30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, August 9, 2022

Binti kinara wakuibia wazee ATM kufikishwa kortini

TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia mkazi wa Chalinze, Halima Juma (23) kwa tuhuma za wizi wa fedha katika mashine za kutolea fedha (ATM).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema Novemba 11 mwaka huu walimkamata Halima akiwa katika ATM za Benki ya CRDB tawi la Mbagala akijifanya kuwasaidia wazee.

“Halima alijifanya kuwasaidia wazee hasa wastaafu, wasiojua kutumia mashine hizo kwa lengo la kuchukua namba za siri na kuwabadilishia kadi na baadaye kuwaibia fedha kwenye akaunti zao,” alisema Mambosasa.

Alisema alikuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akiwabadilishia kadi zao halisi za benki na kuwapa nyingine na baadaye kuiba fedha zilizopo kwenye akaunti zao.

Alisema askari walimtilia shaka na kumkamata na baada ya kukaguliwa ambapo alikutwa na kadi 23 za benki kutoka kwa watu tofauti alizokuwa amezificha kwenye pochi aliyokuwa ameificha sehemu za siri.

“Tumemkuta na kadi za benki ya CRDB saba, NMB sita, NBC mbili, Amana mbili, Benki ya Posta mbili,  ACB mbili, Stanbic moja, DCB moja na Equity kadi moja,” alisema Mambosasa.

Alisema mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na jeshi hilo na atafikishwa mahakamani ushahidi utakapokamilika.

Kulinda uchaguzi kwa helkopta, mbwa

Katika hatua nyingine, alisema jeshi hilo litafanya doria za miguu, pikipiki, mbwa farasi na helkopta kuimarisha ulinzi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemvba 24.

Aidha alisema jeshi hilo litaimarisha ulinzi katika vituo vya kupigia kura, ofisi zote za kata, na vyama vya siasa katika kipindi cha uchaguzi huo.

 “Tutashirikiana na vyombo vyote vya ulinzi na usalama chini ya Mwenyekiti wetu Mkuu wa Mkoa Paul Makonda kuhakikisha jiji lipo salama,” alisema Mambosasa.

Mvua zaua wawili

Mambosasa pia alisema mvua zinazoendelea kunyesha zimeua watu wawili na kujeruhi mmoja .

“Mtu mmoja alisombwa na maji akivuka mto na mwingine alipigwa na radi na kufa palepale huku mmoja akijeruhiwa na radi hiyo,” alisema Mambosasa.

Aliwataka wazazi kuchukua tahadhari kwa kuwazuia watoto kucheza katika madimbwi na kuchukua tahadhari wakati wa kuvuka mito.

“Wazazi wawazuie watoto wao kuvuka makolongo wanapokwenda shuleni kwani maji hayapimwi,” alisema Mambosasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,291FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles