30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Bei ya umeme yashuka

Pg 3Jonas Mushi na Adam Mkwepu, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kushusha bei ya nishati ya umeme kwa watumiaji wakubwa wa majumbani wanaotumia zaidi ya uniti 75 kwa mwezi pamoja na viwanda vikubwa na vya kati.
Tangazo la kushushwa kwa bei ya nishati ya umeme limetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felex Ngamlagosi, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyikia jana ofisini kwake, Dar es Salaam.
Alisema punguzo hilo limezingatia gharama za watumiaji wadogo ni ndogo na wanachangiwa na watumiaji wakubwa wa majumbani wanaotumia zaidi ya uniti 75 kwa mwezi, hivyo kuondoa ulazima wa kuguswa na mabadiliko hayo.
Kwamba kwa msingi huo, wanatakaoguswa na punguzo hilo ni wateja wa viwanda vikubwa na vya kati na watumiaji wakubwa wa majumbani ambao sasa watapata punguzo la jumla ya wastani wa asilimia 2.21.
Ngamlagosi alisema kwa wastani huo, bei ya umeme kwa watumiaji hao wakubwa na wa viwandani inashuka kutoka Sh 257.39 kwa uniti hadi Sh 251.70, ambayo ni sawa na punguzo la Sh 5.69 kwa kila uniti.
“Kwa wateja wa majumbani wenye matumizi ya chini ya wastani wa uniti 75 kwa mwezi, bei ya umeme haitabadilika kwa sababu kundi hili bei yake ni ya chini na gharama zake kuchangiwa na kundi la wateja wakubwa wa majumbani,” alisema Ngamlagosi.
Akifafanua jinsi punguzo hilo lilivyogusa makundi tofauti ya watumiaji wa nishati hiyo, alisema kwa wateja wakubwa wa majumbani wanaotumia zaidi ya uniti 75 na ambao hapo awali walikuwa wakilipa Sh 306 kwa uniti, sasa watalipa Sh 298 ambayo ni sawa na punguzo la shilingi nane.
Kwa wale wanaotumia volti 400, bei ya umeme itashuka kutoka Sh 205 kwa uniti hadi Sh 200 kwa uniti ambayo ni punguzo la shilingi tano kwa uniti, huku wateja wanaounganishwa katika msongo wa kati wa umeme, bei itashuka kutoka Sh 163 kwa uniti hadi Sh 159 kwa uniti, ikiwa ni punguzo la shilingi nne kwa uniti.
Aliwataja wateja wengine kuwa ni wale waliounganishwa katika msongo mkubwa wa umeme ambao nao bei ya umeme itashuka kutoka Sh 159 kwa uniti hadi Sh 156, sawa na punguzo la shilingi tatu.
Ngamlagosi alizitaja sababu za kushuka kwa bei ya umeme kuwa ni pamoja na kushuka kwa gharama za uzalishaji wa nishati hiyo kulikosababishwa na mabadiliko ya bei ya mafuta, thamani ya shilingi na mfumuko wa bei kwa mwaka 2014.
“Bei ya umeme inatakiwa kurekebishwa kila baada ya miezi mitatu kutokana na mabadiliko ya bei ya mafuta, thamani ya shilingi ya Tanzania na mfumuko wa bei ambapo mabadiliko hayo yanahusu bei ya kununua uniti ya umeme na si tozo za mwezi za utoaji huduma,” alisema.
Akizungumzia bei ya mafuta mazito (Heavy Fuel Oil – HFO na Industrial Diesel Oil-IDO), alisema kwa Januari hadi Julai, bei ya IDO iliongezeka kutoka Sh 2,273.74 hadi 2,312.94, ambayo ni sawa na asilimia 35 na kutoka Agosti hadi Desemba bei ilishuka hadi kufikia Sh 2,099.18.
Kwa upande wa HFO, alisema bei iliongezeka hadi kufika Sh 2,210.43 kwa lita Mei na kati ya Juni hadi Desemba ilishuka hadi kufikia Sh 1,444.33.
Alisema mwaka jana ilikadiriwa TANESCO wangezalisha na kununua umeme wa zaidi ya uniti trilioni tano kutoka katika vyanzo vya mitambo ya mafuta na gesi asilia, hata hivyo, uniti zilizozalishwa na TANESCO pamoja na zile zilizonunuliwa kutoka kwa kampuni binafsi zilifikia zaidi ya trilioni tatu, sawa na punguzo la asilimia 29, ikilinganishwa na makadirio.
“Mabadiliko hayo ya bei za mafuta na uzalishaji yanamaanisha mahitaji ya pato la TANESCO yanapungua kwa Sh bilioni 57,” alisema Ngamlagosi.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles