30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Biashara matairi ya mitumba sasa basi

MTZ UCHUMI HII SAFI.inddNa Deus Mhagale, Dar es Salaam

NIPO Mtaa wa Kongo, Dar es Salaam ambao ni maarufu kama ilivyo mitaa mingine ya Tandamti, Livingstone na Pemba yenye pilikapilika nyingi za biashara.

Mtaa wa Pemba umekuwa maarufu kutokana na vijana wengi kushirikiana na vibaka na wanaofanya biashara karibu na soko la Kariakoo.

Ukiibiwa simu yako sehemu yoyote katikati ya jiji ukienda Mtaa wa Pemba kistarabu utauziwa lakini ukijifanya mjuaji huipati.

Hiyo ni sawa na Mtaa wa Gerezani ambao ni maarufu kwa kuuza vifaa vya kwenye magari vilivyoibwa. Ukitaka kuvipata unauziwa kwa bei nzuri, ukitaka kuvichukuwa bure unaweza kuviona kwa macho tu na vikateketezwa vyote huku ukishuhudia.

Katika Mtaa wa Kongo pamoja na nyumba nyingi za wenyeji kuuzwa, sasa yamefumuka maghorofa lakini biashara inayoendeshwa ni ya ‘maisha ya watu’.

Kama Serikali haitaiangalia kwa macho mawili biashara hiyo maisha ya Watanzania yataendelea kupukutika.

Mtaa huo umetokea kuwa maafuru kuuzwa matairi makuukuu yanayotoka katika kila kona ya dunia hii.

Hapa ndipo naingiwa na wasiwasi kama kweli viongozi tuliowapa dhamana ya kuongoza nchi hii wana nia nzuri na maisha yetu, magari wameruhusu kuingizwa makuukuu au kwa msemo maarufu ya mitumba.

Wanaruhusu hata matairi, serikali iingilie kati kiwanda chetu cha General Tyre ili kianze kufanya kazi tuondokane na kiama hiki cha matairi hayo.

Mwasisi wa Taifa hili alikuwa na nia nzuri ya kuanzisha viwanda mfano vya nguo, kila mkoa ulikuwa na kiwanda chake hususan wanakolima pamba.

Lakini kwa viongozi walioachiwa baada ya yeye kustaafu waliamua kuachana navyo na sasa tunashuhudia mitumba ya kila aina hata nguo za ndani tunaletewa  tuvae.

MTZ UCHUMI HII SAFI.inddNguo ni tofauti na matairi, tairi linabeba zaidi ya watu wawili katika gari, hapo ndipo naona umuhimu wa serikali kuliwezesha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kuajiri wafanyakazi wengi katika kila kona na mipaka ya nchi kudhibiti biashara hiyo.

Kamishna wa Polisi na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga,  anasema hapa nchini zaidi ya watu 4000 hufa kila mwaka kutokana na ajali za barabarani.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Kamanda Mpinga anashauri watu wabadilike na kuviheshimu vyombo vya moto na kujali maisha ya watu ambayo hayana mbadala pindi ajali inapotokea.

“Washirikiane na TBS kutokomeza biashara hii ya matairi ya mitumba, askari peke yake hawawezi kutokomeza kwani walengwa ni wananchi. Hivyo kwa ushirikiano wa pamoja itatokomezwa na kubaki historia,” anasema Mpinga.

Naye Mkurugenzi wa TBS, Joseph Masikitiko, anasema ajali nyingi zimekuwa zikitokea kutokana na matairi na magari ya mitumba kutoka nje.

“Matairi yana muda wake wa matumizi, hata yale mapya  yanapokaa stoo bila kutumika yanamaliza muda wa kutumika na kama litafungwa kwenye gari linaweza kusababaisha ajali. Hata kwa magari ndiyo maana kuna muda wa matumizi ya gari ukipita na ushuru wake unakuwa mkubwa.

“Baadhi yetu tunadhani kwamba tairi hata likiwa jipya likikaa muda mrefu bila kutumika haliwezi kuisha muda wake na kuwa kama la mitumba. Ndiyo maana waagizaji wajanja wamekuwa wakiyauza kama mitumba baada ya kubaini yameisha muda wa matumizi yake.

“Shirika langu limeamua kuanzia sasa kupiga marufuku biashara hii ya matairi ya mitumba,” anasema Masikitiko.

Anasema wanaendelea kuwasaka watu wanaohusika na biashara hiyo ili kuwafikisha katika vyombo vya sheria kwani kufanya hivyo ni kusababaisha vifo kwa wananchi wasiokuwa na makosa.

Naye mfanyabaishara wa matairi makuukuu katika Mtaa wa Kongo, Katimba Mbonde, anasema amefanya biashara hiyo kwa miaka mitano sasa na tairi moja huuzwa kwa makubaliano kati ya Sh 150,000 hadi 300,000 kutegemea na nchi lilikotengenezwa na ubora wake.

Anakiri kwamba kuna wafanyabishara wengine wanawaharibia biashara hiyo kwa kuchonga matairi na kuifanya kuwa ya utapeli.

Juma Ali wa Kinondoni, Dar es Salaam anayejishughulisha na biashara hiyo kwa mwaka wa 15 sasa, anaiomba Serikali kufanya uchambuzi wa kina ili kuwabaini wanaouza matairi yaliyochakachuliwa.

Anatolea mfano wa nguo za mitumba kuwa kuna madaraja ya kwanza hadi ya nne na kwamba yeye huuza matairi ya daraja la kwanza hadi la pili.

“Wanaochonga tairi hizo kweli wapo na sisi tumekuwa tukiwapiga vita, lakini kutokana na wafanyabiashara hao kufahamiana na wakubwa wamekuwa wakiendelea na biashara hiyo bila kuguswa,” anasema Ali.

Wafanyabishara hao wanaiomba TBS na Serikali kuendesha msako wa kuwakamata wanaochonga matairi kwani yanasababisha ajali nyingi nchini.

“Ukionyeshwa tairi lililochongwa utadhani ni jipya na kama huna uzoefu wa matairi unaweza kununua bila shaka,” anasema dereva mmoja wa daladala.

Ukiacha vifo vinavyosababishwa na ugaidi duniani ajali za magari zinaweza kuchukua nafasi ya pili kwa kuteketeza wingi wa watu masikini kwa matajiri.

Kulingana na Ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), ajali za barabarani zinaendelea kupoteza maisha ya watu wengi huku ikikadiriwa kuwa watu milioni 1.25 hufariki kila mwaka.

Inaelezwa kuwa ajali za barabarani ndio zinaongoza kusababisha miongoni mwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 29.

Ripoti ya WHO pia imegundua mwanya mkubwa katika maeneo ya usalama wa barabarani na vifo kati ya nchi maskini kwa kuendekeza kutumia matairi makuukuu.

Inasema asilimia 90 ya vifo vya ajali za barabarani vinatokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, japokuwa wana asilimia 54 ya magari duniani.

Mkuu wa kitengo cha magonjwa yasiyoambukiza katika WHO, Etienne Krug anasema kiwango cha juu kabisa cha vifo vya ajali za barabarani kipo barani Afrika kikifuatiwa na mashariki ya kati.

“Afrika ina asilimia mbili pekee ya magari duniani, lakini ina kiwango cha juu sana cha vifo vya barabarani. Baadhi ya nchi kama vile Sweden, Uingereza, Uholanzi wameweza kupunguza viwango vya vifo kwenye barabara zao kwa zaidi ya asilimia 80 katika miongo iliyopita kwa kutekeleza  hatua  kadhaa zinazoeleweka  vyema.

“Tunazungumzia kuhusu kuboresha sheria na kuziimarisha, hususani kwenye vipengele hatari kama vile mwendo kasi, kunywa kilevi, ubora wa magari na matairi na vifaa vyake na kuendesha, kutumia kofia maalum unapoendesha pikipiki, kufunga mkanda na kiti cha mtoto,” anasema.

Krug anasema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, nchi 17 zimekuwa na mafanikio kwa kuweka sheria kali za usalama barabarani.

Ripoti ilionyesha kwamba ajali za waendesha baiskeli na watembea kwa miguu zinafikia asilimia 26 ya vifo vyote vitokanavyo na ajali za barabarani, ambapo idadi hii inafikia asilimia 33 barani Afrika.

Ripoti pia iligundua kwamba baadhi ya magari yaliyouzwa katika asilimia 80 ya nchi zote yameshindwa kufikia viwango vya msingi vya usalama.

IMG_0832Je tairi la gari lina athari gani katika usalama barabarani?

Mhandisi msanifu wa matairi, Tunzo Mnzava, anasema matairi ya magari yanachangia zaidi ya asilimia 60 za ajali za magari katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.

“Sababu za tairi kuleta ajali ni pamoja na kupasuka wakati gari likitembea. Tairi laweza kupasuka kwa sababu nyingi. Kati ya sababu hizi ni kuwa halina uwezo kuhimili ama mwendo au uzito uliobebwa.

“Sababu nyingine ni kuwa na mgandamizo mdogo au mkubwa wa hewa kuliko kiwango kinachopendekezwa,” anasema Mhandisi Mzava.

Mhandisi huyo anasema tatizo linaloonekana kuwa kubwa zaidi ni kutumia matairi ambayo hayana ubora wa viwango vizuri na matumizi ya matairi ambayo kashata zake zimeisha sana hadi kuteleza. Tairi za jinsi hii hazina msuguano mwema na barabara, hivyo kuteleza.

Kulingana na Mhandisi huyo, tairi hufanya gari kuwa gumu kuliendesha. Anasema tatizo hilo lina sababu kadhaa zikiwemo mfumo wa gari, umahiri wa dereva na aina ya tairi zilizotumika hasa kwenye ekseli ya mbele.

“Utafiti unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya ajali zinazotokana na ugumu wa kuendesha gari zinasababishwa na aina ya tairi zilizotumita, mitamo ya tairi inaweza kusababisha gari likawa gumu au jepesi kuendesha,” anasema.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,391FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles