ACHANA na janga la Corona. Sahau uhalifu, hasa dhidi ya watu wenye asili ya Afrika. Pia, weka kando janga la uhaba wa ajira kwa vijana. Kwa sasa, kupanda kwa bei ya nyama ni mtihani mwingine mzito unaomkabili Rais wa Marekani, Joe Biden.
Si tu kumiliki gari, nyumba ya kifahari, bali pia kula nyama ya mbuzi au ya ng’ombe imeonekana kuwa ni anasa mpya kwa raia wengi wa nchi hiyo kubwa duniani.
Ukilinganisha na ilivyokuwa Desemba, mwaka jana, sasa bei ya nyama ya ng’ombe imepanda kwa asilimia 14. Nyama ya nguruwe nayo imekuwa ‘dili’ kwani bei yake imepanda kwa asilimia 12.1, huku nyama za ndege (kuku, bata n.k) ikipaa kwa asilimia 6.6.
“Nyama inapokuwa ghali kiasi hiki, hata ulaji wake unapungua,” anasema Shakeel Anjum (36), mmoja ya wauzaji wa nyama, akiongeza kuwa imefikia hatua wamiliki wa mabucha wamekuwa wakitumia fedha zao kufidia hasara. “Biashara imekwenda taratibu sana kwa kweli.”
Tatizo nini?
Katika hili la bei ya nyama kupanda, kampuni chache zilizopewa mamlaka ya kusambaza nyama nchini Marekani ndizo chanzo cha tatizo kwani zimekuwa zikipanga bei kwa namna zinavyotaka.
Kampuni kubwa nne zilizoshikilia uchakataji na usambazaji wa nyama nchini Marekani ni JBS, Cargill Meat Solutions, Tyson Foods na National Beef Packing Co, ambazo zinamiliki asilimia 55 hadi 85 ya bidhaa hizo sokoni.
Kampuni hizo zimepiga hatua kubwa katika utawala wa soko kwani mwaka 1970 na 1980 zilikuwa zikilimiki asilimia 25 hadi 35 tu.
“Ni kama anavyoamini muuzaji nyama mwingine, Shakeel, anaposema: “Wameungana na kupandisha bei, hatuna la kufanya, wao ndiyo wenye sauti.”
Wafugaji nao kilio
Wakati bei ya nyama ikiwa juu, ungetarajia iwe habari njema kwa wafugaji, Kwamba wangekuwa wakiingiza fedha za kutosha kwa kuuza mifugo yao. Hata hivyo, mambo ni tofauti.
Unaweza kuliona hilo kwa takwimu tu, zikionesha zaidi ya mashamba ya ufugaji 17,000 hufilisika kila mwaka nchini Marekani. Brett Kenzy (49), ni mfugaji anayeishi South Dakota akiwa na ng’ombe zaidi ya 3,000.
Anasema changamoto kubwa ni kwamba wadau wa nyama (kampuni za uchakataji na usambazaji) wameishusha kwa kiasi kikubwa bei ya mifugo, hali inayomtesa tangu mwaka 2015. “Imekuwa ngumu sana… Ngoja tuone, huenda ikapatikana suluhisho.”
Serikali inasemaje?
Julai, mwaka huu, Rais Biden aliidhinisha Dola milioni 500 ziwe ni mkopo kwa wajasirimali wa nyama, lengo likiwa ni kuibua ushindani dhidi ya kampuni chache hizo ili zishushe bei.
Aidha, utawala wake haujakaa kimya juu ya malalamiko yanayoendelea. Na badala yake, imeanza kuchukua hatua dhidi ya walioleta ‘janjajanja’ iliyosababisha bei ya nyama kupanda. Mathalan, ipo kampuni ya uchakataji wa nyama za kuku iliyoko katika Jimbo la Colorado, ambayo imetozwa faini ya Dola milioni 107.
Hata hivyo, kampuni hizo zimeibua manung’uniko zikidai Serikali haina uelewa wa kutosha juu ya soko la nyama na badala yake imekuwa ikiwatumia kama ‘mbuzi wa kafara’ katika hili la bei ya bidhaa hiyo kupanda.
Mkakati mwingine wa Rais Biden ni ahadi yake ya mwezi uliopita, aliposema Serikali itaongeza Dola bilioni 1.4 katika mikopo ya wajasiriamali wadogo (wafugaji, wachakataji wa nyama na wasambazaji) ili kuwanasua katika mkwamo wa janga la Corona.