25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Benki ya Maendeleo, Airtel Money na FSDT waungana

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

BENKI ya Maendeleo Plc imetangaza kuungana na Airtel Money pamoja na FSDT kwa kuzindua kampeni ya Timiza Biashara ambayo inalenga kusaidia vikundi vidogo vidogo vya wajasiriamali, maarufu kama Vicoba ili kuweza kuweka akiba pamoja na kukopa kwa njia ya kidigitali.

Akizungumza jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo, Dk. Ibrahim Mwangalaba alisema hatua ya kuungana na Airtel Money itakuwa na manufaa kwa Watanzania.

“Kwa kuungana na Airtel Money, benki yetu inayo furaha kuzindua suluhisho hili la Timiza Biashara inayowalenga wajasiriamali na wafanya biashara wadogo na wa kati hapa nchini.

“Huduma hii imelenga kutimiza biashara yako na kuleta suluhu ya changamoto ambazo zimekuwa zikivipata vikundi wakati wa kuweka na kukopa katika maeneo mbalimbali wakati inapokuja suala la kuweka akiba na kukopa,” alisema Dk. Mwangalaba. 

Alisema kupitia mpango wa Timiza Biashara pamoja na huduma ya Timiza Vicoba inayowezeshwa na mtandao wa Airtel, kwa sasa inawawezesha wateja kuunda kikundi cha watu kuanzia watano hadi 50.

“Kikundi kinaweza kuundwa na watu kutoka sehemu yoyote Tanzania na sio lazima wanakikundi kuwa eneo moja ili kuweza kupata huduma hii. 

“Wanakikundi wanaweza kuamua siku gani wataweka akiba zao, mikopo itakuwa ya muda gani na wakati gani watakuwa wanafanya marejesho ya mikopo yao,” alisema Dk. Mwangalaba. 

Aliishukuru FSDT ambao wamedhamini kampeni hiyo kwa nia ya kutoa suluhisho la changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara na wajasiriamali. 

Kwa upande wake, Mkurungenzi wa huduma za Airtel Money, Isack Nchunda alisema; “Kampeni ya Timiza Biashara inalenga wajasiriamali na wanavikundi ambao wataunda kikundi cha watu kati ya watano na 50 na baada ya hapo wanaweza kuanza kuweka akiba na kukopa kupitia Timiza Vicoba inayopatikana Airtel Money. 

“Lengo la kuzindua kampeni hii ya Timiza Biashara inayotangaza huduma ya Timiza Vicoba ni kuwajengea Watanzania tabia ya kujiwekea akiba na sana sana kwa wajasiriamali pamoja na wafanyabiashara wadogo.

“Tunalenga kufikisha huduma za kifedha kwa asilimia 80 ya Watanzania ambao hawatumii huduma za kifedha kupitia benki.” 

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uwezeshaji wa Wajasiriamali kutoka FSTD, Dk. Peter Kingu alisema kuwa taasisi yao imekuwa na ajenda kubwa ya kutoa suluhisho ya changamoto za huduma za kifedha nchini na zaidi kwa Watanzania ambao hawajafikiwa na huduma za kibenki kwa maeneo ya vijijini. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles