26.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

BENKI YA NMB YAFUNGUA TAWI LA 31 NYANDA ZA JUU

Na MWANDISHI WETU

-MBEYA

BENKI ya NMB imefungua matawi saba kwa mpigo katika mikoa sita katika juhudi za kujiimarisha zaidi na kuwa karibu na wateja wake wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Kufunguliwa kwa matawi hayo sasa yamefikia 31 kwa mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi.

Matawi ambayo yamefunguliwa na yanatoa huduma kwa jamii ni pamoja na  Kasumulu, Uyole, Mkwajuni, Wanging’ombe, Laela na Kalambo pamoja na Mlele.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Tawi la NMB Uyole lililopo mkoani Mbeya, Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu, Badru Iddy, alisema lengo la benki hiyo ni kusogeza huduma zaidi kwa wananchi ili kuwa karibu na wateja wake.

“Kuzinduliwa kwa tawi hili la NMB Uyole, mahali hapa kunafuatia mahitaji ya muda mrefu ya wateja wetu wa Uyole kupata tawi la NMB lenye nafasi ya kutosha.

“Eneo hili ni karibu zaidi na wafanyabiashara wengi ambao ni wateja wetu wakubwa na wananchi kwa ujumla. Tawi hili kama yalivyo matawi yetu mengine nchini linatoa huduma zote za kibenki zitolewazo na benki yetu,” alisema Badru.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ambaye aliwataka wananchi wa kufungua akaunti katika benki hiyo kwani Serikali ina hisa asilimia 32.

Makalla aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa tawi la Uyole ambapo alisema Benki ya NMB ni sawa na pacha wa Serikali kwani imepeleka huduma kila zilipo ofisi za Serikali.

“Hapa tuelewane, Serikali na Benki ya NMB ni sawa na mapacha kwa kuwa kila mahala ambapo Serikali imepeleka huduma zake za kijamii benki hii hufuatia kwa kuweka huduma za kifedha ili kuwahudumia wananchi wa eneo husika,” alisema Makalla.

Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Jeremiah, aliwataka wananchi kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na hivyo kutumia fursa zinazotokana na Benki ya NMB kukuza uchumi wao na taifa kwa jumla.

 

Hayo aliyasema kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Chiku Galawa, kwenye uzinduzi wa tawi la NMB Mkwajuni wilayani Songwe.

Alisema desturi ya kuhifadhi fedha  benki kunajenga nidhamu ya matumizi ya fedha kuepuka madhara ambayo yanaweza kutokea.

Awali akizungumza wakati wa uzinduzi wa Benki ya NMB Tawi la Mkwajuni, Ofisa Mkuu wa Ukaguzi wa Ndani, Augustino Mbogella, alisema mkakati wa kibiashara wa NMB ni kuhakikisha Watanzania wengi wanapata huduma za kifedha.

“Benki ya NMB imeendelea kuwa benki yenye mtandao mpana wa matawi na ATM kuliko benki nyingine yoyote hapa nchini kwa kuwa na matawi zaidi ya 200 huku ikiwa na mashine za kutolea fedha (ATM machines) zaidi ya 700 nchi nzima na wateja zaidi ya milioni 2.5,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles