Winfrida Mtoi na Ester Mnyika
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini(ERB), Mhandisi Bernard Kavishe, amesema kiasi cha fedha Sh 120 bilioni kinahitajika kwa mwaka ili kutengeneza wahandisi mahiri kupitia Mpango wa Mafunzo kwa Vitendo kwa Wahandisi Wahitimu(SEAP).
Amesema hayo leo Februari 28, 2024 wakati wa kufunga maadhimisho ya miaka 21 ya SEAP na semina ya siku tatu kwa wahandisi wahitimu jijini Dar es Salaam.
Amesema fedha hizo zitatumika kugharamia mahitaji kwa wahandisi wapya wahitimu 10,500 wa mafunzo ya vitendo kupitia mradi huo.
“Kwa mwaka wahandisi wapya wanaomaliza vyuo Tanzania na wengine kutoka nje ni takribani 3500, kwa sababu ni mpango wa miaka mitatu tunaongelea wahandisi takribani 10,500, wale kuwatunza kwa mwezi mmoja ni bilioni 10.
“Kwa maana hiyo mpango huu tungefanya kwa asilimia 100 usaidizi, ungetupeleka mbali kwenye kuongeza kiwango cha wahandisi na ingerudi tu kwa sababu hawa tungewarudisha kwa jamii na kuwapeleka site na wangefanya kazi kwa weledi.
“Kwa hiyo tunaomba Serikali kupata chanzo endelevu cha kusaidia hawa vijana ili mpango wa SEAP usiwe wa hiari uwe wa lazima kama fani ya udaktari,” ameeleza Mhandisi Kavishe.
Amefafanua kuwa uhitaji wa soko la wahandisi mahiri nchini ni 12,000 ikiwa kama nchi ya uchumi wa kati, kwani mhandisi mmoja anatakiwa kuhudumia watu kama 5000.
Naye mgeni rasmi katika hafla hiyo ya kufunga, Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania, Dk. Gemma Modu amewataka wahitimu hao mafunzo waliyopewa katika semina hiyo.
Aidha ameishukuru Serikali ya Norway iliyotoa ufadhili wa wahandisi wa kike na kuwataka wanufaika kuhakikisha wanafuata maelekezo ili bodi iendelee kupata miradi mingine.
Kwa upande wake mmoja wa wanufaika wa mradi wa SEAP mwaka 2018-2021, Mhandisi Nancy Mduma ambaye ni Mhandiri Msaidizi Chuo cha Maji, amesema ni mpango muhimu kwa wahandisi wahitimu wa chuo kwa sababu wanapitia mafunzo maalumu ya kitaaluma na kwenda kuwa wataalamu.
“Zaidi ya yote niwashukuru sana wale wadau wote walioweza kusapoti mpango huu wa SEAP, nawapongeza sana bodi kwa kuwa nipo hivi nilivyo kwa sababu yao. Binafsi nimefaidika sana na mafunzo haya na moja ya faida ni ujuzi wa kitaaluma,” ameeleza Mhandisi Nancy.