29.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Bilioni 4.9 kutatua changamoto ya maji Itumba na Isongole, Ileje

Na Denis Sikonde, Ileje

Serikali imetoa fedha Sh Bilioni 4.9 kwa ajili ya kumaliza changamoto ya tatizo la maji katika miji ya Itumba kata ya Itumba na mji wa Isongole kata ya Isongole wilayani Ileje mkoani Songwe ambapo wananchi wa maeneo hayo wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta maji safi na salama hali inayoathiri familia zao.

Karibu: Sehemu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wakimpokea mkuu wa Wilaya ya Ileje, Anna Gidarya.

Hayo yamebainishwa na Mei 17, 2022 na Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Anna Gidarya wakati wa kujibu kero za wananchi zilizoibuka kwenye mkutano wake wa hadhara katika miji ya Itumba na Isongole ambapo wananchi walipaza sauti zao kuiomba Serikali kuwaletea huduma ya maji safi na salama.

Gidarya amesema kazi ya serikali ni kuhakikisha inamsimamia Mkandarasi ambaye amesaini mkataba kutekeleza mradi huo ili kutatua changamoto ya maji inayowakabili wananchi wa miji hiyo kwa muda mrefu.

“Serikali imesikia kilio chenu, hivyo fedha hizo zipo kwenye mfuko wa Wizara ya Maji kupitia Wakala wa Maji mijini na Vijijini (RUWASA) makao makuu ambapo zitatumika ipasavyo kuhakikisha kuwa mnapata maji kama ilivyokusudiwa.

“Serikali imekuwa ikifanya kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025, hivyo kama viongozi kazi kubwa kwetu ni kuhakikisha wanasimamia fedha hizo kwenye miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo huu wa maji,” amesema Gidarya.

Aidha, Gidarya amesema pindi mradi huo utakapokamilika wananchi wakawe walinzi wa miundombinu ya maji ili ikawanufaishe kwa kizazi kilichopo na baadaye.

Kaimu Mkurugenzi wa mamlaka ya maji katika miji hiyo, Medson Ngailo amesema kuwa zaidi ya wananchi 20,000 watanufaika na mradi huo na Mkandarasi ameanza hatua za awali za maandalizi ya ujenzi huo.

“Mkandarasi ataanza ujenzi wa chujio katika eneo la Bongolo ambalo litatumika kuchuja maji ili wananchi wapate maji safi na salama itakayokuwa ni mwarobaini wa wananchi kupata maji kwa uhakika na yasiyokuwa na tope,” amesema Ngailo.

Ameongeza kuwa kwa mda mrefu wananchi wa miji hiyo hukumbwa na changamoto ya ukosefu wa maji ya uhakika, kwa kupata maji ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu kwa kuwa ni machafu hivyo serikali imetoa fedha ili kuwanusuru na kazia hiyo ambayo ilikuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu.

Awali, Diwani wa kata ya Isongole, Gwalusako Kapesa alipongeza juhudi za serikali na kuiomba kuwatatulia kero hiyo ambayo imekuwa ikikwamisha maendeleo ya wananchi ambao hutumia muda mwingi kutafuta maji.

“Serikali ya awamu ya sita, imesikia kilio cha wananchi kwa kutoa fedha Sh bilioni 4.9 na tayari Mkandarasi amepatikana yupo eneo la chanzo kwa ajili ya kuanza kazi za awali,” amesema Kapesa.

Imani Mwambene mkazi wa Mji wa Isongole alisema ahadi ya aliyekuwa Naibu waziri wa maji na kwa sasa waziri wa maji, Juma Aweso aliwaahidi kutatua changamoto ya maji mpaka sasa imekuwa ni ahadi, hivyo kama serikali imeleta fedha zisimamiwe vizuri ili kutatua changamoto hiyo ni jambo la kupongezwa.

“Tunakuamini mkuu wetu wilaya mama Gidarya kama ulivyoaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa utasimamia hili kuhakikisha kero ya maji inatatuliwa kwa wakazi Isongole,” amesema Mwambene.

Hivi karibuni Mbunge wa la Ileje ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Kasekenya Msongwe aliwaahidi wananchi wa miji hiyo kuwa Serikali itahakikisha inatatua changamoto ya maji na changamoto hiyo kubaki historia pindi mradi huo utakapokamilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles