29.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

Bilioni 17 kutumika kusambaza umeme pembezoni mwa Jiji la Dodoma

Na Veronica Simba-REA

Serikali inatarajia kutumia kiasi cha Sh bilioni 17.3 kuwafikishia umeme wateja wa awali 4,609 kupitia Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Pili katika maeneo yaliyo pembezoni mwa jiji la Dodoma.

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alibainisha hayo jana, Juni 16, 2021 alipokuwa akizindua rasmi mradi huo katika hafla iliyofanyika katika kijiji na kata ya Chihanga, nje kidogo ya Jiji la Dodoma.

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa Kijiji na Kata ya Chihanga, nje kidogo ya jiji la Dodoma, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Pili katika maeneo yaliyo pembezoni mwa jiji la Dodoma, Juni 16, 2021.

Amesema mradi huo utatekelezwa katika kata 16 za Mkoa wa Dodoma kwa kipindi cha miezi 12 ambapo fedha za utekelezaji wake zimetolewa na serikali kwa asilimia 100.

“Tunawaomba wananchi watumie nishati ya umeme katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na madini pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za afya, elimu, maji, mawasiliano na kuboresha thamani za bidhaa za kilimo cha viwanda,” alitoa hamasa Waziri Kalemani.

Aidha, Waziri Kalemani amebainisha kuwa mradi huo hauna fidia hivyo akawataka wananchi ambao wako katika maeneo inakopita miundombinu husika, kutoa maeneo yao pasipo kudai fidia kama mchango wao katika miradi ya maendeleo.

Katika hatua nyingine, Waziri alisisitiza kuwa bei ya kuunganisha umeme wa njia moja kwa wateja wote nchi nzima iwe kijijini au mjini ni Sh 27,000 tu kutoka Sh 177,000 ya awali na kwamba kwa wenye kuhitaji kuunganishiwa umeme wa njia tatu, gharama yake ni Sh 139,000 kutoka Sh 912,000 iliyokuwa ikitozwa awali.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka akizungumza na wananchi wa Kijiji na Kata ya Chihanga, nje kidogo ya jiji la Dodoma (hawapo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Pili katika maeneo yaliyo pembezoni mwa jiji la Dodoma, Juni 16, 2021.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amewataka wananchi kutumia umeme huku wakiuunganisha na maendeleo pamoja na elimu.

“Nyumba tunazoweka umeme tufanye maendeleo. Tuone saluni pamoja na kufunga taa ili kuwawezesha watoto kujisomea na kukuza ufaulu mashuleni,” amesema Mtaka.

Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, alimhakikishia Waziri kuwa wananchi wa Chihanga wako tayari kulipia Sh 27,000 ili waunganishiwe huduma hiyo kwa ajili ya kuutumia katika kukuza kipato na kujiletea maendeleo.

Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde akizungumza na wananchi wa Kijiji na Kata ya Chihanga, nje kidogo ya jiji la Dodoma (hawapo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Awamu ya Pili katika maeneo yaliyo pembezoni mwa jiji la Dodoma, Juni 16, 2021.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo alibainisha kuwa, Mradi huo uliozinduliwa na Waziri Kalemani ni sehemu tu ya mpango mkakati wa Wakala ambao umelenga kusambaza umeme katika maeneo yaliyo pembezoni mwa miji na majiji.

Wakili Kalolo aliongeza kuwa Mradi huo utatekelezwa katika mikoa mitatu ambayo ni Arusha, Mwanza na Dodoma ambapo utaongeza uwekezaji katika nyanja mbalimbali za maeneo yaliyo pembezoni mwa miji ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa viwanda na biashara mbalimbali.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga alieleza kuwa gharama za kutekeleza Mradi huo katika mikoa yote mitatu ya Arusha, Mwanza na Dodoma ni takribani Sh bilioni 31.2 ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 12.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,225FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles