26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Bei ya Umeme kutoka miradi midogo sasa ni Sh 1,600

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Nishati, January Makamba, amesema kuwa, Sh 1,600 itakuwa bei mpya ya umeme kwa unit katika miradi midogo ya umeme iliyo nje ya Gridi ambayo itaanza kutumika Agosti 1, 2022 ili kufanya wananchi kupata umeme wa uhakika na wawekezaji binafsi kuweza kujiendesha na kuwekeza zaidi.

Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza na Muhonja Antony ambaye anafanya kazi za uchomeleaji katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe. Waziri wa Nishati alifika kisiwani humo ili kukagua hali ya upatikanaji umeme unaozalishwa kwa kutumia mitambo ya umeme Jua.

Makamba ameyasema hayoleo Julai 12, 2022 akiwa katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza wakati alipofika kisiwani humo kutatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji umeme wa uhakika.

Maamuzi hayo ya Serikali yamekuja baada ya wawekezaji binafsi wa miradi midogo ya umeme kutakiwa kuuza bei ya umeme kwa Sh 100 kwa unit gharama ambayo iliwapa changamoto za kiuendeshaji na hivyo kushindwa kuwapa wananchi huduma ya umeme ya uhakika.

Akiwa kisiwani Ukara, Makamba alielezwa na wananchi wa kisiwa hicho kuwa, awali walikuwa wakilipa Sh 3,500 kwa unit na  walikuwa wakipata umeme kwa masaa 24 kwa siku lakini baada ya kutangazwa kwa bei ya umeme ya Sh 100, kampuni ya JUMEME inayotoa huduma ya umeme kisiwani humo ilianza kuwapa umeme kwa masaa Sita tu kwa siku na pia kutakiwa kununua umeme kwa tokeni.

Akitoa ufafanuzi kwa wananchi kuhusu upangaji wa bei za nishati, alieleza kuwa unapaswa kuhusisha pande zote mbili ambazo ni Mwekezaji na Serikali hivyo, zoezi la upatikanaji wa bei mpya ya umeme limekuwa la uwazi na kwamba gharama mpya iliyotajwa  haipo juu kama awali ili kutowaumiza wananchi na pia haitakuwa Sh 100 ili kampuni binafsi nazo ziwe na uwezo kufanya shughuli zake kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Baadhi ya Wanawake katika Kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe wakifurahi na Waziri wa Nishati, January Makamba baada ya kutatua changamoto ya upatikanaji umeme kisiwani humo na pia kwa kutoa mitungi 167 ya gesi itakayowafanya wanawake hao kutumia nishati safi na kuondokana na hatari ya kupata magonjwa katika mfumo wa hewa.

Ameeleza kuwa Sera ya Nishati imetamka wazi kuhusu bei ya nishati inayopangwa na Serikali ikiwemo umeme, gesi na mafuta, kuwa lazima iendane na gharama za kuzalisha nishati husika.

Pamoja na kutangaza bei hiyo mpya, Waziri wa Nishati amezitaka kampuni husika kuhakikisha kuwa wanatoa umeme wa uhakika, wawasilishe mpango wa Biashara serikalini pamoja na kuwa na mkataba wa huduma kwa mteja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya JUMEME, Aida Kiangi aliahidi mbele ya wananchi wa Ukara kuwa kuanzia Agosti 1, 2022 umeme kisiwani humo utatolewa kwa masaa 24.

Nguzo za umeme zilizobeba nyaya ambazo zimesimikwa chini ya ziwa Victoria ili kupeleka umeme wa kiasi cha megawati 10 kwenye kisiwa cha Ukerewe kutokea Bunda –Mara.

Katika hatua nyingine, Waziri Makamba ameendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kugawa mitungi ya gesi 167 ambayo itasambazwa kwa Shule za Serikali za Msingi na Sekondari kisiwani Ukara pamoja na walimu wa shule hizo ili wawahamasishe wananchi wengine kutumia nishati safi.

Awali, Waziri wa Nishati alikagua vituo vidogo vya mafuta wilayani Bunda, Mkoa wa Mara katika Kijiji cha Guta B na Kibara ikiwa ni mkakati wake wa kupeleka vituo vya mafuta hadi vijijini ili wananchi wapate Nishati safi na katika mazingira salama ambapo katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imetenga Sh Bilioni 2 ili kutoa mikopo kwa wananchi wanaotaka kuwekeza katika ujenzi wa vituo hivyo vijijini.

Waziri wa Nishati, January Makamba (kulia) akizungumza na mwananchi katika Kijiji cha Kibara wilayani Bunda baada ya kuona jinsi vituo vidogo vya mafuta vijijini vinavyofanya kazi na kuwaeleza wananchi kuhusu fedha zilizotengwa na Serikali takriban Sh bilioni 10 ili kuwakopesha wananchi wanaotaka kuwekeza kwenye vituo vidogo vya mafuta vijijini.

Akiwa safarini kuelekea wilayani Ukerewe Waziri Makamba alikagua nyaya za umeme zinazopita chini ya Ziwa Victoria ambazo zinapeleka umeme wa kiasi cha megawati 10 wilayani humo zikitokea Kisorya wilayani Bunda.

Waziri wa Nishati, January Makamba akitazama nguzo za umeme zilizobeba nyaya ambazo zimesimikwa chini ya ziwa Victoria ili kupeleka umeme kwenye kisiwa cha Ukerewe kutokea Bunda –Mara.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles