29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, October 21, 2021

BILA POLISI CUF PANGECHIMBIKA LEO

Maalim Seif Sharif Hamad

 

 

NA AZIZA MASOUD – DAR ES SALAAM

ZUIO  la Jeshi la Polisi kwa wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) wanaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kutofanya usafi uliopangwa kufanywa leo katika ofisi za chama hicho, Buguruni, Dar es Salaam, zimeepusha vurugu ambazo zingeweza kutokea baina yao na wafuasi wa Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Taarifa za ndani kutoka upande unaomuunga mkono Maalim Seif, zinaeleza kuwa ufanyaji huo wa usafi ulipangwa kwenda sambamba na kuwaondoa kwa nguvu wafuasi wa Profesa Lipumba katika ofisi hizo.

Mmoja wa wafuasi wa Maalim Seif ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa mbali ya kufanya usafi, pia walijiandaa kupambana na vijana wanaodaiwa kuwa wa Profesa Lipumba, ambao wanaonekana wakifanya mazoezi kupitia video zilizotumwa mitandaoni.

“Yaani polisi wameamua kumlinda Profesa Lipumba, lakini kesho (leo) tulitaka tukawachape kama walivyowapiga watu wetu wiki iliyopita, wana bahati,” alisema mwanachama huyo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, juzi alitangaza kupiga marufuku wanachama hao kwenda kufanya usafi katika ofisi hizo, kwa kile alichoeleza kuwa kutokana na uwepo wa viashiria vya vurugu.

Pamoja na Kamishna Sirro kutoweka wazi viashiria hivyo, lakini ni wazi kulikuwa na kila dalili za kutokea kwa vurugu, hasa baada ya upande wa wafuasi wa Profesa Lipumba nao kuanza kusambaza video zinazowaonyesha wakiwa katika mazoezi eneo linalodaiwa kuwa la ofisi hiyo.

Taarifa ambazo MTANZANIA Jumapili limezipata, zinaeleza kuwa upande unaomuunga mkono Maalim Seif uliazimia kufanya usafi kwa lengo walilodai kuwa ni kukomboa ofisi hiyo kutoka mikononi mwa ‘wahuni’, hasa baada ya wenzao kuvamiwa na kujeruhiwa wiki iliyopita na wafuasi wa Profesa Lipumba.

Hata hivyo, Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah  Mtolea, jana alitangaza kusitisha mpango wao wa kwenda kufanya usafi kwa maelekezo ya barua ya polisi.

Taarifa iliyotolewa jana na Mtolea, ambaye pia ni mratibu wa shughuli ya kufanya usafi huo, ilieleza kuwa juzi walipokea barua kutoka Jeshi la Polisi Wilaya ya Buguruni, yenye kumbukumbu namba  BUG/SO.7/2/VOL.II/122 ya Aprili 27, ikishauri na kuzuia wanachama wa CUF kufanya usafi uliokusudiwa kwa hoja ya uvunjifu wa amani.

Alisema baada ya kuipokea barua hiyo iliyosainiwa na Taraja Cibe – SSP, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Buguruni na baadae taarifa ya barua hiyo kutangazwa na Kamishna Sirro, walilazimika kufanya kikao cha mashauriano baina ya wabunge, wakurugenzi wa chama na Kamati ya Uongozi Taifa na kuazimia kwenda kumwona Kamishna Sirro.

“Kutokana na makubaliano ya utekelezaji wa pande zote mbili (Jeshi la Polisi na Uongozi wa CUF), Kamati ya Uongozi ya CUF – Taifa imeona ni busara kutoa muda zaidi kwa Jeshi la Polisi kuchukua hatua walizojiwekea juu ya masuala yaliyojitokeza, hivyo tunawaomba wanachama na viongozi wote kukubaliana na kuahirisha zoezi la kufanya usafi katika ofisi yetu ya Buguruni kesho (leo) kama ilivyokuwa imepangwa.

“Mimi kama mratibu wa zoezi hilo na kwa niaba ya wanachama wa CUF Wilaya ya Temeke ambako mimi ni mbunge, nimeridhishwa na maelekezo haya ya viongozi wangu wa juu na nawaomba sote tuyakubali, walau kwa kipindi hiki,” alisema Mtolea.

Alisema kabla ya uamuzi huo, Kamati ya Uongozi ya Taifa chini ya Mwenyekiti wake Julius Mtatiro,  imechukua hatua za makusudi kuwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini – IGP Ernest Mangu ili kuhakikisha kuwa usafi huo unafanyika kwa amani.

Aliongeza kuwa baada ya mawasiliano na majadiliano hayo, Jeshi la Polisi limeahidi kuchukua hatua za kuwadhibiti wahalifu wote ambao wamekuwa wakiitumia Ofisi Kuu ya CUF Buguruni kuratibu vitendo vya kijinai.

Alisema Jeshi hilo pia limeomba lipewe muda zaidi kuchunguza na kushughulikia matukio ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu wote waliopanga njama za uvamizi wa viongozi na wanahabari katika katika mkutano wa chama hicho uliofanyika Hoteli ya Vina, Mabibo, ikiwamo kumsaka mtu aliyekuwa na bastola.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya ambaye ni mfuasi wa Profesa Lipumba, ameachiwa kwa dhamana baada ya juzi Kamanda Sirro kutangaza kumkamata na watu wengine sita kwa madai ya kuhusishwa na vurugu katika mkutano wa chama hicho uliokuwa umeandaliwa na wafuasi wa Maalim Seif.

Kamanda Sirro juzi aliwaambia waandishi wa habari kuwa jeshi hilo linamshikilia Kambaya na Twaha Abdalla (47) na wengine sita na kwamba jalada lao teyari limeshapelekwa kwa wakili wa Serikali.

Alipotafutwa kwa simu na gazeti hili jana, Kambaya ambaye juzi alionekana akiwa na Profesa Lipumba akitokea Ofisi ya Msajili wa Vyama, walikokwenda kwenye kikao cha usuluhishi, awali aligoma kuzungumzia suala hilo, huku akisisitiza kuwa hajakamatwa isipokuwa aliitwa polisi kwa mahojiano.

“Nyinyi waandishi mnakuza mambo, mimi sijakamatwa, ninachojua niliitwa polisi kwa ajili ya kwenda kuhojiwa, lakini tahariri zote mnahoji kwa nini Kambaya hakamatwi, mnataka nikamatwe na leo (jana) mmeandika nimekamatwa, maana ugomvi wenu mmeuhamishia kwangu, siwezi kuongea, mimi ni mtu mdogo sana katika hii nchi, sidhani kama itakuwa na faida,” alisema Kambaya.

Alipobanwa na kuambiwa juu ya kauli ya Kamanda Sirro ya kumkamata na wenzake sita, ghafla alibadili lugha na kudai kuwa aliachiwa kwa dhamana.

 “Nilikamatwa  majuzi (juzi), nimeachiwa kwa dhamana, mimi ni mshtakiwa, nina haki ya kudhaminiwa na dhamana ni haki yangu, siwezi kuongea tena zaidi ya hapo, maswali mengine kamuulize Sirro, maana naona sasa ugomvi wenu wote mmehamishia kwa Kambaya,” alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,682FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles