Sharifa Mmasi, Mtanzania Digital
CHAMA cha Mpira wa Kikapu Zanzibar (BAZA), kimesikitishwa na uamuzi wa Waziri wa wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita aliyoiotoa Septemba 4, mwaka huu katika ukumbi wa Redio Raha leo visiwani humo, baada ya kusema anataka kuuvunja uongozi huo wa kikapu kwa mamlaka aliyonayo.
Waziri huyo ametoa sababu yakutaka kuvunja uongozi wa BAZA akidai kuwa, kwa mujibu wa katiba yao ibara ya 47 (2) inasema kwamba, uongozi huo wa kikapu unapaswa kufanya uchaguzi wake kila baada ya miaka minne hivyo ulitakiwa kufanyika tangu mwaka jana lakini haikuwa hivyo.
Amesema uongozi huo hauna uhalali wa kuendelea kuwa madarakani kwa sasa na kusisitiza kuwaondoa katika majukumu hayo.
Baada ya Baza kuzinasa tariifa hizo, imekuwa na msimamo wao na kueleza kuwa, bado ni viongozi wa kikapu Zanzibar kwa mujibu wa Katiba yao ya mrajisi wa Baraza la Michezo Visiwani huko (BMTZ).
Baza imedai kuwa, Waziri Tabia ametoa uoamuzi huo kutokana na mihemko, ushawishi, jazba pamoja na kutozingatia vyombo alivyovipa mamlaka ya kusimamia sekta hiyo ya michezo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baza, Ramadhan Khamis Salmin, ameeleza kuwa, Waziri Tabia alinukuu ibara ya 47 ya katiba yao bila kuangalia ibara nyingine ya 35 (3) iliyoupa mamlaka mkutano mkuu wa chama hicho cha mpira wa kikapu kuongezea muda uongozi uliopo madarakani jambo ambalo lilishafanyika Julai 24,2021 na mrajisi alijiridhisha na uhalali wa hatua hiyo.
Ameongezea kuwa, wanaamini wanawajibika na mkutano mkuu ambao umewaweka madarakani.