MEI 5, mwaka 1993 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika familia ya mzee Murhimanya, alizaliwa Bien-Aime a.k.a Bien Melody, msanii wa muziki kizazi kipya anayeiwakilisha vyema nchi yake Australia.
Bien Melody mbali na kuimba ni mtunzi wa nyimbo, mpiga piano, mtayarishaji wa muziki na Dj ambaye alianza kufahamika mwaka 2018 baada ya kuachia wimbo wake wa kwanza unaoitwa, Sio Vitisho.
2019, aliweza kutajwa katika tuzo za African Music Awards Australia na mwaka huo huo alitoa wimbo, Jiachie aliomshirikisha staa wa Bongo Fleva, Beka Flavour ambao ulimpa mashabiki Australia na Afrika Mashariki huku ukishika namba sita kati ya nyimbo kali zenye vionjo mchanganyiko kutoka Australia na Afrika.
MAISHA YA KAWAIDA
Bien alizaliwa na kukua katika familia ya dini ya Kikatoliki na muziki aliuanza akiwa kwenye kwaya kanisani. Katika kipindi hicho Bien alijiunga na vikundi mbalimbali vya kwaya na baadaye akawa kondakta wa daladala kabla hajarejea tena kwenye sanaa ya muziki.
Miongoni mwa kwaya ambazo Bien alizitumikia ni Coeur Sacré ya Kongo na Jeunesse Regina Mundi iliyopo Bujumbura nchini Burundi.
Bien alijifundisha mwenyewe jinsi ya kusomaÂ
muziki na kupiga piano na baada ya kumudu muziki wa kanisani na baadaye akaamua kufanya muziki wa kizazi kipya akiwa msanii binafsi.
AKIWA MSANII BINAFSI
Mwaka 2017 aliachia wimbo wake wa kwanza akiwa msanii binafsi unaoitwa, Nakuitaji ambao aliutengeneza mwenyewe na ulishaondolewa kwenye mtandao wa YouTube.
Jina la Bien lilipata kuchomoza kwenye tuzo mbalimbali kutokana na muziki wake pamoja na kuchekesha katika majukwaa ya matamasha (Sanaa Festival) huko Kusini mwa Australia, Adelaide.
LEBO YAKE
Bien Melody ameunda rekodi lebo yake mwenyewe inayoitwa BM Production ambapo yeye ni Mkurugenzi Mtendaji na mzalishaji mkuu wa muziki.
Bado hajamsaini msanii yeyote kwenye lebo yake lakini amekuwa akitamani kukuza zaidi muziki wa Afrika nchini humo kwa kufungua matawi ya BM Production nchini Tanzania na Burundi.