BEN POL KWA HILI AISEE BIG NO!

0
649

Na CHRISTOPHER MSEKENA

SANAA ina wigo mpana kiasi kwamba msanii anapoitekeleza anaweza kuishangaza jamii na wakati mwingine anaweza kuonekana amekiuka mila na tamaduni za jamii husika.

Mbongo Fleva anayefanya poa kwenye RnB Bongo, Benard Paulo ‘Ben Pol’ wiki hii ametikisa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii baada ya kusambaa kwa picha zake mbili zenye utata.

Katika picha hizo, moja anaonakena amefungwa kitambaa chekundu usoni akiwa hana shati. Ni kama ametekwa.

Nyingine anaonekana akiwa amekaa kwenye kiti cha mbao, akiwa amefungwa mikono yake kwa kamba za katani, lakini akiwa hana nguo yoyote mwilini mwake. Nitazungumzia picha hii ya pili.

Kwa maelezo yake mwenyewe, Ben anasema picha hiyo ameiachia kwa makusudi kwa leo la kutafuta tention kwa mashabiki wake kwa ajili ya project yake mpya ‘Tatu’.

Siyo dhambi msanii kutumia ulingo wa sanaa kuonyesha ujuzi wake, ni sawa kabisa mwanasanaa kutumia upana wa sanaa kujiongezea thamani  katika aina ya sanaa anayofanya lakini hili la Ben Pol iliwaacha njia panda wengi hasa ukizingatia mwimbaji huyo hana utaratibu wa kutumia kiki anapotaka kuachia kazi zake.

Ben Pol ni aina ya wasanii wasiohitaji kiki kwenye kazi zao, hana historia hiyo pia amekuwa mstari wa mbele kuonyesha vitu vipya vya kisanaa katika majukwaa mbalimbali pale anapotumbuiza.

Utakuwa shahidi endapo utatazama maonyesho ya Tamasha la Fiesta aliyofanya mwaka jana. Kila mji aliotumbuiza aliibuka kuwa ‘Man of the show’ kwa kupiga shoo maridadi zenye ubunifu mkubwa uliochanganyika na uafrika, jambo ambalo ni adimu  kwa wasanii wa kizazi hiki.

Kuna aina ya mavazi aliyoyatinga yaliyoonyesha utofauti wake. Mfano shoo ya Dodoma alipendeza kwa mavazi ya kichifu kama ilivyokuwa kwa wakuu wa jamii nyingi za Kiafrika na hata jijini Mwanza hakusita kuongeza ubunifu na kuvaa vazi linalofanana na vazi la kike (sketi).

Vazi lile halikuwa geni. Halikuwashangaza wengi maana wasanii wengi maarufu wa ndani na nje ya nchi walipata kuvaa kabla yake.

Ni mtindo mpya kwenye ulimwengu wa fasheni ingawa katika jamii yetu hutafsiriwa tofauti hasa vazi hilo linapovaliwa na jinsia ya kiume.

Vazi lile limewahi kuvaliwa na mkongwe wa muziki wa dansi kutoka Kongo, Koffi Olomide katika maonyesho yake na hata kwenye video ya wimbo wake uliobamba ‘Selfie’ kipindi cha nyuma.

Tukirudi Bongo mwaka 2013 katika sherehe za tuzo za KTMA, msanii Diamond Platnumz alitupia vazi hilo na likazua gumzo kubwa lakini wataalamu wa mavazi wakatolea ufafanuzi.

Ukiondoa wote hao, mbabe mwingine kwenye Bongo Fleva, Ali Kiba wiki iliyopita alitikisa ulimwengu wa muziki Afrika pale alipopanda jukwaani akiwa na mwonekano wa mwili uliochorwa kiafrika huku vazi lililomsitiri likiwa ni sketi.

Ali Kiba katika onyesho lile la ‘Lip Battle Africa’ aliimba wimbo wa marehemu Brenda Fassie na kushangiliwa na mashabiki kwa kuwa aliitumia sanaa yake kujenga uhalisia uliofanya watu wenye mapenzi na kazi za gwiji huyo wapige kelele za shangwe.

Kwa hili la sasa, Ben Pol ameteleza. Si utamaduni wetu kabisa. Amepita njia ileile aliyopitia Linna Sanga kwa kupiga picha akionyesha ujauzito wake huku nguo akiwa amevaa nguo ambazo hazijamsitiri vyema.

Alichofanya Ben siyo sahihi, hata Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) wamelaani kitendo hicho. Hapo Ben amevuka mipaka ya sanaa na kuvunja kuta za mila, desturi na tamaduni za Kitanzania.

Dhumuni la Ben Pol lilikuwa ni kuonyesha uhalisia wa mtu aliyetekwa ambaye amenyimwa uhuru na kukosa faragha yake.

Ni vizuri ila kwa jamii yetu si sawa ndiyo maana imeleta shida kiasi kwamba ametaka kuiharibu heshima yake aliyoijenga kwa muda mrefu.

Uhuru wa kufikiri na kufikisha ujumbe kwa hadhira usitumike vibaya kiasi cha kutia doa sanaa. Bado kulikuwa na njia nyingi za kufikisha ujumbe lakini si kwa picha ile!

Hata hivyo, picha ileile kama angevaa angalau kaptura tu, ingeondoa ukakasi wote ule. Pia ile picha nyingine aliyojifunga kitambaa chekundu usoni ingeweza kufikisha ujumbe bila kuharibu hali ya hewa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here