26.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

BENKI YA TADB KUWEZESHA KILIMO CHA UMWAGILIAJI

Na Mwandishi Wetu

-Kilombero

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema itaipatia mikopo mikubwa miradi yote inayolimwa kibiashara kwa kutumia teknolojia ya umwagiliaji na kuongeza tija na kuwa na uhakika wa mazao, hivyo kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchi.

Ahadi hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Francis Assenga wakati alipotembelea na kukagua miradi iliyokopeshwa na benki hiyo Wilaya ya  Kilombero mkoani Morogoro.

Alisema kuwa ili kuchagiza na kusaidia mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini wakulima nchini hawana budi kugeukia kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza tija kilimo chao.

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa matumizi madogo ya umwagiliaji katika shughuli za kilimo zimesababisha taasisi nyingi za kifedha hasa mabenki kuhofia kukopesha sekta ya kilimo nchini.

“Ili kuninua uzalishaji wenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini hakuna budi wakuliwa wageukie kilimo cha umwagiliaji ukitilia maanani nchi yetu imejaaliwa vyanzo vingi vya maji ambavyo vikitumiwa kwa busara itachagiza tija katika uzalishaji,” alisema Assenga.

Aliongeza kuwa benki ya kilimo inalenga katika kuinua uzalishaji wenye tija katika sekta ya kilimo kwa kuendeleza miundombinu muhimu, mathalani skimu za umwagiliaji, usafirishaji, hifadhi ya mazao, usindikaji na masoko.

Kwa mujibu wa Asseanga, mikopo hiyo italenga pamoja katika kuboresha miundombinu inayolenga kupunguza mapengo ya upatikanaji wa fedha katika minyororo ya ongezeko la thamani ya kipaumbele.

“Katika kutimiza yote haya, benki imedhamiria kuboresha kwa upatikanaji wa mikopo na huduma za kifedha kwenye miradi ya maendeleo ya Kilimo kwa riba nafuu zilizo chini ya viwango vya kibiashara kwenye soko,” alisema

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilombero,  James Ihunyo  aliwaasa wakulima hao kurudisha mikopo kwa wakati ili wakulima wengine waweze kupatiwa mikopo hiyo.

“Lengo la mikopo hiyo ni kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini, hivyo kuchelewesha mikopo hiyo kwa makusudi ni kurudisha nyuma juhudi hizi,” alisema.

DC huyo aliwasihi wakulima kutambua dhamira ya serikali ya kujali umuhimu wa kilimo kwa kuwaanzishia benki hiyo ambayo imedhamiria kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa kuleta mapinduzi yenye tija katika sekta ya kilimo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles