27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Bendera za Chadema zasitisha mazishi ya polisi

img_7211Na PENDO FUNDISHA, MEBYA

JESHI la Polisi, Mkoa wa Mbeya, jana lilisitisha kwa muda mazishi ya aliyekuwa askari polisi, kitengo cha usalama barabarani mkoani Arusha, Allen Mwakasita, baada ya kuona bendera za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika msafara wa mazishi ya askari huyo.

Bendera hizo zilikuwa zimefungwa kwenye magari yaliyokuwa kwenye msafara wa kwenda katika mazishi yaliyotarajiwa kufanyika katika Kijiji cha Izumbwe, Kata ya Igale, Wilaya ya Mbeya.

Kabla polisi hawajachukua uamuzi huo, awali walionesha kutoridhishwa na baadhi ya viongozi na wafuasi wa  Chadema, kuingilia taratibu za polisi kwa kupeperusha bendera za chama hicho wakati marehemu hakuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Polisi, Wilaya ya Mbeya (OCD), James Chacha, aliwataka wafuasi hao wa Chadema kushusha bendera zao kwa kuwa hazikutakiwa mahali hapo.

“Tunawaombeni ndugu zetu, mtusikilize, marehemu Allen hakuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa na sisi kama jeshi tunataratibu zetu.

“Kwa hiyo, kama mtahitaji kuongozana na msafara huu, tutawaomba mshushe bendera zenu za chama mlizozifunga katika magari yenu,”alisema Chacha.

Baada ya agizo hilo, baadhi ya wafuasi wa Chadema na viongozi wao, walipaza sauti za kumpinga mkuu huyo wa polisi kwa kile walichosema wana haki ya kupeperusha bendera hizo katika mazishi hayo.

“Marehemu Allen anatoka katika familia ambayo wazazi wake ni wanachama waandamizi wa Chadema. Baba yake ni mzee wa baraza la wazee na mama yake ni diwani wa viti maalum Chadema.

“Kwa hiyo, ni lazima tupeperushe bendera hata kama hamtaki kwa sababu tunamuenzi kijana wetu,” alisikika muombolezaji mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Aron Mwakilindi.

Baada ya kutokea hali ya kutoelewana, baadhi ya viongozi wa Chadema walilazimika kufanya kikao na viongozi wa polisi ili kuangalia namna ya kutatua mvutano huo.

Mazungumzo hayo yalipomalizika baada ya saa tatu, viongozi wa chama hicho walikubali marehemu Allen azikwe bila bendera za chama na badala yakwe azikwe kijeshi kama ilivyokuwa imepangwa.

Akizungumza baada ya makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Mbeya, Joseph Mwachembe, aliwataka wafuasi wa chama hicho wawe watulivu ili mazishi hayo yafanyike kwa amani.

“Tumezungumza na kufikia muafaka, kwamba chama kitaliachia Jeshi la Polisi lifanye kazi yake ya maziko na baada ya hapo, chama kitaendelea na taratibu zake.

“Katika msafara wa kwenda kwenye mazishi, magari yenye bendera yawe umbali wa mita 300 kutoka katika msafara wa magari ya polisi,”alisema Mwachembe.

Naye baba mzazi wa marehemu Allen, Daniel Mwakasita, alilishukuru Jeshi la Polisi kwa jinsi lilivyoshiriki mazishi ya mtoto wake huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles