25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

BEBETO WA 1994 KUANZA KAZI MSIMU UJAO

NA BADI MCHOMOLO


KUMEKUWA na aina mbalimbali za ushangiliaji viwanjani, hasa kwa wachezaji pale wanapofanikiwa kufunga bao, kila mmoja anakuwa na hisia tofauti na ndipo anapanga aina yake ya ushangiliaji.

Wapo ambao wananyonya kidole cha mkono baada ya kufunga bao, ikiwa ni sehemu yake ya furaha, sio kwamba anajisikia tu kunyonya, lakini hiyo ni kama salamu kwa familia yake na huku akiwajulisha mashabiki kuwa amefanikiwa kupata mtoto hivyo analea.

Mashabiki wengi wakiona mchezaji anashangilia kwa aina hiyo wanakuwa hawana maswali mengi, wanajua wazi kuwa mchezaji huyo amepata mtoto hivi karibuni. Wapo ambapo wanashangilia kwa kuufunika mpira na jezi tumboni, hii inaonesha kuwa mke wake ni mjamzito.

Aina hizo za ushangiliaji zimeanza miaka ya nyuma sana, huku nyingine zikiendelea kuzaliwa upya kila msimu. Aina ya pekee ambayo ilipendwa na watu wengi katika ulimwengu wa soka ilikuwa mwaka 1994, katika michuano ya 15 ya Kombe la Dunia, iliyofanyika nchini Marekani.

Katika michuano hiyo mabingwa walikuwa Brazil, huku nyota wa timu hiyo ya Taifa ambaye alikuwa anacheza nafasi ya ushambuliaji, Jose Roberto Gama de Oliveira, maarufu kwa jina la Bebeto alianzisha aina pekee ya ushangiliaji ya kumbeba mtoto mikononi.

Aina hiyo ya ushangiliaji ilitokea mara baada ya kuwa na furaha kutokana na kupachika mabao 2-0 dhidi ya Holland katika hatua ya robo fainali, lakini ushangiliaji huo ulikuwa gumzo kila kona kwa kuwa ulionekana kwa mara ya kwanza.

Kumbe siku hiyo ilikuwa ni siku ambaye mke wake alifanikiwa kujifungua mtoto wao wa tatu ambaye alimpa jina la Mattheus Oliveira, hivyo alikuwa anashangilia kwa aina hiyo ili ulimwengu ujue kuwa nyota huyo amepata mtoto wa tatu.

Leo hii ni miaka 23 tangu mtoto huyo ambaye alitambulishwa kwa aina ya pekee katika ushangiliaji, wengi ambao walishuhudia aina hiyo watakuwa na hamu ya kutaka kumuona mtoto huyo kama atakuwa na uwezo wa kucheza soka kama ilivyo kwa baba yake.

Kwa sasa Oliveira mwenye umri wa miaka 23, amekuwa na furaha kubwa kwa kuwa amefanikiwa kusaini mkataba wa kuitumikia klabu ya Sporting ambayo inashiriki Ligi Kuu nchini Ureno, baada ya kumalizana na klabu yake ya Estoril nchini humo.

Kiungo huyo alikuwa anawindwa na klabu mbalimbali barani Ulaya msimu huu kutokana na uwezo aliouonesha misimu miwili akiwa na klabu hiyo ya Estoril, lakini Sporting wameamua kumpa mkataba wa miaka mitano kwa kitita cha pauni milioni 51 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 146 za Kitanzania.

“Nimeamua kuichagua Sporting CP kutokana na ukubwa wa klabu, nina furaha kubwa sana  kupata nafasi hii na wala sikufikiria mara mbili kama nitapata nafasi kama hii. Kwa sababu ya historia ya timu pamoja na baadhi ya wachezaji ambao wamepita kwenye timu huu, hivyo na mimi nataka kuacha historia yangu hapa,” alisema mtoto huyo.

Hata hivyo kwa upande wa baba wa mtoto huyo (Bebeto), alitumia mtandao wa Twitter kuelezea hisia zake mara baada ya kupata taarifa kuwa amesaini miaka mitano ndani ya Sporting CP.

“Najivunia kuwa na wewe mwanangu, hivyo unatakiwa kuendelea kujituma kwa nguvu pamoja na uvumilivu ili uzidi kwenda mbali zaidi ya hapo, ninaamini unaweza kuingia kwenye kitabu cha historia ya Sporting CP.

“Niliweka historia katika kuzaliwa kwako, hivyo huu ni wakati wako wa kuwaonesha watu kuwa ni wewe ambaye ulitambulishwa kipindi cha mwaka 1994 katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Marekani,” alisema Bebeto.

Hata hivyo, Bebeto anaamini kuwa mtoto huyo atakuja na aina yake ya ushangiliaji ambayo itaweka historia katika maisha yake ya soka kama ilivyo yeye na anaamini atakuja kuyafanya makubwa sana katika ulimwengu wa soka.

Bebeto akiwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Brazil alifanikiwa kucheza jumla ya michezo 75 na kufanikiwa kuifungia mabao 39, huku akichukua Ubingwa wa Kombe la Dunia mara mbili 1994 na 1998, akiwa pamoja na Romario na baadaye akiwa na Ronaldo.

Aliweza kupata medali mwaka 1988 na 1996 kwenye michuano ya Olimpiki pamoja na 1989 kwenye michuano ya Copa America.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles