NEWYORK, MAREKANI
BILIONEA mfanyabiashara, Michael Bloomberg mwenye utajiri mara 17 ya alionao Rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump anafikiria kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuteuliwa kuwania urais kupitia chama cha Democrat.
Kwa mujibu wa jarida linalofuatilia watu wenye ukwasi duniani, utajiri wa Bloomberg unafikia dola bilioni 52 (£40bn), hii ni mara 17 zaidi ya utajiri wa Trump mwenye ukwasi utajiri wa dola bilioni 3.1.
Bilionea huyo ambaye pia ni meya wa zamani wa Jiji la New York City ana wasiwasi kama wagombea waliojitokeza kupitia chama hicho ni wazuri kuweza kumgalagaza Trump ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2020 atakuwa anawania kipindi cha pili, mshauri wake amesema.
Taarifa zinaeleza kuwa bilionea huyo mwenye umri wa miaka 77 akiwa amempita miaka minne tu Trump anatarajia kuanza mchakato rasmi kuwania nafasi hiyo wiki hii kupitia chaguzi za ndani ya Democrat akitokea Alabama.
Hadi sasa jumla ya wagombea 17 wamejitokeza kuwania nafasi ya kuteuliwa na chama cha Democrat kugombea urais dhidi ya Trump.
Wanaoongoza hadi sasa katika kinyang’anyiro hicho ndani ya Democrat ni Makamu wa Rais wa zamani Joe Biden, Seneta wa Massachusetts, Elizabeth Warren na Seneta wa Vermont, Bernie Sanders.
Kura za maoni zilizotolewa hivi karibuni zimeonyesha kuwa Warren na Sanders ambao wamekuwa wakichukuliwa kama wapinzani wa Biden wanaweza kushindwa kumkabili Trump iwapo watapitishwa na chama chao.
Hadi sasa, wana-Republican watatu wamesema watajitokeza kupambana na Trump katika uchaguzi wa ndani wa chama chao wa kuwania kusimamishwa kugombea nafasi hiyo ya urais 2020.
Mkosoaji wa muda mrefu Trump naye amejiunga na mbio za kusaka nafasi hiyo kupitia Republican.
Lakini inaonekana kuwa ni ngumu kwa mtu yeyote ndani ya Republican kuchukua vazi kutoka kwa rais anayewania kipindi cha pili.
ALICHOSEMA BLOOMBERG
Katika taarifa yake mshauri wake, Howard Wolfson alisema: ” Sasa tunahitaji kumaliza kazi na kuhakikisha kwamba Trump anashindwa.
“Lakini Mike ana wasiwasi zaidi kuwa wagombea waliojitokeza sasa hawana nafasi nzuri ya kufanya hivyo.
” Kulingana na rekodi yake ya kufanikisha, uongozi na uwezo wake wa kuleta watu pamoja ili kuendesha mabadiliko, Mike angeweza kuchukua pambano kwa Trump na kushinda,” alisema Wolfson.
Rais Trump, 73, hadi jana mchana alikuwa hajatoa neno lolote kuhusiana na uamuzi huo wa bilionea huyo ambaye pia ni rafiki yake.
Huko Alabama, hadi kufikia Ijumaa wagombea lazima wawe wamewasilisha nyaraka muhimu ili waweze kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho, na taarifa za kwenye vyombo vya habari zinaeleza kuwa Bloomberg amechagua jimbo hilo kwa sababu limetoa muda mapema wa mwisho wa kujaza fomu.
Mgombea wa urais kupitia Democrat katika uchaguzi wa Novemba 3, 2020 atachaguliwa baada ya michakato kadhaa .
BLOOMBERG NI NANI?
Bloomberg alikuwa ni mfanyakazi wa benki wa Wall Street kabla ya kupata ufalme wa kuzalisha fedha ambao umebeba jina lake.
Mhisani huyo amechangia mamilioni ya dola kwenye elimu, huduma za afya na mambo mengine.
Kwa asili ni Democrat, alikuja kuwa Republican kwa ajili ya kufanikisha kampeni za kuusaka umeya wake wa New York mwaka 2001.
Alitumikia vipindi vitatu vya kama meya hadi mwaka 2012, alijiunga tena na chama cha Democratic mwaka jana tu.
Ikizingatiwa kama Mwanademokrasia wa wastani, amekuwa akiangazia mabadiliko ya hali ya hewa kama suala muhimu, lakini alipoulizwa kuhusu mbio za urais mapema mwaka huu alikanusha .
Bloomberg ni mfadhili mkubwa wa kundi la kudhibiti ‘Everytown for Gun Safety’, ambalo alisaidia kulianzisha mwaka 2014.
Kundi hilo na Bloomberg, limeonekana kuwa nyuma ya ushindi wa Democrat Virginia katika uchaguzi wa majimbo mapema wiki hii.
Kundi hilo na lile linalojulikana kama National Rifle Association la Virginia –lilichangia dola milioni 2.5 katika uchaguzi huo.
JAJI AMTAKA TRUMP AREJESHE MAMILIONI YA MSAADA ALIYOCHUKUA
Ukiachana na habari hizo za kuelezea uchaguzi wa 2020, wakati huo huo, Jaji wa New York amemtaka Rais Trump kulipa Dola milioni mbili za taasisi yake ya misaada alizochukua na kuzitumia vibaya kwa ajili ya kuchangia kampeni zake za urais za mwaka 2016.
Taasisi hiyo ya The Donald J Trump Foundation ilifungwa 2018.
Waendesha mashataka waliishutumu taasisi hiyo kufanya kazi zenye maslahi ya Trump.
Trump ametakiwa kulipa fedha hizo baada ya Jaji kusema kuwa taasisi hiyo ambayo ilikuwa ikiongozwa na Trump mwenyewe pamoja na wanawe wakubwa watatu haikutakiwa kujihusisha na masuala ya kisiasa.
Trump alijibu baada ya hukumu hiyo kutoka akisema “kila senti ilikwenda kwenye taasisi hiyo”.