Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally amewataka wasanii kumuenzi hayati baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa vitendo kwa kuyaenzi mambo matatu ikiwamo Muungano.
Akizungumza katika kongamano la Sanaa la Mwalimu Nyerere lililoandaliwa na wasanii jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Novemba 15, ameyataja mambo mengine kuwa ni lugha ya Kiswahili na Azimio la Arusha.
“Napenda niwakumbushe mambo matatu muhimu kwa wasanii la kwanza ni Muungano wetu na wasanii wana mchango mkubwa katika hilo kujifunza na kuuelewea historia na kuasisiwa kwake, kuudumisha na kuulinda, la pili lugha ya Kiswahili kukuza na kuilinda na katika hili tunafanya vizuri nimpongeze waziri.
“La tatu ni Azimio la Arusha hili sasa kwa sababu liliweka misingi ya usawa haki na kutukumbusha kuwa sisi hatuna wajomba na tunapaswa kujitegemea kama mnamkumbuka mwalimu mnapaswa pia kuyakumbuka haya muungano, na utaifa wetu.
“Naleta salamu za mwenyekiti wetu wa chama, salamu ambazo ananipa kila mara ninapokuwa kwenye shughuli za siasa anasema anawapenda sana hatawaangusha endeleeni kumuombea na kuliombea taifa.
“Niwashukuru kwa kuandaa tamasha hili ambalo ni muhimu sana katika taifa letu kama mtakumbuka mwaka huu wote wa 2019 umekuwa muhimu kwa kukumbuka miaka 20 ya kumbukumbu ya baba wa taifa maisha ya mwalimu na fikra zake na kila mwaka kunakuwa na shamra zaidi kuliko mwaka uliotangulia, na kwa wasanii hili ni jukumu lenu kwa sababu klwa mujibu wa mwalimu sanaa ni roho ya taifa,” amesema.