25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Bashir kuachia ngazi 2020 Sudan

alKHARTOUM, SUDAN

RAIS Omar al-Bashir ametangaza kuondoka madarakani ifikapo mwaka 2020 wakati muhula wake wa sasa utakapomalizika.

Bashir pia amekanusha tuhuma kuwa wanajeshi wake wamekuwa wakitekeleza dhuluma kwenye vita vipya dhidi ya wanavijiji weusi katika eneo la Darfur, magharibi mwa Sudan.

Kiongozi huyo anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) kwa tuhuma za kutekeleza mauaji ya halaiki na uhalifu wa kivita eneo hilo.

Bashir ambaye yu madarakani tangu mwaka 1989, alishinda Uchaguzi Mkuu wa Aprili mwaka jana kwa kupata asilimia 98 ya kura, lakini ukasuswa na wapinzani.

Akizungumza na mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Thomas Fessy, Bashir alisema kwamba kazi yake ‘inachosha’ na hivyo muhula wake wa sasa utakuwa wa mwisho.

“Mwaka 2020, kutakuwa na rais mpya na mimi nitakuwa rais wa zamani,” alisema.

Hata hivyo, mwandishi huyo amesema kuwa wakosoaji wake watasema kuwa awali aliahidi kung’atuka, lakini baadaye akakosa kutimiza ahadi hiyo.

Umoja wa Mataifa (UN) umesema zaidi ya watu milioni 2.5 wamefurushwa makwao katika eneo la Darfur tangu mwaka 2003, huku 100,000 wakiyakimbia makazi mwaka huu pekee.

Rais Bashir amesema hakuna haja ya kuwa na walinda amani wa UN wala wafanyakazi wa misaada eneo la Darfur.

Amekana taarifa za kutekelezwa kwa dhuluma zaidi maeneo ya milima ya Jebel Marra ambako wanajeshi wa Serikali walianzisha operesheni Januari mwaka huu.

“Madai haya yote hayana msingi, ripoti hizo zote hazina ukweli.

“Namtaka yeyote azuru vijiji vilivyotekwa na wanajeshi, na wanionyeshe walau kijiji kimoja ambacho kimeteketezwa. Kusema kweli, hakujakuwa na mashambulio yoyote ya kutoka angani,” alisema.

Rais huyo alisema wote waliotoroka mapigano walikimbilia maeneo yanayodhibitiwa na Serikali na kwamba hiyo ni ishara tosha kuwa hawashambulii raia.

Pia alisema makadirio ya UN kwamba zaidi ya watu 100,000 wametoroka makwao eneo la Darfur tangu Januari kwa sababu ya mapigano ‘yametiwa chumvi na si ya kweli.’

Aidha alisema makadirio ya UN kwamba watu milioni 2.5 milioni wanaishi kambini eneo la Darfur si ya kweli na kwamba idadi halisi ni watu karibu 160,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles