30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

BASHIRU: SIWEZI KUCHAMBUA TENA, MNATAKA NIFUKUZWE

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana (kushoto) akiagana na Katibu Mkuu mpya Dk. Bashiru Ali (kulia) na wanachama wengine baada ya kumkabidhi ofisi jijini Dar es Salaam jana. | PICHA SILVAN KIWALE

ELIZABETH HOMBO Na EVANS MAGEGE-DAR ES SALAAM       |       


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho ilimteua, hivyo inaweza pia kumfukuza endapo atakwenda kinyume na maamuzi ya vikao.

Kutokana na hilo, amesema msimamo wake kuhusu Katiba Mpya, kwa sasa utakuwa tofauti na ule aliokuwa nao awali kabla ya kuingia rasmi kwenye siasa za CCM. Kwamba sasa ataendana na maelekezo ya chama hicho tawala.

Hayo aliyesema jana baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana katika Ofisi ndogo ya CCM Lumumba, Dar es Salaam.

Akijibu swali aliloulizwa na gazeti hili, alisema: “Leo nazungumza kama Katibu Mkuu (anacheka) …unaelewa eh! Kwahiyo swali hilo lina majibu humo humo na umenirahisishia, nikiwa mchambuzi ninachambua kwelikweli, ukiwa msemaji wa chama unawasilisha yaliyoamuliwa na vikao.

“Kwahiyo, msimamo wa kikao cha Halmashauri Kuu ni chombo kimeniteua na kinaweza kunifukuza, kwenye uchambuzi kule nisingefukuzwa, hapa bwana kama unanitakia mema siwezi kuchambua yale ambayo hayajaamuliwa na vikao.”

Msomi huyo aliyebobea kwenye uchambuzi wa sayansi ya siasa, alisema anaamini endapo vyama vya siasa vitaheshimu kazi zao na zile za Serikali, wanaweza kujadili namna ya kurekebisha katiba hizo.

“Lakini jambo kubwa ni kwamba nchi hii kama tutaheshimu katiba za vyama vyetu zilizopo na katiba za Serikali zetu mbili zilizopo, tunaweza tukaanzia hapo kujadili namna ya kurekebisha katiba hizo.

“Kwahiyo msisitizo wangu ndivyo nilivyosema na nakushuruku sana Humphrey (Humphrey Polepole) ulininukuu vizuri na gazeti la MTANZANIA nalo likaninukuu vizuri.

“Nilisema mimi ni mtiifu wa katiba ya chama na nitakuwa mtiifu kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na nitakuwa mtiifu kwa historia ya mapambano ya ukombozi wa taifa hili,” alisema Dk. Bashiru.

 

SIASA ZA MAJUKWAANI

Alipoulizwa kuhusu uchanga wake katika siasa za majukwaani, alisema hataonekana kwenye majukwaa kwa sababu wapo waliopewa dhamana hiyo na kwamba kazi yake ni kubuni mikakati.

“Kazi niliyopewa si siasa za majukwaani, siasa za majukwaani ni mwenyekiti wa chama akisaidiwa na makamu wake wawili, kule mikoani kuna wenyeviti wa vyama na wa wilaya, tuna wabunge na madiwani.

“Na ni marufuku kwa mtendaji kufanya kazi ya mwanasiasa, kazi ya kupiga siasa safi, lakini ni wale waliochaguliwa kwa miaka mitano mitano, sisi ni watendaji, tunaweza kukaa saa moja, mwaka mmoja.

“Kwahiyo kama mtendaji hamtaniona kwenye majukwaa kwa sababu wapo waliopewa dhamana ya kukaa kwenye majukwaa, kazi yangu mimi ni kubuni mikakati, kazi yangu mimi ni kutoa taarifa kwenye kikao, kazi yangu mimi ni kusimamia maelekezo ya chama, hayo si masuala ya jukwaani, ni masuala ya mezani,” alisema.

UANACHAMA WAKE CCM

Alipoulizwa kuhusu siku aliyojiunga na CCM, alisema amepewa kazi hiyo akiwa ni mwanachama wa chama hicho tawala.

“Hilo swali la vikao. Ukitaka kujiunga CCM unajiunga kwa vikao, unakwenda kwenye tawi, na hilo ni swali la kitafiti, kama mwanahabari tafuta nilijiunga wapi, ili uwe mwanachama lazima uende kwenye tawi.

“Nakushawishi kabisa nenda kafanye utafiti utajua tawi gani nimejiunga, nimepata kadi lini, ninachokuhakikishia nimepewa kazi hii nikiwa mwanachama wa CCM,” alisema Dk. Bashiru.

 

KUINGIA MSITUNI

Alisema miaka yote alikuwa mchambuzi wa sayansi ya siasa, lakini sasa atalazimika kuingia msituni kujifunza namna gani ataweza akazungumza kama mzungumzaji wa chombo cha utendaji cha chama.

“Katika tasnia ya taaluma, sasa nafungua ukurasa mpya wa kuendeleza urafiki huo katika eneo la utendaji katika chama kinachotawala nchi yetu.

“Leo nimekabidhiwa ofisi rasmi na rafiki yangu Komredi Abdul, wengine wanamwita Abdlurahman Kinana, lakini mimi namwita Abdul kwa sababu ni rafiki yangu wa muda mrefu sana.

“Kama alivyosema, amefanya kazi hiyo ya kunitambulisha kwa watumishi wenzangu, pili amenikabidhi vitendea kazi ambavyo vinahitaji muda wa kuvisoma na tatu ni kunipongeza kwa kuteuliwa kwa vigelegele na nderemo na kikao cha juu cha maamuzi cha Halmashauri Kuu.

“Kwahiyo tumemaliza zoezi hilo, itabidi baadaye nijifunze, Humphrey (Polepole) yeye ni mwenyeji kidogo, anifundishe hata namna ya kuzungumza na vyombo vya habari masuala ya siasa ya chama tawala.

“Mimi nilikuwa tu ni mchambuzi napiga nondo za sayansi ya siasa, sasa lazima niingie msituni kujifunza namna gani naweza nikazungumza kama mzungumzaji wa chombo cha utendaji cha chama, kwahiyo nawaomba mniwie radhi, leo (jana) sina cha kuwaeleza zaidi ya kuwashukuru.

“Na mambo mengine nawaahidi ushirikiano mkubwa, tunayo idara maalumu ya kutuunganisha sisi na umma, kupitia vyombo vya habari na njia zingine.

“Matarajio yangu ni kwamba mtatukosoa, lakini kwa nia ya kujenga, mtatushauri na mtatuhoji kuhitaji ufafanuzi kwa sababu chama hiki ni chama kinachotawala nchi hii.

“Hivyo kuna sababu ya kutoa ufafanuzi wa namna kinavyotoa uongozi kwa nchi, kwahiyo watendaji wangu wote wapo na wakuu wa idara wamesikia, kwamba tuna wajibu wa kushirikiana na vyombo vya habari ili watuunganishe na umma,” alisema.

 

VIPAUMBELE

Akizungumzia kuhusu vipaumbele vyake, alisema ataanzia pale ilipoishia kwa sababu vipo ndani ya nyenzo aliyokabidhiwa.

“Ilani ya chama hiki nimekikuta karibu kiko katikati ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, kwahiyo naanzia hapo hapo, kwa mfano mwaka 1995 wakati tunaanza mfumo wa vyama vingi, CCM kiliahidi kufanya utaratibu wa haraka kuhamia Dodoma.

“Lakini miaka hiyo haikuwezekana na mwaka 2015 tumeanza, kwahiyo hicho nacho ni kipaumbele cha utekelezaji wa ahadi tunazozitoa. Nasikia kuna watu wanasema haipo kwenye ilani, wakasome ilani ya CCM, jambo lile tumelipanga tangu mwaka 1995,” alisema.

 

NIDHAMU KWA WATENDAJI

“Nidhamu ni dhana inayohusiana na uwajibikaji na ni tamaduni nzuri sana kwa taasisi yoyote, kwahiyo kama mtendaji, mwenyekiti wa sekretarieti wa Halmashauri Kuu ya CCM, nadhani jukumu langu kubwa ni kuhakikisha kwamba utendaji kwa maana ya utekelezaji wa maazimio ya vikao vya chama unaenda kama ilivyokubaliwa.

“Usipopindisha na ukafanya kwa ufanisi ndiyo nidhamu yenyewe, usipopotosha ndiyo nidhamu yenyewe, ukitii maagizo yale ndiyo nidhamu yenyewe, ukifafanua vizuri kwa ufasaha ndiyo nidhamu yenyewe.

“Kwahiyo mambo matatu katika sekretarieti nimeshawaeleza. Kwanza; bidii ya kazi ambayo nayo inahitaji nidhamu pia. Pili; maarifa ya kutenda kazi hiyo. Nimewaomba sana tuendelee kujifunza na mimi mwenyewe nimeanza kazi ya kujifunza. Tatu; ni nidhamu ninayoisema ya uwajibikaji, ni sehemu ya majukumu yetu tuliyokabidhiwa,” alisema.

 

KINANA ANENA

Kwa upande wake, Katibu Mkuu aliyestaafu, Kinana, aliwaomba watendaji wa chama hicho kumpa ushirikiano Dk. Bashiru.

“Nimekuja ofisini kwa mambo matatu; kwanza kumpongeza Dk. Bashiru kwa kuteuliwa kuwa katibu mkuu, pili nimemkabidhi ofisi na tatu nimemtambulisha kwa watendaji kazi zilizokuwa zinafanyika na nimewaomba wampe ushirikiano na ninyi waandishi wa habari naomba mpeni ushirikiano kama mlivyokuwa mnanipa mimi,” alisema Kinana.

Dk. Bashiru aliteuliwa Jumanne ya wiki hii na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kilichokaa kwa siku mbili Ikulu, Dar es Salaam.

Msomi huyo aliyeongoza tume ya kuchunguza mali za CCM, amerithi mikoba ya Kinana ambaye aliomba kujiuzulu nafasi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,896FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles