26.1 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

Basata yaupinga wimbo wa Ney wa Mitego

neyHERIETH FAUSTINE NA CHRISTOPHER MSEKENA

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limesema kutokana na wadau wengi wa muziki kupinga wimbo mpya wa ‘Shika adabu yako’ wa mwana hip hop, Emmanuel Elibariki, ‘Ney wa Mitego’, wimbo huo umejifungia wenyewe na hawatarajii chombo chochote cha habari kuupa nafasi ya kusikika kwa jamii.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Godfrey Mngereza, alisema wimbo huo haufai na umejifungia wenyewe kutokana na kuwa na matamshi ya udhalilishaji kwa watu waliotajwa katika wimbo huo.
“Jamii imeshaukataa, hivyo BASATA hatutegemei vyombo vya habari vikiupiga wimbo huo ama kuuandika vizuri wimbo huo kutokana na kutokufaa kwa jamii.

“Ni wimbo usiofaa, Ney tunamjua, ni msanii ambaye hata unashindwa kumpima ana akili ya namna gani anapoandika mistari yake, sijui huwa anafikiria nini,” alisema Mngereza.
Hata hivyo, Ney kupitia akaunti yake ya Instagram ameandika kwamba waliosemwa kwenye huo wimbo ndio wameufungia kwenye masikio yao na si BASATA.

“Pale unaposikia eti kuna wasiopenda kuambiwa ukweli wamezusha eti wimbo wa Shika Adabu Yako umefungiwa na Basata, wimbo haujafungiwa, ila wenye makundi kwenye mitandao waliochanwa ndio wameufungia kwenye masikio yao kwa sababu hawataki kusikia ukweli, wameandika habari za kufungiwa. Hata ingekuwa kweli umefungiwa wamechelewa sana, sababu mpaka panya wanaujua,’’ alimaliza kwa majigambo Ney.

Katika hatua nyingine, Baraza hilo limekiri ugumu wa kuzuia video za muziki zisizo na maadili nchini kutokana na sekta ya sanaa kuwa na mwingiliano na taasisi nyingi za usimamizi na ufuatiliaji wa kazi za wasanii.
Mngereza alisema watu wengi wamekuwa wakilitupia lawama BASATA bila kujua jukumu la udhibiti wa video zisizo na maadili linahitaji ushirikiano na taasisi nyingi zisizoingiliana kisheria.

“Sisi BASATA tumejitahidi kwa nafasi yetu kuzuia video chafu zisionyeshwe kwa mujibu wa sheria za Baraza, lakini kuna changamoto kubwa kulimaliza tatizo hili kwa sababu sekta hii inahusisha taasisi nyingi ambazo haziingiliani kisheria, ndiyo maana inakuwa ngumu kulimaliza kabisa,” alisema Mngereza.

Aliongeza kuwa, licha ya changamoto hizo, BASATA wamekuwa wakitimiza jukumu la kufungia baadhi ya kazi za wasanii hao na wakati mwingine huwashauri juu ya madhara ya video hizo kwa jamii inayowazunguka na wengi wao hawarudii.

Pia kuhusiana na video zisizo na maadili, Basata wanadai maelezo zaidi watakuwa nayo Bodi ya Filamu, kwa kuwa ndio wanaosimamia kazi za filamu pamoja na vitu vinavyohusiana na picha za video.
Hata hivyo, viongozi wa Bodi hiyo ya Filamu walipotafutwa kwa njia ya simu haikuwa na jibu la suala hilo, zaidi ya kumtaka mwandishi kufika ofisini kwao.

Katika uchunguzi uliofanywa na Mtanzania, umegundua kwamba wasanii wengi nchini kwa sasa hawajali kufungiwa kazi zao, wakisema wanatafuta soko la nje wanalodai linahitaji video za namna hiyo ndipo wapate maonyesho katika nchi hizo.

Wasanii hao hudai video za nyimbo zao zinapokamilika huzipeleka katika vituo vyenye majina makubwa vilivyopo katika nchi zilizoendelea kimuziki na zikifanikiwa kuchezwa huko husaidia kukuza na kutangaza muziki wao, hivyo hata kama zikifungiwa kuonyeshwa na vituo vya runinga vya nchini, huendelea kuchezwa na kutazamwa kupitia vituo hivyo, vikiwemo Trace, BET, Mtv Base na vingine vingi.

Pia Mtanzania imegundua kwamba baadhi ya wasanii hawana kauli kwa waongozaji wa video wa nje kwa vyovyote wanavyowashauri kufanya katika uandaaji wa video za nyimbo zao, kutokana na woga wa kukutana na waongozaji hao ambao wengi wao wamezoea kupiga picha za video za namna hiyo, lakini wapo pia wasanii wanaotaka video za namna hiyo wakidhani ndizo zitakazowatangaza zaidi kimataifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles