko alisema ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ya uzalishaji kwenye migodi mikubwa na ya kati kwa kuwaweka maofisa madini wakazi (MROs).

Alisema lengo la kuweka maofisa hao ni kusimamia na kuwasilisha taarifa za uzalishaji wa kila siku pamoja na kudhibiti mianya ya utoroshwaji madini.

Katika maeneo ya viwanja vya ndege na mipakani, alisema wamewekwa wasimamizi kuhakikisha madini yanayopitishwa yana vibali husika na kuzuia utoroshaji.

“Nitoe wito kwa Watanzania kufanya shughuli za madini kwa kuzingatia sheria za nchi ikiwemo Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kama ilivyorekebishwa mwaka 2017 pamoja na kanuni zake,” alisema.

ONYO KWA WATUMISHI

Biteko alibainisha kuibuka kwa matukio ya baadhi ya watumishi wasio waaminifu kushirikiana na wachimbaji na wafanyabiashara madini wasio waaminifu kuiibia Serikali mapato kupitia kuwasilisha taarifa zisizo sahihi za uzalishaji madini.

“Katika kuhakikisha tunakomesha tabia hii isiyo ya kizalendo inayopelekea Serikali kupoteza mapato, Serikali imeendelea kuchukua hatua kali za kinidhamu ikiwemo kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi na kuwafikisha mahakamani waliobainika kuwa na makosa,” alisema.

WACHIMBAJI WADOGO WAONGEZA MAPATO

Kuhusu uendelezaji wa eneo la kimkakati kwenye migodi ya Mirerani, Biteko alisema baada ya kujengwa ukuta kuzunguka mgodi huo, udhibiti madini ya Tanzanite umeimarika na hivyo kuongeza ukusanyaji maduhuli yatokanayo na madini hayo.

Alisema wachimbaji wadogo wameitika wito wa kulipa kodi ambapo sasa wanalipa kuliko kipindi chochote kwenye historia ya uchimbaji kwenye eneo hilo.

“Wachimbaji wadogo Mirerani walikuwa wanachangia kwa asilimia 6 hadi 10 ya mapato yote, kiasi kikubwa kilikuwa kikichangiwa na mgodi wa TanzaniteOne.

 “Mwaka 2017 Sh bilioni moja zilikusanywa, kati ya fedha hizo Sh milioni 930 zilikusanywa kutoka mgodi huo kama mrabaha wa ada ya ukaguzi ikiwa sawa na asilimia 85 ya mapato yatokanayo na uzalishaji wa Tanzanite na Sh milioni 164.1 sawa na asilimia 15 zilikusanywa kutoka kwa wachimbaji wadogo,” alisema.

Alisema mwaka 2018, wachimbaji wadogo pekee wamechangia Sh bilioni 1.4 na uzalishaji umeongezeka kutoka kilo 147.7 hadi 781.204.

Biteko alisema ili kutekeleza majukumu ya wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2019/20, aliliomba Bunge kuidhinisha na kupitisha makadirio ya sh bilioni 49.4 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.

UPINZANI

Akiwasilisha jana bungeni, msemaji mkuu wa upinzani katika Wizara ya Madini, John Heche, alisema katika mwaka huu wa fedha, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh bilioni 19.62 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisema hadi kufikia Februari, wizara hiyo ilikuwa imepokea Sh milioni 100, sawa na asilimia 0.5 ya bajeti iliyoidhinishwa.

MAONI YA KAMATI
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mariam Ditopile, alisema licha ya Serikali kudhibiti utoroshwaji wa madini, kamati inashauri kuendelea kuwekwa mikakati endelevu na mbinu za kisasa kudhibiti biashara ya madidi isiyo rasmi.

MAONI YA WABUNGE

Mbunge wa Viti Maalumu, Neema Mgaya (CCM) alisema ukuta wa Mererani mkoani Arusha umeweza kuokoa madini ambayo yalikuwa yakitoroshwa nje ya nchi.

Mbunge wa Nyang’wale, Hussein Amar (CCM), aliitaka Serikali ichukue hatua za haraka kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata leseni.

Maftaha Nachuma (CUF) wa Mtwara Mjini, alihoji kuhusiana na utekelezaji wa mlundikano wa leseni zaidi ya 99  za uchimbaji wa madini ya Tanzanite katika eneo la Mirerani.  

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma (CCM) alidai kwamba kuna shida kubwa kwa watendaji katika wizara hiyo kutotimiza wajibu wao, hivyo alitaka wanajeshi waende wakafanye kazi.

BAJETI YAPITA

Akihitimisha mjadala wa wizara yake, Biteko alisema kipaumbele cha awamu ya tano ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki yake.

“Urasimu, Serikali itachukua hatua kuhakikisha wananchi wanapata haki zao.

“One Stop Centre tunataka kuwaondolea urasimu na hilo litakuwa jengo moja katika ofisi moja,” alisema.

Kuhusu wafayakazi wa wizara yake kutokuwa waaminifu, Biteko  alisema jambo hilo analichukua na watalifanyia kazi.

“GGM wameanza kulipa fidia, kama kuna mwananchi anadhani hajalipwa vizuri awasiliane na wizara yangu, kuna mtu amelipwa milioni 74 mara ya kwanza, lakini pia ameleta jina mara ya pili anataka alipwe tena, sio sawa Mheshimiwa Spika, lazima tuwalinde wawekezaji,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles