Asha Bani-Dar es Salaam
Benki ya Biashara Afrika (CBA) imetoa msaada wa matenki ya maji yanayofunguliwa kwa mguu katika hospitali nne jijini Dar es Salaam ikiwa ni jitihada za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.
Akikabidhi msaada huo leo Ijumaa Mei 15, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Gift Shoko amesema kuwa mchango huo ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa na CBA katika kuunga mkono jitihada za serikali kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa homa ya mapafu nchini.
“CBA imeweka nia thabiti ya kusaidia hospitali kwa kugawa vifaa vinavyohitajika kutakasa mikono kama njia muhimu ya kuzuia maambukizi.
“Mara baada ya kuona ongezeko la mahitaji ya kunawa mikono, CBA ilianza mchakato wa kuandaa matenki ya kuhifadhia maji ili kuwezesha watu kunawa mikono wanapokuwa hospitalini kwani ni moja kati ya maeneo muhimu kwa afya ya wakazi wa Dar es Salaaam,” amesema Shoko.
Aidha ameongeza kuwa hospitali zilizonufaika na msaada huo ni Amana, Sinza, Mwananyamala na Lugalo kutokana na kuhudumia watu wengi kila siku na kwamba wanatarajia kufikia hospitali nyingi zaidi katika siku zijazo.
Ili kuwasaidia wateja na Watanzania kwa ujumla kupata elimu ya virusi vya corona, Benki ya CBA inatoa elimu kupitia barua-pepe, ujumbe mfupi wa simu, mabango katika maeneo mbalimbali pamoja na mitandao ya kijamii (facebook na twitter) ili kutoa taarifa sahihi kuhusu COVID-19 na jinsi ya kulinda, kuzuia maambukizi na kuchukua hatua mbalimbali.