BENAZIR BHUTTO: WAZIRI MKUU WA PAKISTAN ALIYEPITIA MISUKOSUKO

0
652

Na Leah H. Mwainyekule

OKTOBA 9, 2012 huko Mingora, Pakistan gari lililokuwa limejaa wanafunzi wa kike lilisimamishwa.  Mmoja wa wapiganaji wa Taliban aikuwa akimtafuta binti mmoja na alipomtambua, alimwambia kwamba analazimika kummaliza, kwani amemlazimisha kufanya hivyo.  Alilenga bunduki yake kwenye kuelekea kichwa cha yule binti na kufyatua risasi.

Malala Yousafzai alikuwa na umri wa miaka 15 tu alipopigwa risasi kutokana na kuwaudhi Taliban kwa kupiga kampeni kuzungumzia umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.  Taliban walilichukua hilo kama tusi kubwa linalopingana na imani yao na utamaduni wao.

Malala kwa sasa yu mzima kabisa, akitarajia kujiunga na chuo kikuu nchini Uingereza hivi karibuni baada ya kuhamia huko tangu alipopigwa risasi.  Ni mwandishi wa vitabu na pia ni mshindi wa tuzo ya Nobel kwa mwaka 2014, tuzo aliyoshinda pamoja na Kailash Satyarthi, kutokana na juhudi za wawili hao kupigana dhidi ya unyanyasaji wa watoto na vijana, pamoja na kupigania haki ya elimu kwa watoto wote.  Lakini zaidi ya yote, Malala ana ndoto za kuwa Waziri Mkuu wa Pakistan na ndoto hii inatokana na mtu anayemthamini kuliko wote duniani: Benazir Bhutto.

Benazir Bhutto ni mwanamama anayetazamwa na mabinti wengi sana duniani kwa jicho la kipekee, hasa katika nchi zinazominya kidogo haki ya watoto wa kike na haki za wanawake wenyewe.  Mabinti kama Malala wanamuona Bhutto kama shujaa wao, na licha ya kashkash zote ambazo mwanamama huyo amepitia tangu alipoingia kwenye ulingo wa siasa, bado mabinti wengi wanataka kuwa yeye.

Desemba mwaka huu itakuwa miaka 10 tangu Bhutto alipouwawa.  Jina la Bhutto kamwe haliwezi kufutika, si tu kwa mabinti wanaoisaka elimu kwa nguvu, bali na wanawake wengi sana duniani wanaowania uongozi katika dunia ambayo bado haikubali sana mwanamke kuongoza nchi.  Historia ni kithibitisho kwamba Bhutto atabaki kuwa mwanamke wa kipekee sana.

Benazir Bhutto alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke nchini Pakistan kuanzia mwaka 1988 hadi 1990 na katika kipindi kingine cha mwaka 1993 hadi 1996.  Alizaliwa mjini Karachi katika familia ya wanasiasa, kwani baba yake, Zulfikar Ali Bhutto, alianzisha chama cha siasa cha Pakistan People’s Party (PPP) na kuwa Waziri Mkuu wa Pakistan mwaka 1973.

Zulfikar mwenyewe naye alijifunza siasa kutoka kwa baba yake, Shah Nawaz Bhutto, mwanasiasa maarufu sana ambaye miaka ya nyuma aliwahi kuwa Waziri Mkuu katika Jimbo la Junaqadh.  Akiwa mtoto wa kwanza kuzaliwa kwenye familia yao, Benazir Bhutto alimpenda sana na kumheshimu baba yake na hivyo haikuwa ajabu kwamba alifuata  nyayo zake za siasa.  Mapenzi hayo kwa baba yake pengine yalitokana na ukweli kwamba licha ya kuwa katika nchi ya Kiislam ambayo haikuthamini elimu kwa mtoto wa kike, baba huyo alimsisitizia mwanaye umuhimu wa elimu na haikuwa ajabu kwa mwanamama huyo kusoma katika vyuo vikuu viwili vinavyoongoza kwa ubora dunia: Harvard na Oxford.

Misukosuko ya kisiasa kwa Bhutto ilianza mwaka 1977 baada ya baba yake kuondolewa madarakani katika Mapinduzi ya Kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Muhammad Zia-ul-Haq. Zia aliamua kutangaza Pakistan kuwa chini ya sheria za kijeshi, na Zulfikar alikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji ya Muhammad Ahmed Khan Kauri.  Wakati wadogo zake wa kiume waliamua kwenda nje ya nchi kutafuta watetezi wa baba yao, Benazir Bhutto na mama yake waliamua kubaki Pakistan na kujikuta wakikamatwa mara nyingine na kuwekwa kizuizini kwa vipindi vifupi.

Zulfikar alipatikana na hatia na kuhukumiwa kuuawa, adhabu iliyotekelezwa Aprili mwaka 1979.  Baada tu ya hapo, Bhutto na mama yake walikamatwa na kufungwa kwa miezi sita, kabla ya kutolewa na kupewa kifungo cha nyumbani kwa miezi sita mingine.  Waliachiwa huru kabisa Aprili ya mwaka 1980.

Wakati Bhutto na mama yake wakiteuliwa kuwa wenyeviti wenza wa chama cha PPP, kaka zake – Murtaza na Shahnawaz – waliunda kikundi cha Al Zulfikar ambacho kiliwafundisha wanachama wake namna ya kufanya mauaji kwa ajili ya kuuondoa utawala wa kijeshi.

Baada ya kikundi cha Al Zulfikar kupanga utekaji wa ndege ya Shirika la Ndege la Kimataifa la Pakistan mwaka 1981, Serikali ilitumia kisingizio hicho kwa ajili ya kuwakamata tena Bhutto na mama yake.  Baada ya miezi minne mama yake aliachiwa kutokana na matatizo ya kiafya, lakini licha ya Bhutto mwenyewe kutohusika na utekaji ule, alihamishiwa gereza la Sukkur na kurejeshwa tena Karachi baada ya muda.  Muda mwingi wa kifungo chake hicho aliutumia katika eneo lenye ulinzi mkali mbali na wafungwa wengine.

Zia alipotembelea Marekani Desemba ya mwaka 1982, Serikali ya nchi hiyo ilizungumzia suala la kifungo cha Bhutto, na jumuiya ya kimataifa ikaendelea kumsonga. Hatimaye Serikali ya Pakistan ilikubali kumuachia Bhutto huru na Januari ya mwaka 1984 aliachiwa na kupakiwa kwenye ndege iliyoelekea Geneva na kisha nchini Uingereza.

Julai ya 1985, kaka yake Bhutto, Shhnawaza, alikufa katika mazingira ya kutatanisha nchi Ufaransa.  Bhutto aliamini kwamba Zia anahusika katika mauaji ya kaka yake na Serikali ya Pakistan ilimruhusu kuuleta mwili wa kaka yake nchini Pakistan ili uzikwe kwenye makaburi ya familia yao.  Hata hivyo baada tu ya mazishi, Bhuto alikamatwa na kupewa kifungo cha nyumbani kwa takribani miezi mitatu.  Baada ya kuchiwa huru, alirejea katika maisha yake nchini Uingereza.

Pamoja na misukosuko yote aliyoipitia, Bhutto aliamua kurejea nchini mwake baada ya Pakistan kuondoa sheria za kijeshi.  Alipofika uwanja wa ndege alilakiwa na umati mkubwa wa watu na baada ya hapo alipokwenda kuzungumza katika uwanja wa Iqbal Park, takribani watu milioni mbili walifika kumsikiliza akitema cheche dhidi ya utawala wa Zia. Mwezi Agosti mwaka huo wa 1986 alikamatwa tena na kushikiliwa kwa wiki chache.

Wakati huo huo, Bhutto alikubali kuolewa na mwanaume ambaye mama yake alimchagulia.  Ndoa kati ya Bhutto na Asif Ali Zardari ilifungwa mjini Karachi Desemba 1987 na ilikuwa na lengo mahususi la kumfanya Bhutto akubalike zaidi katika jamii kutokana na kuwa katika ndoa.

Muda mfupi baada ya ndoa Bhutto alipata ujauzito, na Mei 1988 Zia alivunja Bunge na kuitisha uchaguzi  kufanyika Novemba mwaka huo, akijua fika kwamba mpinzani wake mkuu atakuwa akijifungua kipindi hicho na hivyo asingeweza kupata muda wa kufanya kampeni na kushinda uchaguzi. Zia pia alipiga marufuku vyama kufanya kampeni na badala yake kuamuru wagombea wasimame wenyewe na kujifanyia kampeni binafsi, jambo ambalo lingekuwa gumu kwa Bhutto kwa wakati huo.

Hata hivyo, Zia alikufa ghafla Agosti mwaka huo baada ya ndege aliyokuwa amepanda kuanguka.  Vile vile, mahakama kuu ilifuta amri ya Zia juu ya wagombea kusimama kama watu binafsi na badala yake kukubaliana na uwakilishi wa vyama.  Hilo lilisaidia Bhutto kuwa mgombea kupitia chama chake.

Kutokana na Pakistan kuwa nchi iliyoshikilia sana imani ya Kiislam, wengi walizungumzia kutokubaliana na suala la mwanamke kuwa kiongozi, hasa mwanamke mwenyewe ambaye hakufuata sana maadili ya Kiislamu.  Wafuasi wa Zia na wengine wenye msimamo mkali waliungana na kuunda chama cha Islami Jamhoori Ittehad (IJI), huku wakisaidiwa na Usalama wa Taifa wa nchi hiyo ambao ulijaribu kuiba kura ili kumnyang’anya Bhutto ushindi.

Licha ya vikwazo vyote hivyo, chama cha Bhutto kilishinda viti 93 kati ya 205, huku IJI kikipata viti 54.  Wiki mbili baadaye Rais Ghulam Ishaq Khan aliamua kumwalika Bhutto kuunda Serikali kwa shingo upande.  Bhutto aliapishwa kuwa Waziri Mkuu wa Pakistan Desemba 1988 na kuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke nchini Pakistan, Waziri wa kwanza mwanamke katika nchi yenye imani kali ya Kiislam, mwanamke wa nne kuwa Waziri Mkuu duniani na Waziri Mkuu mwenye umri mdogo zaidi duniani.

Kuapishwa kwa Bhutto kuwa Waziri Mkuu kulipokelewa kwa shangwe kubwa na watu wengine, hasa wanawake ambao waliona ameonyesha njia ya uhuru wa siasa za vyama vingi, pamoja na kukua kwa haki za wanawake.

Hata hivyo, licha ya kuwa kiongozi wa Serikali na kuahidi mwanga mpya wa tumaini kwa wengi, wapo wengine wenye nguvu zaidi ambao hawakumtaka.  Watu watatu muhimu katika nchi hiyo: Mkuu wa Jeshi, Aslam Beg, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Hamid Gul, pmoja na Rais Khan, wote walikuwa wakipingana na familia ya kina Bhutto, pamoja na suala la mwanamke kuwa Waziri Mkuu.  Upinzani wa watu hao watatu ulikuwa wa wazi kiasi kwamba ilikuwa ngumu kwa Bhutto kufanya kazi zake kama Waziri Mkuu.

Bhutto alishindwa hata kupitisha miswada mbalimbali mbayo ilihitaji sahihi ya Rais, kutokana na Rais huyo kumpiga vita na kutoitia sahihi.  Hata hivyo, alifanikiwa kuwaachia huru wafungwa wengi wa kisiasa waliokuwa wamewekwa kizuizini chini ya utawala wa Zia.

Msuguano kati ya Bhutto na Rais ulishamiri mwaka 1990 na kutokana na Rais Khan kupiga kura ya turufu hii ya sera nyingi za Bhutto na migogoro kuibuka nchini Pakistan, Bhutto alituhumiwa kwa kutoweza kutawala.  Hali kadhalika, mume wa Bhutto naye aliingia katika kashfa ya rushwa, ikidaiwa kwamba alikuwa akiomba ‘kitu kidogo’  kwa wafanyabiashara mblimbali ili mambo yao yaende vizuri.  Jina maarufu la mume huyo hadi leo hii ni “Mr. Ten Percent”.

Kutokana na hayo na pia tuhuma kwamba Bhutto alikuwa akimruhusu mumewe kuhudhuria baadhi ya mikutano ya Baraza la Mawaziri ilhali yeye si Waziri, Agosti ya mwaka 1990 Rais Khan alitumia nguvu yake ya kikatiba na kuufuta uongozi wa Bhutto.

Hata hivyo, umaarufu wa Bhutto haukuweza kufutika.  Mwaka 1993 uliitishwa uchaguzi na chama chake kilishinda viti vingi zaidi na hivyo Oktoba 19 mwaka huo Benazir Bhutto aliapishwa kuwa Waziri Mkuu kwa kipindi kingine. Katika kipindi chake hicho cha pili, Bhutto aliwateua Mama yake pamoja na mumewe kuwa mawaziri.  Baadaye alilazimika kuondoka nchini Pakistan na kwenda kuishi uhamishoni nchini Dubai.

Pervez Musharraf alikuwa kiongozi wa Pakistan kipindi chote hicho, lakini umaarufu wake ulizidi kupungua miongoni mwa watu na matukio ya mabomu ya kujitoa mhanga yalizidi. Marekani ilikuwa ikimhitaji Musharraf kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugaidi hivyo ilitaka aendelee kubaki madarakani, lakini vile vile iliona umuhimu wa Bhutto kurejea nchini Pakistan kusaidiana na Musharraf, kutokana na umaarufu aliokuwa nao.

Bhutto alirejea nchini Pakistan Oktoba 2007 na Musharraf hakupendezwa na kitendo cha mwanamama huyo kurejea kabla ya uchaguzi, kwani angeweza kirahisi sana kuwa Waziri Mkuu kwa mara nyingine katika uchaguzi wa mwaka 2008.  Musharraf alimuonya Bhutto kwamba Pakistan siyo salama na anaweza akauawa na adui zake ambao walikuwa wakiongezeka kila siku na kutishia hata usalama wake yeye Musharraf.

Haya hivyo, Bhutto aliomba Uingereza na Marekani kuchukua jukumu la kuhakikisha usalama wake, lakini nchi hizo mbili zilikataa.  Badala yake, kikosi cha usalama wa Bhutto kiliandaliwa na Musharraf mwenyewe.

Jaribio la mauaji liifanyika dhidi ya Bhutto wakati msafara wae ukipita katikati ya umati wa watu mjini Karachi. Watu 149 waliuawa na 402 kujeruhiwa baada ya mabomu mawili kulipuliwa, lakini Bhutto hakudhurika. Bhutto mwenyewe alidai anawafahamu waliohusika na jaribo la kumuua na alimuandikia Musharraf majina ya washukiwa na kuomba Scotland Yard ya Uingreza na FBI ya Marekani kuitwa kufanya uchaguzi, lakini Musharraf alikataa kuvihusisha vyombo hivyo.

Asubuhi ya Desemba 27, 2007, Bhutto alikutana na Rais wa Afghanistan, Hamid Karzai.  Mchana ule alitoa hotuba kwa wafuasi wa chama chake cha PPP na wakati akiondoka katika eno hilo, aliamua kusimama juu ya gari na kupungia mkono umati wa watu uliokuwapo.  Mita tatu tu kutoa kwenye gari lake, mwanaume mmoja alimpiga risasi tatu na pia kujilipua bomu la kujitoa muhanga.  Bhutto alikimbizwa hospitali, lakini akatangazwa kuwa amefariki dunia na kesho yake alizikwa karibu na kaburi la baba yake kwenye makaburi ya familia yao.

Hivyo ndivyo historia ya Benazir Bhutto inavyoishia.  Wengi walimlilia duniani kote, hasa kutokana na ujasiri wake wa kuweza kupenya makali mengi hadi kufanikiwa kuwa Waziri Mkuu katika nchi kama Pakistan.  Licha ya Pakistan kutuhumiwa kwamba haiheshimu haki za binadamu na usawa wa kijinsia, bado nchi hiyo inaweza kutamba kuwa mbele zaidi ya nchi kama Marekani ambayo haijawahi hata kuwa na Rais mwanamke, wakati Pakistan, licha ya misimamo yao mikali, walikuwa na Benazir Bhutto.

Ndio maana si ajabu kwa nchi hiyo kutoa wanawake wengine jasiri, mfano mzuri sana ukiwa wa Malala Yousafzai.  Licha ya kuona misukosuko aliyopitia Bhutto na licha ya yeye mwenyewe kupitia shida, bado anataka kuwa Waziri Mkuu wa nchi yake, akiamini kwamba anaweza kuongoza na kuibadilisha ikawa bora zaidi na mahala salama kwa kuishi kwa watu wa jinsia zote na itikadi zote.

Hivyo ndivyo nyota ya Benazir Bhutto inavyoendelea kuishi.  Ujasiri wake haufananishwi na mtu yeyote hapa duniani na hiyo ndiyo sababu atabaki kuwa nyota mioyoni mwa wengi.  Kifo chake kimezaa kina Bhutto wengi zaidi wa kuweza kuibadilisha dunia kuwa mahala pema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here