33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Bashungwa amsweka ndani mkandarasi daraja Mpijichini

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Waziri wa Ujenzi, Inocent Bashungwa ameagiza kukamatwa kwa mkandarasi anayejenga Daraja la Mpijichini lililopo Wilaya ya Kinondoni kutokana na kuchelewesha kazi.

Mkandarasi huyo Panjianguang wa Kampuni ya China Railway Seventh Group (CRSG), anadaiwa kuchelewesha ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 140 na barabara unganishi kilomita 2.3.

Akizungumza leo Aprili 30,2024 baada ya kufanya ziara kukagua miundombinu iliyoharibiwa na mvua, Bashungwa amesema mkandarasi huyo ni mbabaishaji kwani amepewa kazi maeneo mbalimbali ya nchi lakini amevurunda.

“Huyu mmemtoa wapi, kwenye mkataba ‘Works manager’ nani ni incharge…yuko likizo wakati wana Mbweni na Bagamoyo wanahitaji ujenzi wa barabara…Site Agent ameenda China.

“Huyu ni mbabaishaji OCD nenda naye akatoe maelezo na sisi tukatoe maelezo, nataka mtendaji mkuu wa kampuni hii aje ofisini. Huu ni mradi wa tano hatuwezi kubembelezana lazima tuchukue hatua,” amesema Bashungwa.

Meneja Mradi wa Kampuni ya China Railway Seventh Group (CRSG) akiwa mikononi mwa polisi baada ya Waziri wa Ujenzi, Inocent Bashungwa, kuagiza akamatwe.

Ameitaja miradi mingine ambayo mkandarasi huyo amevurunda ni pamoja na Barabara ya Sanzate – Nata mkoani Mara, Kibaoni – Mlele (Katavi) ambako alikuta magari 150 yameegeshwa huku yote yakiwa mabovu na Amani Mahoro – Luhanda mkoani Ruvuma.

Waziri huyo amesema kama mkandarasi huyo akishindwa watachukua hatua za kisheria kuhakikisha wanapata mwingine wa kulijenga daraja hilo.

Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam, John Mkumbo, amesema bado mkandarasi huyo hajamaliza kuweka mitambo ambapo amefikia asilimia 58 huku wafanyakazi muhimu akiwa nao sita badala ya 10 wanaotakiwa.

Waziri Bashungwa amesema pia barabara inayoanzia katika daraja hilo kuelekea Mingoi iko Tarura lakini itapandishwa hadhi na kupelekwa Tanroad ili ijengwe kwa viwango vinavyotakiwa.

Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa amesema wako kwenye hatua ya kumpata mkandarasi ili Barabara ya Mwai Kibaki ijengwe njia nne ambapo pia itatoa matoleo ya kujenga njia ya mwendokasi.

Aidha amemuelekeza mkurugenzi wa Matengenezo Tanroads kutenga bajeti maalumu kutengeneza Barabara ya Bunju B – Mpigi Magohe – Mbezi kwa kiwango cha Changarawe na baada ya mvua kuisha itajengwa kwa kiwango cha lami.

Waziri wa Ujenzi, Inocent Bashungwa (Kushoto), akipita katika daraja la muda la Mpijichini baada ya kufanya ziara kukagua miundombinu iliyoharibiwa na mvua.

Nao wananchi wa Mabwepande wamesema hawana hata kilomita moja ya lami na kuiomba Serikali kuwajengea ikiwemo Barabara inayounganisha maeneo ya Buju B na Mbezi Louis.

Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge, amesema wametenga asilimia 10 kupitia mapato ya ndani ili kuendelea kuchangia matengenezo ya barabara za halmashauri hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles