Kutoa Sh trilioni 1.3 kuboresha elimu
Na Mwandishi wetu
MKURUGENZI Mkazi wa Benki ya Dunia (WB) nchini, Bella Bird, amesema benki hiyo inakamilisha maandalizi ya kufadhili miradi inayohusu sekta ya elimu hasa elimu ya awali na sekondari nchini itakayogharimu Sh trilioni 1.357.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, Bird alisema hayo alipokutana Raisi John Magufuli, Ikulu Dar es Salaam jana.
Alisema maandalizi ya ufadhili huo yanatarajiwa kukamilika mwezi ujao.
Bird alisema miradi inayotekelezwa kwa ufadhili wa benki hiyo chini imefikia thamani ya Sh trilioni 10.186 na maendeleo ya miradi hiyo ni mazuri.
“Kwa hiyo nimekutana na Mhe. Rais Magufuli kuzungumzia maendeleo ya miradi hiyo na kwa ujumla maendeleo ni mazuri,” taarifa ya Ikulu ilimnukuu Bird akisema.
Alisema Benki ya Dunia imejipanga kuendelea kutoa mikopo nafuu kwa miradi ya maendeleo nchini kukuza uchumi na kupunguza umasikini.
Desemba 4, 2017, Bird ambaye anaiwakilisha WB Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, alikutana tena na Rais Magufuli na kueleza jinsi benki hiyo ilivyojipanga kuendelea kutoa mikopo nafuu kwa miradi ya maendeleo nchini kukuza uchumi na kupunguza umasikini.
Alibainisha maeneo ya kipaumbele kuwa ni miundombinu na hasa ya barabara na reli; kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme; Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na elimu kwa kujielekeza katika ubora na kuhakikisha idadi ya wanaopata elimu inaongezeka.
Maeneo mengine ni kuboresha sekta ya afya, kuongeza upatikanaji wa maji, usimamizi bora wa ardhi, mawasiliano, huduma za fedha jumuishi, vituo vya pamoja vya Serikali na kusaidia familia masikini.
Bird alimpongeza Rais Magufuli kwa usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Benki ya Dunia na kuahidi benki hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mingine.
“Mwaka uliopita Benki ya Dunia ilitoa mikopo nafuu yenye thamani ya dola 1.2 bilioni za Marekani (Sh trilioni 2.7).
“Fedha hizi zimekwenda katika miradi na tunafurahi kuwa inakwenda vizuri na wananchi wanafurahia.
“Kwa sasa tunapanga namna tutakavyotoa mikopo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za maendeleo katika kipindi kijacho,” alisema Bird.
Rais Magufuli alishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano na Tanzania na kumhakikishia Bird kuwa Serikali itasimamia fedha zote zinazotolewa na benki zilete matokeo yanayotarajiwa.
Alisema maeneo ambayo benki hiyo imeyataja kuwa ya kipaumbele katika fedha zitakazotolewa ni muhimu kwa ustawi wa Tanzania.
Hivi karibuni iliripotiwa kuwa WB ilizuia msaada wa Dola 50 milioni za Marekani (zaidi ya bilioni Sh112) kwa Tanzania ikitaka majadiliano zaidi kuhusu mabadiliko yanayotarajiwa kufanywa kwenye Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.
Fedha hizo zilikuwa kuisaidia Serikali kuboresha mfumo wa kukusanya, kuchakata na kutunza kumbukumbu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) lakini benki hiyo inaamini kuna vifungu vinavyokandamiza uhuru wa kujieleza.
Taarifa iliyochapishwa Oktoba Mosi na mtandao wa Eye on Global Transparency ilisema benki hiyo inasikitishwa na ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza na mwenendo wa demokrasia.
Hata hivyo, baadaye , Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James, alisema serikali haitambui kuwapo msaada wa aina hiyo.
“Serikali haijawahi kuomba wala kuwa kwenye mchakato wa kukopa Dola milioni 50 kwa ajili ya kazi za Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
“Mimi kama Katibu Mkuu nasema hatujawahi kuandika barua kuomba hizo fedha,” alisema James alipozungumza na gazeti moja la kila siku.