BASHE AITAKA NEC ITENDE HAKI

0
1173

Na MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAMMbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutenda haki ili uchaguzi wa Septemba 16 uwe wa haki na upinzani wasipate sababu ya kufanya vurugu.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni katika Jimbo la Ukonga, uliofanyika jana Mziga Mwanagati,  ambapo alisema CCM kimejipanga hivyo ni vyema NEC wakatenda haki.

Pia aliviomba vyombo vya ulinzi na usalama kutoa ulinzi wa kutosha kwa mgombea Ubunge wa Chadema, Asia Msangi kwani amesikia watu wa chama chake wakidai kuwa mgombea wao anataka kutekwa.

“Nimesikia hoja kuwa CCM wanataka kumteka mgombea wao,vyombo vya ulinzi naomba mtoe ulinzi huyu dada kuanzi nyumbani kwake, kwenye gari na kwenye kampeni ili isije ikafika mahali wakaanza kusema ametekwa,” alisema Bashe.

Alisema siyo vyema kupuuza maneno yanayosemwa kwani wakati wa uchaguzi wa Uchaguzi Mdogo wa Kinondoni walipuuza yakatokea maafa.

Bashe pia alitaka viongozi wa upinzani kuacha kusema kuwa wanaohamia CCM wamenunuliwa kwani kuna wengi wamehama chama tawala na kwenda upinzani lakini lakini hakuna aliyesema amenunuliwa.

Alisema kati ya waliowahi kuhama upinzani ni pamoja na mgombea wa CCM wa jimbo hilo, Mwita Waitara, mgombea wao wa Monduli, Julius Kalanga na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa.

“Naomba wapinzani watuambie waliwapa Sh ngapi hawa? Vyama vya siasa ni sawa na gari unapanda likupeleke mahali, ukiona halikufikishi unashuka, ndivyo alivyofanya Waitara.

“Kwasasa CCM ndio chama pekee chenye demokrsia, kinaruhusu kukosoana, mnazungumza hapa na Waziri Mkuu yupo, huko kwao hakuna hayo mambo ni zidumu fikrza za mwenyekiti kwa hiyo naomba waangalie nyumba yao waache haya mambo ya kusema watu wamenunuliwa,” alisema Bashe.

Kwa upande wake Mbunge wa Mtera, Livingston Lusinde, alisema tatizo la upinzani wakipelekewa ulinzi wanasema CCM imewapelekea mashushushu.

Kwa upande wake Waitara, alisema wakati akiwa mbunge kupitia Chadema, mgombea wa sasa wa Chadema alikuwa akimuhujumu.

“Wao walikuwa wanaangia mipango ya 2020, nimelalamika kwa viongozi wote lakini hakuna hatua iliyochukuliwa, nikaamua kuondoka,” alisema Waitara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here