26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

BARUA YA KUMNUSURU MALASUSA  YASOMWA MAKANISANI

 

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


WAUMINI  wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),  Dayosisi ya Mashariki na Pwani(DMP),  walisomewa barua maalumu kuhusiana na suala  la Askofu wao, Dk. Alex Malasusa.

Kusomwa kwa barua hiyo jana kunatokana na kikao cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani kilichokutana Jumatano iliyopita.

Barua hiyo iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Godfrey Nkini, ilisomwa katika usharika mbalimbali za dayosisi hiyo wakati wa matangazo.

Kwa mujibu wa barua hiyo, washarika wametakiwa kufahamu kwamba Dk. Malasusa ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani na dayosisi itaendelea na umoja na mshikamano na askofu huyo katika kuongoza na kuihubiri injili ya Yesu Kristo.

“Halmashauri kuu inaendelea kulifuatilia jambo hili kwa makini. Washarika mnaombwa kuwa watulivu na kuliombea kanisa.

“Tunaombwa kutunza amani na umoja wa kanisa kama neno la Mungu linavyosema,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.

Askofu Malasusa, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini na Kati, Solomon Massangwa na Askofu wa Dayosisi ya Kusini Mashariki, Dk. Lucas Mbedule, wanatuhumiwa kwa usaliti kutokana na uamuzi wao wa kuzuia waraka wa Pasaka ulioandaliwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo usisomwe katika dayosisi wanazoziongoza.

Jumapili iliyopita Askofu Mbedule alilazimika kuomba radhi kutii maagizo ya Baraza la Maaskofu wa KKKT.

Waraka huo ulioandaliwa mwishoni mwa Machi mwaka huu, wiki moja kabla ya maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka, ulichambua masuala ya jamii, uchumi, maisha ya siasa, umuhimu wa katiba mpya na matukio yaliyo kinyume na kile walichokiita tunu na misingi ya taifa.

Licha ya barua hiyo ya kanisa kusomwa baadhi ya waumini walihoji hatua hiyo kutokana na kutosomwa na waraka wa kanisa wa Pasaka na badala yake wamesomewa barua ya kumkingia kifua Askofu Malasusa.

Hatua ya halmashauri kuu ya dayosisi hiyo imeonyesha kumkingia kifua kutokana na barua iliyoandaliwa na chombo hicho na ilisomwa jana.

Kwa mujibu wa nakala ya barua hiyo ambayo MTANZANIA imeipata, Halmashauri Kuu ya Dayosisi hiyo, imesema haikuwa na lengo la kupingana na maazimio ya Mkutano Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa  KKKT juu ya kusomwa kwa Waraka wa Pasaka.

Barua hiyo imesema maelekezo yote yaliyotolewa yamezingatiwa na imesisitiza kuwa umoja na mshikamano kwa Askofu Dk. Malasusa utaendelea katika kuongoza na kuihubiri Injili ya Yesu Kristo.

Chanzo cha kuaminika cha gazeti hili  kililionyesha nakala ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa DMP, Godfrey Nkini, iliyoelekezwa kusomwa katika ibada za dayosisi hiyo.

Barua hiyo ilieleza kuwa halmashauri hiyo ilikaa kikao Mei 2, mwaka huu na ilijadili na kujiridhisha kuhusu barua aliyoandikiwa Askofu Malasusa kuwa alikiuka mapatano yaliyotolewa na mkutano wa maaskofu wa KKKT.

“Halmashauri Kuu imetafakari kwa kina jambo hili na kujiridhisha kwamba: Haikuwa lengo la DMP kupingana na maazimio ya Mkutano wa Maaskofu daima. Maelekezo yote yaliyotolewa na KKKT Makao Makuu yamezingatiwa.

“Hata hivyo, Halmashauri Kuu imesikitishwa kwa jinsi suala zima lilivyotunzwa hadi kufikia vyombo vya habari na baadhi yao kupotosha ukweli wa suala zima,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Kuhusu Askofu Malasusa barua hiyo ilisisitiza: “Washirika mfahamu kwamba Malasusa ni Askofu wa DMP. Halmashauri inatoa pole nyingi kwa Baba Askofu na familia yake kwa usumbufu uliojitokeza. DMP itaendelea na umoja na mshikamano na Askofu Malasusa katika kuongoza na kuhubiri Injili ya Yesu Kristo.”

Pamoja na barua hiyo kutoa pole kwa washirika wote kutokana na kuumizwa kwao na taarifa za kuandikiwa barua Askofu Malasusa za kukiuka mapatano ya Baraza la Maaskofu, ilizodai haikuwa lengo la KKKT Makao Makuu kuwaumiza waumini wake, pia ilieleza inaendelea kulifuatilia jambo hilo kwa makini.

Pia barua hiyo iliwaelekeza washirika hao kuwa watulivu na kuliombea kanisa na kutunza amani na umoja.

Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili lilizipata na kuandika wiki iliyopita, zilisema uamuzi wa kumtenga Askofu Malasusa ulifikiwa na kikao cha Baraza la Maaskofu wapatao 25, lililoketi mjini Arusha, chini ya kiongozi wake ambaye ndiye mkuu wa kanisa hilo, Askofu Dk. Fredrick Shoo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles