23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

BILA VITUO VYA POLISI WATU HAWA WATAISHIJE?

NA MARKUS MPANGALA, +255 764 936 655

JESHI la Polisi limepata Kiongozi mpya, Kamanda Simon Sirro. Si mtu mpya kwa kuwa anafahamika tangu makuzi yake. Kiongozi Sirro anafahamika tangu akiwa askari wa cheo cha chini, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo na baadaye Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Hii ni sehemu ndogo tu kumhusu Sirro ndani ya Jeshi la Polisi. Kwa maana hiyo kiongozi huyo mpya aliyechukua nafasi ya Ernest Mangu anao wajibu wa kuendeleza na kuleta ufanisi wa utendaji wa Jeshi la Polisi nchini.

Pamoja na hayo, ninalo jambo linaloniogopesha mno kwenye jamii zetu. Nimechunguza kwa muda mrefu na baadaye kuchora picha ya miaka ijayo, kwamba ni kwa namna gani tutaendelea kuishi katika jamii ambayo haina vituo vya polisi?

Ni kwa vipi wananchi wawe mbali na walinda usalama na mali zao? Ni kwanini wananchi washindwe kupata huduma za kiusalama kupitia kwa polisi kwenye baadhi ya maeneo? Chukulia mfano maeneo yaliyoko mipakani, lakini hayana vituo vya polisi.

Takwimu za Jeshi la Polisi kulingana na tovuti yao (www.policeforce.go.tz) zinaonyesha kuwa matukio ya uhalifu na ajali zilizoripotiwa kati ya Januari hadi Desemba 2015 ni 1,909,685.

Aidha, takwimu hizo zinaonyesha ongezeko la matukio ya uhalifu na ajali ni nyingi kuliko ripoti ya mwaka 2014. Mwaka 2014 matukio ya uhalifu na ajali yaliyoripotiwa ni 1,654,247. Ndiyo kusema ongezeko hilo ni matukio 255,438 sawa na asilimia 15.4.

Idadi ya matukio ya uhalifu pekee yaliyoripotiwa mwaka 2015 ni 519,203. Hata hivyo imeonyesha kupungua kwa uhalifu kwa sababu mwaka 2014 kulikuwa na matukio 528,575. Ikiwa na maana ni pungufu ya 9,372  sawa na asilimia 1.8.

Ripoti ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2015 imeonyesha aina tofauti za matukio ya uvunjaji wa sheria; uhalifu, ujambazi, uporaji, udhalilishaji, unyang’anyi na kadhalika.

Kila mkoa unazo taarifa zake. Nafasi hii haitoshi kutaja mikoa yote na matukio yake ya uhalifu au uvunjaji wa sheria.

Hoja yangu ya leo ni namna ambavyo matukio kama hayo yanapotokea maeneo ambayo hayana vituo vya polisi. Kwamba wananchi watalindwaje katikati ya matukio ya  ghafla ya uhalifu?

Chukulia mfano, katika Wilaya ya Nyasa na vijiji vyake, miji, vitongoji na kadhalika, nini kitatokea iwapo matukio ya uhalifu yatatamalaki huku vituo vya polisi vikikosekana?

Mfano, kutoka Mji wa Lituhui hadi Lundu, katikati hakuna kituo cha polisi. Kutoka Kijiji cha Lundu hadi Mji mdogo wa Liuli hakuna kituo cha polisi.

Kwamba katika mwambao wa ziwa Nyasa kwenye wilaya hiyo, ni miji midogo ya Lituhi, Liuli na Mbamba Bay ndiyo yenye vituo vya polisi. Hii ina maana Lituhi iliyopo kwenye Tarafa ya Ruhuhu inahudumia wananchi wa vijiji vya Njomole, Ndumbi, Liweta, Mbaha, Lundu, Kihanga, Ngumbo, Mkili na kadhalika.

Kwamba katika tarafa nzima ya Ruhuhu kuna kituo kimoja ya Polisi. Vilevile katika tarafa ya Ruhekei kuna vituo vichache, kwa maana ya Liuli na Mbamba Bay pekee.

Swali langu la msingi ni namna gani Jeshi la Polisi linaweza kuhudumia wakazi wa maeneo hayo? Ni kwa vipi wananchi wetu wataweza kupata huduma za ulinzi na usalama wakati wote au nyakati za matatizo?

Ninazungumza hayo kwakuwa mimi ni mwenyeji wa wilaya husika. Kwa mfano, unapofika njia panda kati ya Songea, Mbinga na Nyasa (Kijiji cha Kitai) ina maana ndipo unaachana na huduma za Jeshi la Polisi kwa ukaribu.

Ukifika Kijiji cha Amanimakoro, kuna wawekezaji wa makaa ya mawe kutoka TanCoal. Swali letu linarudi ni kwa vipi katika maeneo hayo tunaweka ulinzi na usalama wa mali za wawekezaji na raia?

Mfano mwingine ni katika Kijiji cha Ndumbi, kuna gati la bandari limejengwa hapo, ikiwa ni ishara ya mwelekeo mpya wa matumizi ya bandari hiyo ambayo kwa miaka mingi imetajwa kuwa na kina kifupi.

Ni nani anahusika kulinda vifusi vya makaa ya mawe au usalama wa raia na mali zao? Namna gani tunaweza kuwahudumia wananchi wetu kwa ufasaha kabla ya kusubiri matukio ya uhalifu na vitendo vya uvunjaji wa sheria?

Ninasema hayo kwa sababu wakazi wa mwambao wa Ziwa Nyasa wanapakana na nchi ya Malawi. Hii ina maana upande wa Magharibi unakuwa wa nchi nyingine. Ni kwa namna gani tunawapa huduma ya ulinzi wa usalama na mali zao? Ni lini tutatambua kuwa maeneo ya pembezoni yanahitaji kuwa na vituo vya polisi kama sehemu muhimu ya kuimarisha ulinzi na usalama?

Jambo zuri ni kwamba Jeshi la Polisi linaendesha mpango wa Polisi Jamii. Binafsi sijawahi kuona wala kusikia kuwa mpango huo unaihusisha wilaya hiyo au jamii hiyo licha ya kutambua kuwa ni suala linalotakiwa kufanyika katika jamii nzima.

Tunaweza kusema matukio ya uhalifu na uvunjaji wa sheria hayafanyiki sana katika  maeneo ya pembezoni au vijijini. Ni kweli, lakini itafaa nini kusubiri matukio yajitokeze ndipo tuanza mikakati ya kukabiliana na matatizo hayo?

Kwa maoni yangu ni kwamba, nchi yetu italindwa kwa mikono, akili na nguvu zetu wenyewe. Ni muhimu maeneo kama hayo kuwekwa vituo vya polisi kama sehemu ya kwanza ya kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi pamoja na rasilimali zetu kabla ya kuwatazama maadui wa nchi yetu. Hatujachelewa. Tuanze sasa kwa kujiuliza hivi jamii iliyopo mbali au isiyo na vituo vya polisi inaishi namna gani.

Baruapepe; [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles