WATU 12 wamefariki dunia papo hapo na wengine 19 kujeruhiwa, baada ya basi la Kampuni ya Takbir kugongana na lori la mafuta katika Kijiji cha Kizonzo, Shelui Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Ajali hiyo ilitokea katika barabara kuu ya Dar es Salaam – Mwanza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 1.30 usiku wakati basi hilo lilipokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Geita.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori, Charles Kayene ambaye baada ya ajali hiyo alitoroka na anatafutwa na polisi.
“Dereva huyo alikuwa akiendesha lori ya Scania namba T 230 BRJ.
“Kabla ya ajali dereva huyo alikuwa akitaka kuyapita magari mengine lakini kwa bahati mbaya alipoteza mwelekeo na kusababisha ajali hiyo.
“Lori hilo lilikuwa na tela namba T 314 CTS lililokuwa likitoka Mwanza kwenda Dar es Salaam,” alisema Kamanda Sedoyeka.
Alisema hadi sasa waliofariki dunia hawajatambuliwa na wala haijulikani mahali walikokua wakienda, ingawa basi hilo husafiri kati ya Dar es Salaam na Geita.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Dk. Timoth Sumbe, alisema walipokea maiti 12 na majeruhi 19.
Alisema kwa kuwa hospitali hiyo haina chumba kikubwa cha kuhifadhi maiti, baadhi ya maiti ilisafirishwa kwenda kuhifadhiwa Hospitali ya Mkoa wa Singida.
Alisema majeruhi watano wako katika hali mbaya na wanatarajia kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa Bugando mkoani Mwanza kwa matibabu zaidi.
Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Oscar Uzengi, aliiambia MTANZANIA kuwa mwendo wa basi lao ulibadilika na kuwa wa kasi baada ya dereva wa pili wa basi hilo kuliendesha walipofika Singida.
Alisema walianza safari Dar es Salaam katika hali ya kawaida ingawa walikamatwa na polisi wa usalama barabarani baada ya kufika Singida.
“Mimi nilikuwa nimekaa viti vya mbele nilikuwa nikiona mwendo wa gari ukiwa wa kawaida ingawa tulipofika Singida tulikamatwa na trafiki.
“Baadaye aliingia dereva mwingine na hapo ndipo mwendo ulianza kuwa wa kasi na kuwafanya baadhi ya abiria wakawa wanalalamika kwa sauti za chini chini.
“Kwa bahati mbaya haukupita muda mrefu ndipo ajali ikatokea na kusababisha madhara haya,” alisema abiria huyo.