Na Clara Matimo, Mwanza
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela katika Mkoa wa Mwanza, imepokea zaidi ya Sh bilioni 32 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masalla, kwenye maadhimisho ya siku 365 za Rais Samia, lengo likiwa ni kuelezea mafanikio yaliyopatikana wilayani humo ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wa kiongozi huyo.
Ameitaja miradi hiyo ambayo imegusa sekta mbalimbali na inayowanufaisha wananchi wa wilaya hiyo kuwa ni afya, maji, elimu, nishati, miundombinu ya barabara na upimaji wa ardhi.
Amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia, wilaya hiyo imepokea Sh bilioni 26 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi stendi kuu ya mabasi na malori iliyojengwa eneo la Nyamhongolo na Sh milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa sekondari buzuruga.
“Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia, kwa kutoa fedha nyingi katika wilaya yetu ndani ya mwaka mmoja ambazo zimegusa sekta mbalimbali, sasa hivi tuko bize tunatekeleza miradi kwa manufaa ya wananchi na hiyo ndiyo kiu kubwa ya rais wetu, tumepokea fedha Sh milioni 800 kujenga wodi hospitali ya wilaya, milioni 150 ujenzi wa zahanati tatu ambazo ziko kwenye kata zetu.
“Tulipokea Sh bilioni 1.94 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa hii imetuwezesha kujenga vyumba 97 vya madarasa ya shule za sekondari kabla ya hapo hali ilikuwa ni ngumu baadhi ya wanafunzi walikuwa wanalazimika kusomea nje na kulikuwa na mrundikano mkubwa katika madarasa,”amesema na kuongeza
“Fedha hiyo ilitutaka tujenge vyumba vya madarsa pia tununue madawati lakini sisi tulienda mbali zaidi fedha tuliyobakiza tumejenga ofisi za walimu 28 ambazo hazikuwemo kwenye mpango kazi, tumemalizia majengo ya shule ambayo wananchi waliyaanzisha, tumenunua madawati zaidi ya 1,000, tumeweka mpango kazi hadi Septemba mwaka huu hakuna mwanafunzi anayekaa chini wala anakosa sehemu ya kujifunzia,”alisema Masalla.
Amesema wanaendelea na zoezi la kupima viwanja na kumikikisha wananchi maeneo mbalimbali baada ya kupokea Sh bilioni 3.5 ambazo rais amewapatia kama mkopo wenye masharti nafuu.
Masalla amesema kwa kasi ya maendeleo ambayo Rais Samia ameanza nayo, wananchi wa Wilaya ya Ilemela watarajie mambo makubwa kutoka kwenye serikali ya awamu ya sita ikiwemo kumalizia kutekeleza miradi mikubwa ambayo tayari serikali imeisha toa fedha ikiwemo ya maji na umeme.
“Ili tutekeleze miradi hiyo kwa ufanisi na kwa wakati, wito wangu kwa wananchi wa Wilaya ya Ilemela waendelee kutoa ushirikiano kwa mheshimiwa rais, viongozi wa mkoa, wilaya na kata kwa kufanya hivyo watatupa mwanya wa kuwafikishia yale ambayo wanayatamani na ambayo Rais Samia anayataka kwa wananchi wake maana lengo la rais wetu ni kuwatatulia wananchi wake changamoto mbalimbali zinazowakabili,”amesema Masalla.