BASHIRU ATAKA WASIOENDELEZA ARDHI WANYANG’ANYWE

0
803

Na Ramadhan Libenanga, Morogoro

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema katika uongozi wake hayuko tayari kuona kikundi cha watu wachache wenye fedha wanajilimbikizia ardhi huku wananchi wenye kipato cha chini wakiendelea kupigana na wafugaji kwa sababu ya ufinyu wa ardhi.

Kutokana na hali hiyo, alisema ataiagiza Serikali kuyapoka maeneo hayo kutoka kwa watu hao na kuwapa wananchi ili kumaliza migogoro ya ardhi inayosababisha wananchi wengi kupoteza maisha na kupata vilema vya kudumu.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani hapa jana, alisema Morogoro ni moja ya mkoa wenye migogoro mingi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji huku baadhi ya watu wakimiliki maeneo mengi bila kuyaendeleza.

“Siko tayari kuona familia nyingi za kimasikini zikiendelea kunyanyasika na matukio ya aina hiyo,” alisema

Katika hatua nyingine, alisema wananchi wengi wamekuwa wakinyanyasika katika kudai haki zao za msingi kutokana na kukithiri kwa matukio ya rushwa kwa watumishi serikalini.

Alisema CCM mpya inataka viongozi bora na si bora viongozi hivyo ni jukumu lao kuhakikisha matukio yote yenye lengo la kudhulumu haki za wananchi yanakwisha.

Pia alisema viongozi, watumishi ndani ya chama hicho na serikalini watakaoshindwa kuhudumia wananchi wajiondoe mara moja ili kuwapisha wenye kufuata na kutekeleza ilani ya CCM.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here