PATRICIA KIMELEMETA – dar es salaam
SERIKALI inatarajia kuwasilisha muswada wa bima ya afya bungeni, ambao ukipitishwa itakuwa lazima kwa kila Mtanzania kuwa na bima ya afya.
Hayo yalisemwa jijini hapa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu katika kongamano la wadau wa afya.
Kongamano hilo ambalo limeshirikisha nchi zaidi ya 10 kutoka ndani na nje ya Afrika limefadhiliwa na Ubalozi wa Uswisi nchini.
Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri Ummy alisema muswada huo utawasilishwa bungeni Aprili na lengo la Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anatumia bima ya afya kupata huduma bora za matibabu.
Alisema kupitishwa kwa muswada huo kutasaidia kutoa fursa kwa Watanzania kujiunga na bima ya afya kwa lazima ili waweze kupata huduma za matibabu.
“Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020 asilimia 70 ya Watanzania wamejiunga kwenye bima ya afya kupitia mifuko mbalimbali ya uchangiaji,” alisema Ummy.
Alisema ifikapo mwaka 2025, asilimia 85 ya Watanzania wataweza kutumia bima ya afya kupata huduma za matibabu katika vituo mbalimbali vya afya nchini.
“Tunatarajia kuwasilisha muswada bungeni wa bima ya afya kwa wote ni lazima ifikapo Aprili, lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za matibabu kwa kutumia bima,” alisema.
Aliongeza kuwa hadi sasa Serikali imetumia Sh bilioni 30 kugharamia huduma za matibabu kwa wagonjwa wa saratani ambao ni wanachama wake.
VIFURUSHI VYA BIMA YA AFYA
Ummy alisema Machi mwaka huu wanatarajia kuzindua vifurushi vya bima ya afya ambavyo vitaisaidia sekta isiyo rasmi kupata bima ya afya.
Alisema Serikali itashirikiana na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi ili waweze kujiunga na bima ya afya.
Oktoba mwaka jana, Ummy alisema idadi ya watu wanaotumia huduma za mifuko ya bima ya umma ni 17,656,697 sawa na asilimia 33 ya Watanzania wote.
Alisema wanaotumia bima ya taifa idadi yao imeongezeka kutoka 164,708 mwaka 2001/2002 hadi 873,012 Septemba 2018.
“Ongezeko hili limetokana na kanuni na misingi inayotumika katika kuendesha utaratibu wa mfuko huu, ikiwa ni pamoja na uchangiaji wenye usawa kwa kuzingatia viwango vya mshahara, usawa katika kupata huduma na ushiriki wa Serikali katika usimamizi kwa faida ya wanachama,” alisema Ummy.
Alisema upande wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF),
jumla ya kaya zilizojiunga Septemba mwaka jana zilikuwa 2,220,953 ikiwa ni sawa
na wanufaika 13,506,330 sawa na asilimia 25 ya Watanzania wote.
Aidha Ummy alisema hadi sasa idadi ya wanachama wengi waliojiunga, asilimia 67
ni watumishi wa umma ambao wanajiunga kwa mujibu wa sheria.
Alisema mfuko unaendelea kutoa elimu na kubuni vifurushi mbalimbali vitakavyovutia wananchi wengi kujiunga na kufaidika.
Ummy alisema mfuko huo utawawezesha wanachama wengi zaidi kujiunga hasa wale wa sekta isiyo rasmi na kujiwekea malengo ya kuwafikia Watanzania asilimia 50 mwaka 2020.
“Mfuko umekamilisha uandaaji wa vifurushi vya michango na mafao kulingana na uwezo wa wananchi kulipia bima ya afya, suala hili lipo katika hatua za mwisho kabla ya kuanza kwa utekelezaji,” alisema Ummy.
Alisema kuwa mpango huo utamwezesha mwananchi kuchagua vifurushi vya aina mbalimbaliu vya huduma anayoitaka kwa utaratibu utakaojulikana kama ‘JIPIMIE’ na wanachama watalipa kidogo kidogo kwa utaratibu ujulikanao kama ‘DUNDULIZA’ ambao tayari umeshakamilika.