BIL. 4.5/- ZAIFUNGA STAR TV, RFA

0
903

Na MASYENENE DAMIAN -MWANZA


KAMPUNI ya Sahara Communication, imefungiwa kurusha matangazo yake kutokana na deni la malimbikizo ya kodi ya Sh bilioni 4.5 inayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Licha ya kufungiwa kwa matangazo yake, kampuni hiyo inayomiliki vyombo vya habari vya Star TV, Redio Free Africa (RFA) na Kiss FM imepewa muda wa  siku 14 kukamilisha malipo ya deni hilo ama ipigwe mnada endapo itashindwa kulipa kwa muda huo.

Kazi ya kuifungia kampuni hiyo ilifanywa na Kampuni ya udalali ya Sukah Auction Mart and Court Brokers ya jijini Mwanza, ambayo ni Wakala wa ukusanyaji kodi wa TRA ambapo walifunga sehemu ya ofisi za Kampuni ya Sahara yenye makao yake makuu wilayani Ilemela, mkoani Mwanza jana.

Akizungumza jana baada ya kufunga sehemu ya ofisi hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Sukah, Sukah Saleh alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuelekezwa na TRA kuvifunga vituo vya Star TV, Kiss FM na RFA na kuvisimamisha kutorusha matangazo hadi pale deni hilo litakapolipwa.

“Maagizo ni kwamba vituo hivi visiwe hewani kwa hiyo sisi tumefunga kama vitaendelea kuwa hewani basi vitakuwa vimekiuka masharti.

“Wanadaiwa kiasi cha Sh bilioni 4.5 kwa hiyo wamepewa siku 14, walipe na wakishalipa ndiyo watafunguliwa na kama siku 14 zikiisha hawajalipa tunakuja kupiga mnada mali zao,” alisema.

Naye Ofisa kutoka TRA ambaye alisimamia zoezi hilo, Rogart Tairo, alisema zoezi hilo ni utekelezaji wa sheria namba 61 ya usimamizi wa fedha ya mwaka 2015, ambapo hutekelezwa kwa mdaiwa sugu kama Kampuni ya Sahara.

“Hii ni hatua ya mwisho kabisa ya ukusanyaji kodi, imefikiwa baada ya taratibu zote kushindikana mfano kudai kwa njia ya kawaida, kuandikiana barua na kwenda benki kuangalia kama kuna fedha za kufidia deni hili, tunafunga leo kwa hatua ya mwisho ikishindikana na hapo tutapiga mnada mali zake,” alisema Tairo.

Kwa upande wake Meneja Utumishi na Utawala wa Kampuni ya Sahara, Raphael Shilatu, alisema wamekutwa na hali hiyo kutokana na malimbikizo ya muda mrefu yaliyosababishwa na uwekezaji mkubwa walioufanya kutokana na kuhama kutoka analogia kwenda dijitali.

“Wakati wa kuhama kutoka analogia kwenda dijitali tulifanya uwekezaji mkubwa uliotugharimu sana kwa sababu tulikopa fedha benki.

“Jambo hili ni la ghafla sana siwezi kusema ni kiasi gani tunadaiwa lakini niwatoe wasiwasi wasikilizaji na watazamaji wetu kwamba ni jambo la muda mfupi kampuni inafanya jitihada kuhakikisha inalimaliza tatizo hili na vyombo vyake vinarudi hewani,” alisema Shilatu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here