26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Biashara ya nyamapori na mapambano ya ujangili

Na Bakari Kimwanga-DAR ES SALAAM 

KWA muda mrefu Taifa limekuwa likigubikwa na matukio kadhaa ikiwamo suala la uwindaji haramu ambao pia huchochea ujangili katika maeneo maalumu yaliyohifadhiwa na hifadhi za taifa kwa ujumla.

Kutokana na hali hiyo kila wakati Serikali imekuwa ikiandaa mikakati mbalimbali ambayo itasaidia katika kupunguza au kuondoa kabisa ujangili nchini.

Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kama mkakati  wa kudhibiti biashara hiyo lakini bado sehemu ya kubwa ya majangili wamekuwa wakitumiwa na baadhi ya watu yakiwamo mahoteli makubwa kwa lengo la kupata aina fulani nyama kwa ajili ya kuwauzia wateja wao wanapokuwa kwenye mapumziko.

Internews East Afrika kwa kushirikiana na Earth Jornalism ni wadau muhimu katika kufuatilia masuala la hifadhi kwa nchi za Afrika ikiwamo Tanzania.

Mmoja wahudumu wa hoteli moja moja jijini Arusha ( jina linahifadhiwa), Joseph Makubwa ( si jina lake halisi kwa sababu za usalama) anaeleza kwamba kwa katika hoteli yao wamekuwa wakipokea wageni mbalimbali wakiwamo watalii kutoka nchi za nje, ambapo wapo baadhi yao hupenda kula nyamapori na hata kufikia kutoa fedha ili waweze kupata huduma hiyo.

“Je wewe unatoka wapi? Kama unataka nyamapori sema utapata maana hapa huwa kuna watu maalumu ambao sisi huwapa kazi na wao kwenda kwenye maeneo ya porini na kutuletea ingawa bei huwa juu kidogo.

“… kama unataka swala wao hutuuzia; nyama ya nyumbu, swala na digidigi huuzwa hadi Shilingi 30,000 hadi 50,000 kwa kilo. Lakini hii hufanyika kwa usiri mkubwa sana na si kawaida kama unavyofikia na kwa kuwa wewe ni mteja wetu na umekaa hapa kwa muda wa siku nyingi tunaweza kukusaidia ila ninakuomba sana wasijue watu wengine. Kwa kuwa umeniambia mimi kama mpishi inatosha kabisa kukupatia hitaji lako,” anasema Makubwa

Kutokana na hali hiyo mwandishi wa makala hii alilazimika kutoa kiasi cha Sh 30,000 ili aweza kutengenezewa nyama ya swala na mpishi huyo, lakini katika hali isiyo ya kawaida badala ya kupata kwa kiasi cha makubaliano, alijikuta akitengenezewa nusu yake na kuambiwa kwamba niwe mvumilivu kwa kuwa hali si nzuri na wawindaji wameahidi itapatikana kwa wingi baada ya siku nne.

Hali hiyo iliibua shaka kubwa na hata kubaki na maswali kadhaa je ile nyama nusu ilitoka wapi na ilipatikana kwa njia gani na je sheria inazingatiwa katika uwindaji wa wanyamapori ambao bidhaa zake huuzwa?

HALI ILIVYO

Wakati serikali ikihangaika kudhibiti rasilimali wanyama ili zisimalizwe na majangili, imebainika kuwa baadhi ya hoteli kubwa za kitalii na watu binafsi kuwa ndio chanzo cha mtandao wa soko la wanyamapori nchini, ikiwamo nyumbu, swala na digidigi.

Hatua hiyo inatajwa kama moja ya kikwazo cha kufifisha uchumi wa Taifa kwa na vijiji vinavyozunguka Hifadhi za Taifa pamoja na mapori ya akiba.

Wakizungumzia hali hiyo viongozi wa Jumuiya ya Wanyamapori ya Burunge, ambayo inapakana na Hifadhi za Taifa za Tarangire na Manyara.

Akitoa ufafanuzi huo, Mwenyekiti Mstaafu wa jumuiya hiyo, Noah Teveli, anasema kuwa utafiti wao umebaini soko hilo.

Kutokana na hali hiyo anasema ni lazima kuwepo na mkakati wa kina wa kudhibiti biashara hiyo haramu ambapo kwa sasa rasilimali wanyama wanaweza kumalizika.

“Wapo wanawinda kinyume cha sheria ikiwamo digidigi, swala lakini kama ulivyouliza inakuaje nyumbu ambaye ukubwa wake kama ng’ombe lakini soko lake halijulikani. Ukweli ni kwamba tangu mwaka 2007, tumekuwa tukiendesha tafiti mbalimbali ambapo tumebaini pasi na shaka licha nyama hizi kuuzwa kwa wana vijiji lakini pia zipo baadhi ya hoteli kubwa za kitalii nazo zimekuwa zikinunua nyama hizi kisiri.

“Na si hizo tu hata baadhi ya taasisi na watu binafsi wenye uwezo wao hapa nchini nao hawataki kula nyama zingine zaidi ya za porini, hili lipo na sasa ni lazima kuwapo na mkakati maalumu wa kudhibiti hili. Na mtandao wa wanaouwa wanyama wetu wapo hata baadhi ya askari ambao wamekuwa wakishirikiana na mtandao wa majangili kwani wakati mwingine hutumika na silaha za askari wetu.

“Sasa nini cha kufanya ndio maana sisi Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge, tumelazimika kuongeza nguvu ikiwamo kutolewa kwa mafunzo ya mara kwa mara kwa askari wetu kwa kushirikisha vyombo vingine vya usalama ikiwamo hata jeshi letu,” anasema Teveli.

MAJANGILI 25 MBARONI

Kutokana na kile kinachooneka kufanikiwa kwa mapambano dhidi ya ujangili wa tembo na wanyama wengine kufanikiwa, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanyamapori Burunge, Benson Mwaise, anasema kuwa  kwa mwaka 2016/17, walifanikiwa kuwakamata majangili zaidi ya 25 ambao walikuwa wakiuwa wanyama kinyume cha sheria.

Anasema baada ya kuwakamata majangili hao wamewafikishwa mahakamani ambapo hadi sasa kesi 13 zimeshatolewa uamuzi ikiwamo washtakiwa kufungwa huku kesi tia zikiendelea kusikilizwa.

Mwaise anasema kuwa, baada ya kuimarishwa kwa doria katika maeno yote ya hifadhi wameona mafanikio ikiwamo kuongezeka kwa wanyama wa aina mbalimbali ambao wamekuwa wakichangia uchumi wa Taifa kwa zaidi ya asilimia 80.

KIKOSI CHA UJANGILI

Kamanda wa Kikosi  Dhidi ya Ujangili  (KDU) Kanda ya Kaskazini ambacho kipo chini ya  Mamlaka ya usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mbanjoko Peter, anasema kuwa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika mapambano dhidi ya  watu wanaojihusisha na ujangili wa uwindaji wa wanyama kwa ajili ya kitoweo na biashara.

“Changamoto ya uwindaji wa nyamapori (BUSH MEAT) lipo zaidi  katika maeneo ya Longido, Simanjiro na Loliondo, ambapo kwa sasa tumeyaweka  chini ya uangalizi wa vikosi vya ulinzi, kuhakikisha tunatokomeza aina yoyote ya ujangili huku magari, baiskeli, pikipiki pamoja na nyaya zinazotumika kwenye ujangili huo tunazishikilia .

Anasema kuanzia Julai 2018 mpaka sasa tayari watuhumiwa zaidi ya 113 wamekamatwa kwa kuhusika na makosa ya ujangili, ambapo waliitaka jamii kutambua kwamba rasilimali wanyama ikitunzwa vizuri itaendelea kukuza uchumi wa nchi na kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles