29.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Bilionea wa Mil. 7 kwa dakika asomewa mashtaka mapya 222

Watuhumiwa wa wizi wa Sh milioni 7 kwa dakika wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, Mohamed Mustafa Yusufali (kulia) na mfanyabiashara wa Arusha, Samwel Lema wakiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana.
Watuhumiwa wa wizi wa Sh milioni 7 kwa dakika wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, Mohamed Mustafa Yusufali (kulia) na mfanyabiashara wa Arusha, Samwel Lema wakiwa katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana.

Na PATRICIA KIMELEMETA – DAR ES SALAAM,

MFANYABIASHARA aliyetajwa na Rais Dk. John Magufuli, kuwa anajipatia Sh milioni 7 kila baada ya dakika moja, Mohamed Yusufali, maarufu ‘Choma’, amepandishwa tena kizimbani akiwa na mfanyabiashara maarufu wa Arusha na Dar es Salaam, Samuel Lema, wakikabiliwa na mashtaka 222, likiwamo la ukwepaji kodi ya zaidi ya Sh bilioni 14.

Awali, wafanyabiashara hao walitakiwa kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam juzi, lakini ilishindikana kutokana na muda wa mahakama kuisha, ikizingatiwa walikuwa na idadi kubwa ya mashtaka.

Kutokana na hali hiyo, walifikishwa mahakamani hapo jana saa 3:00 asubuhi na kupandishwa kizimbani saa 5:15. Walisomewa mashtaka yanayowakabili mbele ya Hakimu Mkazi, Wilbard Mashauri.

Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri ulikuwa na mawakili wanne wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi.

Wengine ni Jackline Nyantori, Diana Lukondo na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai.

Wakili Mutalemwa, alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo namba 32 ya mwaka 2016 ni mpya ambayo inawakabili washtakiwa hao, na kwamba wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa kati ya Januari mosi, 2012 na Desemba 31, mwaka jana katika mikoa ya Arusha na Dar es Salaam.

Inadaiwa kwa nia ovu, walikula njama na mtu mwingine ambaye hakufikishwa mahakamani ili kukwepa kodi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya Sh bilioni 14.05.

Pia katika shtaka la pili la kughushi, inadaiwa walilitenda Julai 17, mwaka jana Dar es Salaam ambapo kwa pamoja walitengeneza hati ya uongo ili kuonyesha Kampuni ya Northern Engineering Works Limited, imenunua hisa za Kampuni ya Farmplant Dsm Limited kwa Sh milioni 4.3, na kushindwa kulipa kodi, wakijua ni uongo.

Pia katika shtaka la kukwepa kodi linalomkabili mshtakiwa wa kwanza Lema, inadaiwa alilitenda kati ya Januari mosi, 2012 na Desemba 31, 2015 Dar es Salaam.

Inadaiwa akiwa Meneja wa Kampuni ya Northern Engineering Works Limited na Elerai Constructions Ltd ambazo zimesajiliwa kama mlipa kodi kwa Kamishna wa TRA, kwa nia ovu alikwepesha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya sh bilioni 14.05.

Pia katika shtaka la utakatishaji fedha, linalowakabili washtakiwa wote wawili, inadaiwa walilitenda katika nyakati tofauti, kati ya Februari mosi, 2012 na Februari 25, 2013 kati ya jijini Arusha na Dar es Salaam.

Inadaiwa kwa nia ovu, walijihusisha katika uhamishaji wa fedha sh milioni 420 wakitambua ni kinyume na sheria na kuziweka katika Benki ya I&M (T) Ltd tawi la Kariakoo kwa kutumia akaunti yenye jina la Iqbal Jaferali Jafferjee.

Inadaiwa wakati wakiwa wanahifadhi kiasi hicho katika benki hiyo, walitambua fika kama uhamishaji huo umetokana na fedha haramu – za utakatishaji fedha.

Pia katika shtaka la mwisho la 222 la kuisababishia TRA hasara, inadaiwa kuwa walilitenda kwa nyakati tofauti kati ya Januari mosi, 2012 na Desemba 31, mwaka jana katika jiji na mkoa wa Dar es Salaam.

Inadaiwa kwa pamoja, kwa sababu zao za nia ovu, waliwasilisha kwa kamishna wa TRA taarifa za uongo za mrejesho wa kodi jambo lililoisababishia mamlaka hiyo kupata hasara ya Sh bilioni 14.05.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mashauri aliwaambia washtakiwa hao hawatakiwi kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi hiyo.

Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Alex Mgongolwa aliiomba mahakama hiyo kuwasilisha ombi dogo kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai na kuiomba kulifuta shtaka la 221 la utakatishaji fedha kwa sababu halina matakwa ya kisheria.

Alidai hata kama mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza kesi hiyo, ina haki na uwezo wa kupokea maombi yanayoendana na kesi.

Mgongolwa alidai kuwa kutokana na hali hiyo, ombi la kuitaka mahakama hiyo kulifuta shtaka hilo la 221 baada ya kuwapo kwa upungufu wa kisheria, haliwezi kurekebishika wala kufumbiwa macho zaidi ya kufutwa.

Alidai katika sayansi ya sheria, kosa la utakatishaji fedha linatambuliwa katika hatua kubwa nne ikiwemo ‘Blesment; – kuchukua fedha na kuziweka nyumbani ama sehemu ya starehe pamoja na ‘Integration’ – mali iliyojengwa kuuzwa kisha fedha kutumika katika matumizi mengine.

Alidai kutokana na hali hiyo, hawawezi kusema mtu ameiba fedha peke yake ndipo atakuwa ametakatisha fedha, hivyo basi hoja zilizotolewa katika shtaka hilo hazijakidhi matakwa ya kisheria na kwamba ni bora lifutwe kabisa.

Baada ya kusema hayo, Wakili Mutalemwa aliiomba mahakama kuwapa muda wa siku mbili ili waweze kupitia hoja za upande wa utetezi na kuwasilisha majibu yao tarehe itakayopangwa.

Kutokana na hali hiyo, Wakili Mgongolwa aliwataka upande wa Jamhuri kujibu hoja hizo hapo hapo kwa madai kuwa walikuwa na muda mrefu wa kujadili hati ya mashtaka na kuwasilisha majibu.

Hakimu Mashauri alikubaliana na hoja ya upande wa Jamhuri na kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 28, mwaka huu ambapo utawasilisha majibu ya hoja zilizowasilishwa na utetezi katika kesi hiyo huku washtakiwa hao wakirudishwa rumande.

Julai 12, mwaka huu, Choma alipandishwa kizimbani akiwa na wenzake wanne na kusomewa mashtaka 199 yaliyokuwa yakiwakabili likiwamo la utakatishaji fedha na kuisababisha Serikali hasara ya sh bilioni 15.6.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles