BARCELONA, HISPANIA
MABINGWA wa Ligi Kuu nchini Hispania, Barcelona, wanakomaa na beki wao, Javier Mascherano, asiondoke kujiunga na beki mwenzake, Dani Alves, katika klabu ya Juventus.
Tayari beki wa pembeni wa klabu hiyo ya Barcelona, Alves amejiunga na mabingwa wa nchini Italia, Juventus, kwa mkataba wa miaka miwili hivyo Mascherano alikuwa anatarajia kuambatana na mchezaji huyo Juventus.
Mkurugenzi wa michezo klabu ya Barcelona, Ariedo Braida, amesema kwamba hakuna nafasi ya Mascherano kujiunga na klabu yoyote kwa sasa.
“Ni wazi kwamba, Mascherano hawezi kujiunga na Juventus kwa sasa, ataendelea kuwa mchezaji wetu msimu ujao, tunatarajia kufanya naye mazungumzo na ninaamini hawezi kuachana na sisi,” alisema Braida.
Inadaiwa kwamba, mchezaji huyo alidai kwamba anataka kuondoka kwenye klabu hiyo kutokana na kutochezeshwa katika nafasi ya kiungo kama ilivyo wakati anaitumikia Liverpool, wakati huo Barcelona walidai kwamba wanafanya hivyo kutokana na kukosa beki wa uhakika.