Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Benki ya Akiba imezindua kampeni ya kidijitali ijulikanayo kama ‘Twende Kidijitali’ ili kutoa suluhisho la changamoto za kifedha.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa leo Desemba 18,2024 inalenga kuboresha uzoefu wa wateja kupitia suluhisho la kifedha la kisasa, haraka na la kuaminika.
Kampeni hiyo inahamasisha matumizi ya huduma za kidijitali kama vile ACB Mobile, Internet Banking, VISA na Akiba Wakala.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa ACB, Dk. Danford Muyango, amesema wamejizatiti kuboresha uzoefu wa wateja wao kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Amesema kampeni hiyo ya Twende Kidijitali pia imeungwa mkono na kampeni ya msimu wa sikukuu ‘Twende Kidijitali, Tukuvushe Januari’.
“Kampeni hii ni mwendelezo wa azma ya Akiba Commercial Bank Plc kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali ya benki na kuhamasisha wateja kufurahia manufaa ya kutumia teknolojia katika kutatua mahitaji yao ya kifedha.
“Kampeni pia inalenga kusaidia wateja katika kipindi cha Januari ambacho mara nyingi kinakuwa kigumu kifedha,” amesema Dk. Muyango.
Ametaja vigezo vya kushiriki kampeni hiyo kuwa ni idadi na thamani ya miamala ya kidijitali ambapo wateja watapimwa kulingana na idadi na thamani ya miamala yao kupitia huduma za kidijitali.
Pia amesema wateja walio na ushiriki mkubwa watakuwa na nafasi ya kushinda zawadi za fedha taslimu.
Sharti jingine ni uzoefu wa kidijitali na maoni ya wateja ambapo watakaoshiriki kwa kutoa maoni ya thamani kuhusu huduma za kidijitali watapata nafasi ya kushinda katika droo ndogo.
Aidha amesema wateja watakaowaalika wateja wengine kufanya miamala kwa njia ya ATM, POS, Wakala, Mobile Banking au Internet Banking watajishindia zawadi.
“Benki ya Akiba inawakaribisha wateja wote kushiriki nasi katika safari hii ya kidijitali, watembelee matawi yetu au kuangalia majukwaa yetu ya kidijitali,” amesema.