26.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

Baraza la Usalama laidhinisha mkataba wa kusitisha vita Libya

GENEVA, USWISI 

BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa limeidhinisha mkataba wa kusimamisha mapigano nchini Libya, huku likitoa wito kwa pande hasimu kuutekeleza kikamilifu.

Duru za kidiplomasia zinaeleza kuwa azimio kuhusu Libya linatarajiwa kupitishwa na baraza hilo siku zijazo.

Taarifa ya pamoja ya baraza hilo imepongeza mkataba wa kusitisha mapigano nchini Libya uliotiwa saini mjini Geneva, Uswisi.

Umoja wa Mataifa umezihimiza pande hizo kuonyesha nia katika kutafuta suluhisho la kisiasa la mzozo kwenye vikao vitakavyoanza nchini Tunisia Desemba 9.

Taarifa hiyo ya Baraza la Usalama imekumbusha pia umuhimu wa kuheshimu marufuku ya silaha ya mwaka 2011.

Limeziomba pia nchi za nje na pande zinazohusika nchini Libya kujiepusha kujiingiza kati kwenye masuala ya ndani ya taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.

Oktoba 23, mwaka huu, pande hasimu nchini Libya zilitia saini mkataba wa kudumu wa kusitisha mapigano mjini Geneva, baada siku tano za mazungumzo chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa. 

Hatua hiyo inayolenga juhudi za kukomesha umwagikaji wa damu katika nchi hiyo iliyokumbwa na machafuko kwa takribani miaka kumi sasa ilipongezwa na Umoja wa Mataifa.

Mjumbe mwandamanizi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Libya, Stephanie Williams, aliyaita makubaliano hayo kuwa ya kihistoria baada ya mapigano ya miaka kadhaa yaliyoigawanya nchi hiyo pande mbili. 

Williams alisema makundi yenye silaha na vikosi vya kijeshi yamekubali kurejea kwenye kambi zao na kwamba makubaliano yaliyofikiwa yataanza kutekelezwa mara moja.

Pamoja na hatua nyingine, makubaliano hayo yanazingatia kuondolewa kwa mamluki wa kutoka nje na kuwezesha kufanyika mazungumzo mwezi ujao ili kutafuta suluhisho la kudumu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alisema makubaliano yaliyofikiwa ni muhimu sana, hata hivyo ameeleza kuwa juhudi zaidi zinahitajika.

Libya ilitumbukia katika vurumai baada ya nchi za NATO kuivamia mwaka 2011 na kumwondoa kiongozi wake kanali Muammar Gaddaffi aliyetawala kwa muda mrefu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,734FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles