Na Christina Gauluhanga, Dar Es Salaam
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imeshusha bei ya mafuta ya petroli kutokana na kushuka kwa bei yake katika soko la dunia.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Ewura, Felix Ngamlagosi, alisema wameamua kushusha bei za ndani kwa kuwa mafuta yameshuka kwa kiasi kikubwa katika soko la dunia.
Alisema bei za rejareja za mafuta ya aina zote, yaani petroli, dizeli na mafuta ya taa zimebadilika ikilinganishwa na toleo la Februari, mwaka huu.
“Bei hizi zitaanza kutumika kesho (leo), pamoja na kutambua bei kikomo za bidhaa mbalimbali za petroli nchi nzima,” alisema Ngamlagosi.
Alisema kuanzia mwezi huu, bei ya petroli itapungua kwa Sh 31 kwa lita sawa na asilimia 1.70, dizeli Sh 114 kwa lita sawa na asilimia 7.10 na mafuta ya taa Sh 234 sawa na asilimia 13.75.
“Ukilinganisha na mwezi uliopita, lita moja ya petroli ilikuwa ni Sh 34.36 sawa na asilimia 1.98, dizeli Sh 116.58 sawa na asilimia 7.80 na mafuta ya taa Sh 236.59 sawa na asilimia 14.84,” alisema.
Ngamlagosi alisema hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya bei za mafuta kwa Mkoa wa Tanga mwezi huu kutokana na kutopokea mafuta mapya kupitia Bandari ya Tanga mwezi uliopita.
Alisema kwa mujibu wa sheria ya mafuta ya mwaka 2015, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko ambapo Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei za kikomo za bidhaa za mafuta.
“Kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi tu bei hizo ziwe chini ya bei kikomo kama ilivyotafsiriwa na Ewura,” alisema Ngamlagosi.