BINTI YA RAIS CONGO ASHITAKIWA KWA RUSHWA UFARANSA

0
579
Rais Denis Sassou Nguesso wa Congo
Rais Denis Sassou Nguesso wa Congo

PARIS, UFARANSA

BINTI wa Rais Denis Sassou Nguesso wa Congo, Julienne Sassou Nguesso amefunguliwa mashitaka ya rushwa nchini hapa.

Uamuzi huo wa Mahakama za hapa ni matokeo ya uchunguzi wa tuhuma za ufisadi zinazozihusisha familia tatu za viongozi wa Afrika, ambao mali zao zilizopo hapa zinashikiliwa kwa uchunguzi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), binti huyo mwenye umri wa miaka 50, na mumewe Guy Johnson (53) wamewekwa chini ya uchunguzi wiki hii kwa ‘matumizi mabaya na kutakatisha fedha.’

Wapelelezi wanajaribu kuangalia namna wawili hao walivyoweza kununua jumba kubwa la kifahari mwaka 2006 kwa euro milioni tatu katika kitongoji cha Neuilly-sur-Seine mjini Paris.

Julliene Sassou Nguesso ni wakala wa bima na mumewe ni wakili.

Kati ya mwaka wa 2007 na 2011, jumba hilo lenye vyumba saba vya kulala na bwawa la kuogelea lilifanyiwa ukarabati wa euro milioni 5.34, na kuongeza kiasi cha uwezekezaji wao kufikia karibu euro milioni 10.

Wapelelezi wanaamini wenzi hao huenda walifadhili sehemu ya mradi huo kupitia kampuni ya kigeni nchini Shelisheli na mauzo ya hisa alizomiliki Julienne Sassou Nguesso katika kampuni moja ya mawasiliano ya simu inayohusishwa na tuhuma za ufisadi.

Aidha wachunguzi waligundua kuwa mamilioni ya euro za serikali yalisafirishwa kutoka Brazzaville tangu mwaka 2007 hadi kwenye akaunti za kigeni nchini Shelisheli, kisiwa cha Mauritius na Hong Kong, ambazo wanaamini zilitumika kufadhili maisha ya kifahari ya jamaa za familia ya rais.

Maafisa wa Ufaransa wamekuwa wakiuchunguza ukoo mzima wa Sassou Nguesso pamoja na jamaa za Rais Omar Bongo wa Gabon na Rais Teodoro Obiang Nguema wa Guinea ya Ikweta.

Mwanawe Obiang, Teodorin, kwa sasa anapambana na kesi katika mahakama ya Paris kwa madai ya kupora mali za nchi hiyo ili kufadhili maisha yake ya kifahari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here