BEKI EVERTON BADO AIOTA ALBINO UNITED

0
647

NA MWANDISHI WETU


BEKI wa kati aliyejiunga na timu ya soka ya Everton inayoshiriki Ligi Kuu England akitokea Burnley, Michael Keane, ameikumbuka timu ya Albino United waliyoitembelea wakifanya mazoezi chini ya kocha wao Alex Kashasha wakati wa ziara yao hapa nchini.

Everton iliweka historia ya kuwa timu ya kwanza inayoshiriki Ligi Kuu England kutua Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla kucheza mchezo wake wa kwanza wa kimataifa wa kirafiki kuelekea msimu mpya wa ligi yao.

Safari hiyo ambayo iliwezeshwa na kampuni ya SportPesa ambao ni wadhamini wao ilishuhudia wakicheza na Gor Mahia ya Kenya katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Keane ambaye kipaji chake kilikuzwa katika kituo cha Manchester United alisema amekuwa akisikia watu wenye ulemavu wa ngozi wanapitia hali ngumu sana hivyo basi wao kuja pamoja na kufurahia nao ilikua jambo zuri.

“Ni vigumu kuona timu kama ya Albino United kwetu Uingereza kwasababu wanachukuliwa kama watu wasiokuwa na mchango kwenye jamii hivyo kuona watu wanapata shida sio jambo rahisi hata kidogo ila tumefarijika na timu tuliyoiona Tanzania na tunawahimiza wacheze kwa bidii na kuendelee kufurahia katika kile wanachokifanya,” alisema.

Kwa upande wake, kiungo wa Everton, Tom Davies, ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya England chini ya miaka 19 alisema ni mara yake ya kwanza kukutana na timu ya mpira wa miguu iliyoundwa na watu wenye ulemavu ili kufikisha ujumbe kwa jamii.

“Hii ni mara yangu ya kwanza kuona timu kama hii lakini nimeona umoja kati yao na inaleta picha nzuri ukiwa hapa. Wote ni marafiki na nina Imani kocha ataweza kuwasaidia sana, kwa kweli nina furaha sana kuwepo hapa,” alisema.

Davies alisema licha ya mpira wa miguu kuwa mchezo unaoleta watu pamoja, anawashauri Albino United kuendelea kufurahia kucheza pamoja.

“Ni vizuri kuona timu inavyocheza na kufurahia wanachokifanya na hiyo ndio maana halisi ya soka na michezo kwa ujumla ya kuwaleta watu pamoja,” alisema.

Mbali na kufanya nao mazoezi, wachezaji hao waliongoza zoezi la kugawa zawadi kama vile shin guards, mipira, jezi, kamba za kuruka, pampu za kujazia mipira pamoja na vifaa vingine vingi vya kimichezo kwa wachezaji wa Albino United.

Everton walikuja nchini na ujumbe wao wa Together Inspired ‘Kwa pamoja tumehamasika’ ukiwa ni ujumbe uliyoambatana na kampeni ya uzinduzi wa jezi yao mpya ya ugenini ambayo waliitumia kwa mara ya kwanza kwenye mchezo dhidi ya Gor Mahia katika ardhi ya Tanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here